Habari za Punde

Bonanza la kuchunguza afya za wananchi na kuchangia damu kwa hiari lafanyika Mkoa wa Kaskazini Unguja

  Afisa uhamasishaji Benki ya Damu Zanzibar Bakari Magarawa akiwapatia elimu Wananchi  wa Mkoa wa Kaskazini Unguja umuhimu wa kuchangia damu katika bonanza lililofanyika Skuli ya Mahonda.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM ambae ni mwanachama wa Taasisi ya G1 Laila Burhan Ngozi akifanyiwa uchunguzi wa damu kwenye bonanza la kuchunguza afya na kuchangia damu kwa hiari, lililoandaliwa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Unguja katika skuli ya Mahonda
 Mwakilishi wa Jimbo la Jangombe Abdalla Maulid Diwan akijumuika kupima afya  katika bonanza lililoandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya kiraia G1 na Chama cha Mapnduzi Mkoa Kaskazini Unguja ikiwa ni maadhimisho ya  miaka 41 ya Chama hicho katika skuli ya Mahonda.
 Mwanachi wa Mahonda Bi Mwajuma Ali Abdalla akiwa mwenye furaha baada ya kupatiwa majibu kutoka  kwa mchunguzi  wa afya Juma Hemedi kutoka Kitengo cha Zanzibar  Youth Empowerment  Associaction.
  Muandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC Kheri Salum akishiriki katika zoezi la kuchangia damu kwa hiari katika Tamasha lilioandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya G1 na CCM Mkoa Kaskazini Unguja.
Makamo Mwenyekiti wa Taasisi ya G1 Ramadhani Kimara akijumuika wananchi wa Mkoa Kaskazini Unguja kuchangia Damu kwa hiari katika bonanza hilo.
Picha na Abdalla Omar Maelezo Zanzibar

Na Ramadhani Ali – Maelezo                        
Katika kuadhimisha miaka 41 ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi, Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya G1 kwa kushirikiana na Chama Mkoa wa Kaskazini Unguja wameandaa bonanza la kuchunguza afya za wananchi na kuchangia damu kwa hiari lililofanyika Skuli ya Mahonda.
Bonanza hilo la nne kuandaliwa na Taasisi ya G1 lilikuwa na lengo la  kupunguza mahitaji ya damu katika Hospitali na vituo vya afya Zanzibar na kuokoa maisha ya wananchi.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Afisa uhamasishaji wa Benki ya damu Nd. Bakari Magarawa alisema matumizi ya damu yameongezeka sana Zanzibar kutoakana na kiwango kikubwa cha mama wanaojifungua, ajali za mara kwa mara na harakati za maisha ya wananchi.
Aliipongeza Taasisi ya G1 kwa kuelewa umuhimu wa damu kwa matumizi ya wananchi na juhudi wanazofanya za kuwahamasisha ili kuchangia kwa hiari na kuongeza ididi ya wananchama kwenye Benki yao.
Amezishauri Taasisi nyengine za kiraia kufanya juhudi kuwahamasisha wanachama wao na wananchi wengine kujitokeza kuchangia damu kwa hiari ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa damu katika hospitali.
Aidha amewataka wananchi waliojitokeza kuchangia damu katika Bonanza hilo kuendelea kuchangia kila baada ya miezi mitatu ili wawe wanachama wa kudumu.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya G1 Nd. Ramadhan Kamara aliahidi kuwa wataendelea kutowa elimu kwa jamii ili kuhakikisha Zanzibar inaondokana na tatizo la upatikanaji wa damu na kila mwananchi atakaehitaji aweze kuipata bila usumbufu.
“Tunataka tufike pahala tuhakikishe suala la kuchangia damu kwa hiari linakuwa ni jambo la kawaida kwa wananchi wote kila kipindi cha miezi mitatu waweze kutoa bila kuhimizwa,” alisisitiza Kamara.
Kiongozi wa G1 ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Jangombe Abdalla Maulid Diwani alisema juhudi zinazofanywa na Taasisi yao ni kutaka kuona wanapunguza vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa damu hasa akinamama wanapojifungua, wakati wa upasuaji na wananchi wanaopata ajali.
Amesema malengo yao ni kuendelea kuandaa mabonanza ya aina hiyo kila inapobidi ili kukusanya damu zaidi kwa ajili ya wananchi na amewaomba wafadhili waendelee kuwasaidia baadhi ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya kuwapa wananchi baada ya kuchangia damu.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.