Habari za Punde

Rais Dk Shein atoa pongezi kwa vikosi vya ulinzi kwa kushiriki kikamilifu katika sherehe za Mapinduzi


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                29.01.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameungana pamoja na Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi walioshiriki katika gwaride la kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula cha mchana alichowaandalia kutokana na ushiriki wao katika sherehe hizo zilizofanyika Januari 12 mwaka huu.

Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Unguja, na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na Makamanda wa Vikosi vya Ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shukrani zake Dk. Shein kwa Wapiganaji hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, alitoa pongezi kwa vikosi hivyo kwa kushiriki kikamilifu katika sherehe hizo kutokana na gwaride zuri ambalo lilikuwa kivutio kikubwa cha sherehe hizo zilizofanyika Januari 12, 2018 katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Waziri Gavu alitoa shukurani na pongezi za dhati kwa vikosi hivyo kwa kuazimisha kwa hali ya juu kilele cha miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ambazo zilifana kwa kiasi kikubwa.

Katika shukurani hizo, Waziri Gavu alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuwaandalia chakula cha mchana wahusika wote kwa kufanya kazi kwa pamoja na baadae kufurahi kwa pamoja kwa kula nao pamoja chakula cha mchana.

Waziri Gavu alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha wazi upendo mkubwa alionao Rais Dk. Shein kwa wananchi wake kwa kufanya kazi kwa pamoja na baadae kufurahi kwa pamoja hali ambayo imewapelekea vikosi hivyo kufarajika na hatua hiyo ya Rais.

Aidha, alivipongeza kwa dhati vyombo hivyo vya ulinzi kwa kutekeleza majukumu yote waliyopangiwa ikiwa ni pamoja na kuwalinda wananchi pamoja na mali zao sambamba na kuhakikisha amani na utulivu inaimarishwa hapa nchini.

Pamoja na hayo, Waziri Gavu alitoa wito kuendelea kuyalinda na kuyatunza Mapinduzi pamoja na kudumisha uzalendo.

Ni utamaduni aliouweka Dk. Shein wa kuwaandalia chakula cha mchana Vikosi vya Ulinzi vinavyoshiriki katika gwaride la sherehe za Mapinduzi pamoja na vijana na wanafunzi ambao nao hushiriki sherehe hizo kwa kila mwaka ambapo hapo jana aliwaandalia vijana na wanafunzi walioshiriki katika maadhimisho ya Sherehe za kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika eneo hilo la viwanja vya Makamo Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Unguja

Rajab Mkasaba, Ikulu

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.