USIKU wa kuamkia leo ulikuwa ni wa kihistoria kwa timu ya
mpira wa miguu ya Taifa ya Zanzibar,’Zanzibar Heroes’ baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwazawadia viwanja vya kujenga nyumba pamoja
na fedha taslim Shilingi milioni tatu kwa kila mchezaji na kiongozi wa timu
hiyo.
Zawadi hizo alizitowa
katika tafrija maalum iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani
Kikwajuni mjini Zanzibar sambamba na taarab maalum aliyowaandalia timu hiyo
iliyotumbuizwa na kikundi cha Taifa cha
Taarab cha Zanzibar kufuatia kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu ya Vyama
vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ na kupata nafasi ya pili.
Viongozi mbali mbali
wa Serikali, vyama vya siasa, ZFA, na waalikwa wengine wakiwemo veterani walihudhuria
katika tafrija hiyo maalum ambayo Dk. Shein aliwaandaliwa wachezaji na viongozi
wa timu hiyo baada ya hapo juzi kuwaandaliwa chakula cha mchana katika viwanja
vya Ikulu mjini Zanzibar.
Dk. Shein alitoa
zawadi hiyo kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa hapo juzi huko katika viwanja vya
Ikulu mjini Zanzibar ambapo akitoa salamu zake na pongezi kwa wachezaji na
viongozi wa timu hiyo alikataa kuzitaja zawadi hizo na ambazo jumla yake
zilikuwa tatu na aliitaja ile ya taaraab tu na kusema mbili angezitaja hapo
jana.
Vigeregere, hoihoi na
nderemo zilisikika katika ukumbi huo kutoka kwa wachezaji na viongozi wa timu
hiyo pamoja na hadhara iliyohudhuria tafrija hiyo mara baada ya Rais Dk. Shein
kuzitangaza zawadi hizo ambazo kila mmoja alikuwa anasubiri kwa hamu kuzisikia.
Rais Dk. Shein
aliwakabidhi hundi ya Shilingi za Kitanzania milioni tatu kwa kila mchezaji na
viongozi ambao kwa ujumla wao ni 33 huku akiwaeleza kuwa kwa upande wa viwanja
watakabidhiwa si muda mrefu baada ya kukamilika hati zao na nyaraka nyengine
muhimu kutoka kwa Wizara husika ya Ardhi, Maji, Nishati na Mzingira.
Aidha, Dk. Shein aliwausia
wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuwa zawadi hiyo ya viwanja aliyowapa ni
muhimu wakaitunza na kuienzi na kubaki nayo na hatofurahi iwapo atatokezea mmoja
miongoni mwao na kuiuza kwani hilo sio lengo lake na yeye atajua kwa
atakaefanya hivyo.
Dk. Shein alieleza
kuwa hiyo walioipata wao ni bahati kubwa sana kwani wapo maveterani waliocheza
mpira wakati huo na kushinda mashindano mbali mbali lakini hawakupata zawadi
hizo ambazo zina umuhimu mkubwa katika maisha yao.
Mapema katika hutoba
yake Dk. Shein alisema kuwa timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes ilibezwa
sana na kuitwa majina mbali mbali
waliitwa wala urojo, wala ubuyu bila ya kuelewa kuwa hao waliowaita majina hayo
hawajui kuwa vyakula hivyo vina nguvu.
Aliongeza kuwa
kutokana na timu hiyo kuogopwa shutuma mbali mbali ilishutumiwa timu hiyo na
kueleza kuwa si jambo la rahisi timu ya Kenya wakatamani tena kukutana na ‘Zanzibar
Heroes’ katika fainali ya mashindano hayo yaliofanyika nchini Kenya.
Alisema kuwa kutokana
na timu hiyo kuonesha soka safi hivi sasa inaheshimiwa na kusisitiza kuwa
mchezo wa mpira hujenga udugu, maelewano na kuimarisha urafiki sambamba na
kutoa ajira.
Dk. Shein alitoa
historia ya mpira wa miguu hapa Zanzibar na kueleza kuwa ushindi huo haukuja
kwa bahati mbaya kwani Zanzibar ina historia kubwa ya soka tokea mwaka 1919
kulipoanzishwa timu ya ‘Kiungani School Team’ pamoja na makocha wa mpira wa
miguu na kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha michezo kwa vitendo
na si kwa maneno.
Aidha, aliitaka Wizara
ya Habari,Utalii, Utamaduni na Michezo kuongeza kasi ya kuongoza mpira na sio
kugombana wenyewe kwa wenyewe hadi kufikishana mahakamani kwani Wazanzibari
wanataka mpira na sio kwenda mahakamani
Pia, alikubali ombi
lililotolewa na Kocha wa timu hiyo Hemed Suleiman Moroko hapo juzi katika
viwanja vya Ikulu la kuomba kumualika nchini Rais wa Shirikisho la Soka Barani
Afrika Ahmad Ahmad kuja Zanzibar ili kufanya mazungumzo nae kwa ajili ya
kuzungumzia mustakbali wa Zanzibar katika soka kimataifa na kuahidi kufanya
hivyo kwa kiongozi huyo na viongozi wengine wa soko ulimwenguni.
Dk. Shein alitoa agizo
kwa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kuhakikisha ktimu hiyo
inapelekwa kisiwani Pemba kwa kutumia meli mpya ya MV Mapinduzi II ili wananchi
wa kisiwani humo wapate kuiona timu yao na kufurahi kwa pamoja.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawekeza katika timu
hiyo ili timu hiyo iwe bora na wachezaji waliopo wataongezwa ili kocha awe na
uwezo wa kuchagua.
Nae Kocha Mkuu wa timu
hiyo alitoa shukurani zake kubwa kwa Rais Dk. Shein kwa kuwazawadia zawadi hizo
ambazo ni za pekee na kumpa ahsante huku akieleza kwa niaba ya wenziwe kuwa
hawana cha kumlipa Rais Dk. Shein ila kumpa ahsante huku wakiahaidi kuwa
watahakikisha wanalipa deni kubwa walilonalo katika kuieletea Zanzibar ushindi.
Kikundi hicho cha
Taarab kilipiga nyimbo mbali mbali zikiqwemo za kuwasifu wachezaji hao pamoja
na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya
michezo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment