Habari za Punde

Rais Dk Shein awataka Watanzania kujitathmini Uzalendo WaoSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dodoma                                   09.12.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Watanzania kujitathmini uzalendo wao kutokana na kushuka kwa kasi na ari ya uzalendo huku akisisitiza haja ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kutokana na jinsi anavyotekeleza uzalendo kwa vitendo.  

Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya Kampeni ya “Uzalendo na Utaifa”, iliyofanyika katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo kauli mbiu ya sherehe hizo mwaka huu ni ‘Uhuru wetu ni tunu, tuudumishe, tulinde rasilimali zetu, tuwe wazalendo, tukemee rushwa na uzembe”..

Katika hotuba yake Dk. Shein alitumia fursa hiyo akieleza maana ya mzalendo na uzalendo na kueleza kuwa mzalendo ni yule aliyezaliwa pahala fulani kwenye asili yake ambapo pia, ni mtu mwenye mapenzi ya dhati sana ya kuitumikia nchi yake na kueleza maana ya uzalendo kuwa ni hali ya mtu kuwa na nasaba ya asili ya nchi ambaye pia hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya nchi yake.

Alieleza kuwa kasi na ari na mwamko wa uzalendo imepungua kwani uzalendo ni vitendo na unapovitekeleza ndipo unapokuwa Mtanzania halisi na mzalendo halisi.

Aliongeza kuwa tangu kufanyika kwa uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar waasisi wa pande mbili hizo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Julius Kambarage Nyerere walifanya kazi kubwa ya kuwaandaa Watanzania kuwa wazalendo.

Dk. Shein alieleza kuwa uzalendo una muda mrefu na pia, ni jambo kogwe kwani uzalendo hutengenezwa na huwekewa mazingira mazuri ili wananchi wawe wazalendo kazi ambayo waliifanya waaasisi hao kwa kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika na kuwa Jamhuri ya Mungano wa  Tanzania, kazi ambayo ilikuwa ni ya kizalendo.

Alieleza kuwa viwango vya uzalendo vimekuwa vikitofautiana kwani baadhi ya Watanzania wanatofautiana kwani kuna baadhi yao wanapokwenda nchi za nje hujificha kutambuliwa kuwa wao ni Watanzania na kuukana Utanzania wao jambo ambalo linaonesha wazi kuwa hao si wazalendo.

Alieleza kuwa uzalendo huendelezwa na hufanywa kwa vitendo, kwani kumbukumbu zinaonesha kuwa mara baada ya uhuru Baba wa Taifa akisisistiza Uhuru na kazi ambapo hivi sasa kujitolea kumepungua ambapo Tanzania kuna utaratibu wa kupeana bahasha ama posho kwa kuwalipa watu hali ambayo haikuwepo kabla ya uhuru na hata Mapinduzi.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Wazanzibari walijenga nyumba za Michezani kwa kujitolea kutokana na uzalendo waliokuwa nao jambo ambalo limekuwa ni tofauti kwani hivi leo wapo wananchi wanaoisema Serikali na viongozi wa Serikiali kwa lugha zisizo nzuri, hivyo ni lazima Watanzania wajitathmini na kumuunga mkono Rais Magufuli ili jamii iendelee kuwa na uzalendo kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Dk. Shein alisema kuwa uzalendo ni kila kitu, hata utawala bora ni uzalendo kwani unapozungumza huwa unazungumziwa utawala wa sheria na lazima kila mmoja akipende chake cha Tanzania na kukumbusha msemo wa Marehemu mzee Karume kuwa “ Kithamini kilichochako mpaka usahau cha mwenzako”, alisema Dk. Shein.

Aliongeza kuwa uzalendo ni sehemu ya maisha hivyo ni lazima ufanywe kwa vitendo huku akisisitiza kuwafundisha watoto mila, desturi, maadili na uadilifu kwani malezi yamepungua kwa kiasi kikubwa hivi sasa.

Alieleza kuwa uzalendo unaanza nyumbani kumfunza mtoto katika familia kwani hapo zamani mtoto hulelewa na mtaa mzima na sio baba na mama peke yao jambo ambalo lilipelekea watoto kuwa na malezi mazuri na kuwakuza wakiwa wazalendo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumpongeza Makamo wa Rais kwa niaba ya Rais Magufuli kwa  kubuni jambo hilo ambalo ni muhimu sana na ipo haja ya kuungana apamoja katika kuhakaikisha Kampeni hiyo inafanikiwa kwa manufaa ya  Tanzania.

Akizungumzia kuhusu suala zima juu ya lugha ya Kiswahili, Dk. Shein alisisitiza haja ya kukizungumza na kukithamini Kiswahii na kueleza namna Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Mzee Karume walipoamua kukifanya kiswahili kuwa ni lugha ya taifa.

Aidha, Dk. Shein alimpongeza Rais Magufuli kwa kuwahimiza Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukizungumza kiswahili katika shughuli zao zote hasa kwa kufahamu kwamba lugha hiyo ina haiba kubwa, kwani ni lugha ya pwani iliyoanzia Zanzibar na kuenea katika ukanda wa Afrika Mashariki na hatimae duniani kote.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza haja kwa Watanzania kukiimarisha kiswahili kwani kuna baadhi ya wananchi wahaitendei haki lugha hiyo kwa kuizungumza visivyo.

Aliongeza kuwa kuna kila sababu ya kukizungumza Kiswahili na kukiendeleza ikiwa ni pamoja na kuyasoma na kuyafuatilia makkamusi ya Bara na Zanzibar ambayo yanatoa muongozo mzuri wa kiswahili huku akisisitiza kuwa hakuna mbadala wa uzalendo na wananchi wote wana asili ya Tanzania.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kuwashirikisha wasanii mbali mbali wakiwemo waimbaji wakongwe pamoja na wale wa kizazi kipya.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.