Habari za Punde

Skuli ya maandalizi kujengwa Kijiji cha Mtimbu Pujini

 Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Rashid Hadidi Rashid, akiangalia eneo linalotarajiwa na kujengwa Skuli ya Nasari ya huko katika kijiji cha Mtimbu Pujini.
Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Rashid Hadidi Rashid, akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Mtimbu Pujini , wakati ya ziara yake ya kuangalia changamoto zinazo wakabili Wananchi wa kijiji hicho.

PICHA NA JAMILA ABDALLA-MAELEZO PEMBA.Na/Jamila Abdallah - Maelezo. 

Serikali  ya wilaya Chake Chake , imesema  itahakikisha inasaidia na wananchi wa Kijiji cha Mtimbu Pujini katika kutatua changamoto ya elimu kwa kushirikiana nao katika ujenzi wa    Skuli ya maandalizi  kijijini hapo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Rashid Hadidi Rashid, alipokuwa akizungumza na Wananchi wa kijiji hicho juu ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwa ni miongoni  mwa ziara zake za kuonana na Wananchi katika shehia zao kuangalia mambo mbali mbali ya kimaendeleo.

Aliwataka wananchi wa kijiji cha Mtimbu Pujini  kuunganisha nguvu za pamoja katika kuimarisha maendeleo katika kijiji chao kwani maendeleo yao yataletwa na wao wenyewe.

Hadidi, alisema ni vyema wananchi kushirikiana  katika kujiletea maendeleo na kuachana na itikadi zao kwani maendeleo hayawezi kuletwa na mtu mmoja bila mashirikiano ya pamoja.

"Mashirikiano yapamoja ndio silaha pekee ya kuimarisha maendeleo  ,hebu kuweni tayari tuweze kutatua changamoto hizo hususan hii ya elimu", alisema   Hadidi.

Aidha  aliwahimiza wazazi kusimamia vyema masuala ya  elimu  kwa watoto wao kwani  elimu ndio mkombozi wao wa baadaye na wakumbuke kuwa hakuna urithi mzuri kama kumuachia mtoto Elimu.

Kwa upande wao ,Wananchi wa kijiji cha Mtimbu Pujini walisema mbali na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo wamekuwa  wakilalamikia kukithiri kwa watumiaji wa dawa za kulevya ambao huchangia wizi  na uharibifu wa mazao.      
Wananchi hao walisema kijiji cha Mtimbu sasa kimekuwa kukijitokeza vitendo viovu ambavyo awali vilikuwa havipo kutokana na vijana kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya.

Ali Kombo Masoud  mkaazi wa Kijiji hicho , alisema kijiji chao kimekuwa kikikabiliwa na changamoto nyingi, hivyo ameiomba Serikali ya Wilaya  kukisaidia kijiji  hicho ili kiweze kujiletea maendeleo na kuondosha changamoto  zinazowakabili .   

"Mtimbu ni kijiji kilichoko nyuma kimaendeleo hivyo tunaomba Serikali utusaidie ili tuweze kujikwamua kimaendeleo na sisi"alisema Masoud.

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba , amekuwa na kawaida ya kufanya ziara katika Shehia mbali mbali zilizomo ndani ya Wilaya hiyo kunagalia na kusikiliza kero zinawakabili Wananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.