Habari za Punde

Ufunguzi wa Bandari ya Mkokotoni Zanzibar

Na Khadija Khamis –Maelezo 03/01/2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed amewataka wafanyakazi wa shirika Bandari  Zanzibar kufanya kazi kwa bidii na kujenga uadilifu ili kuipatia pato serikali pamoja na kuleta maendeleo katika nchi.

Kauli hiyo ameieleza leo huko katika ufunguzi wa jengo la Ofisi ya Shirika la Bandari Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini  Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra ya sherehe ya miaka 54 ya Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar.

Alisema wafanyakazi  waweze kupambana katika kuhakikisha wanazuia rushwa na uingizaji wa biashara haramu jambo ambalo linaharibu nguvu kazi ya taifa na kuipunguzia pato serikali

“Lazima wafanyakazi wadhibiti kuvuja mapato kama hakuna mapato katika serikali na maendeleo hayapo na kipato hakiwi ikiwa kinatumiwa kwa ubadhirifu ” alisema Waziri .

Aidha alisema juhudi za serikali ni kutekeleza ilani ya chama ambayo inalengo la kuwaletea maendeleo mbali mbali wananchi wake bila ya upendeleo na kusimamia utekelezaji wa ahadi   jambo ambalo ndio malengo makuu ya Mapinduzi .

Alifahamisha serikali inatoa huduma kwa wananchi wote bila ya kuwa na ubaguzi wa rangi wala jinsia yoyote katika sekta mbali mbali za serikali pamoja na njanja tofauti za kisiasa kiuchumi na kijamii .

Alisema bandari ndogo ndogo zina mtindo wa kupitisha  biashara ya haramu ikiwemo madawa ya kulevya na kutumia mbinu mbali mbali za kuichafua nchi hivyo alizitaka taasisi husika kuchukua juhudi za kukabiliana nazo.

Alieleza kuwa Zaidi ya Shilling Million 378 zilizotumika katika Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Shirika la Bandari la Mkokotoni na kuhakikisha  kuwa si muda mrefu utaanza ujenzi wa gati ambalo linatarajiwa liwe la kisasa lenye hadhi inayolingana na mkoa huo.

Nae katibu Mkuu wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe amesema ujenzi huu ni utekelezaji wa ilani  ya chama ambayo aliahidi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ni moja ya ahadi zake za  kuhakikisha anaimarisha maendeleo  ya miundo mbinu ya Mkoa Kaskazini kwa  kutekeleza ahadi mbali mbali ikiwemo  ujenzi  wa Ofisi ya Bandari pamoja na Gati mpya  ya mkokotoni ambayo inatarajia kuchukua mizigo ya uzito wa tani mia moja.

Aidha alisema  ujenzi wa  bandari hiyo inakusudiwa kutumia Zaidi ya Tsh,Bilioni moja na  Million 800 na gati hiyo inatarajiwa kuwa na  urefu  wa  mita  170 na upana wa mita sita  bandari hiyo inasafirisha abiria kwa kwenda na kurudi pamoja na mizigo mkaa mbao pamoja na dhamani .

Shirika la Bandari lilianzishwa mwaka 1997 ikiwa ni muunganiko wa Idara mbili ikiwemo  Idara ya Bandari pamoja na Zanzibar  Wharf age (Ofeji) kwa lengo la kuleta ufanisi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

1 comment:

  1. Tujitahidi jamaniii eeenh, Idara ya Zanzibar Ofeji ndio ipi tena jamaniii? Tuwe makini waandishi, vyenginevyo tutazalisha waandishi na Taifa bovu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.