Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar Mhe. Omar Said Shaban akitowa Salamu za Chama cha Mawakili Zanzibar wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, ilioadhimishwa katika Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Zanzibar.
Mhe. Dr Ali Mohammed Shein – Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mh. Omar Othman Makungu – Jaji Mkuu wa Zanzibar
Mh Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dr Abdulhamid Yahya Mzee, Katibu wa Baraza la Mapinduzi
na Katibu Mkuu Kiongozi
Mh. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar mliokuwepo
pamoja na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Mh. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Naibu
Mkurugenzi wa Mashtaka
Mh. Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi
Waheshimiwa Mahakimu na Makadhi wa ngazi zote za
Mahakama za Zanzibar
Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea na Wanasheria
wote mliopo
Naomba nitambue pia uwepo wa Ma Naibu Katibu Wakuu wa Wizara
ya Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kaimu Mrajis wa Mahakama Kuu
ya Tanzania pamoja Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Lakini pia nachukua fursa hii kuwapongeza wasanii wetu
wa Utenzi na Igizo kwa kazi Yao yenye ujumbe maridhawa ambao bila ya Shaka
unatupa nafasi ya kutafakari zaidi juu ya changamoto zilizopo kwenye jamii na
namna ya kukabiliana nazo. `
Mheshimiwa Mgeni
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia
kukutana tena Leo ikiwa ni muendelezo wa utaratibu uliowekwa na Mahakama wenye
kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama. Mkusanyiko kama huu unatupa fursa
ya wadau wote katika Uga wa Sheria kukumbushana wajibu wetu katika maeneo mbali
mbali kwa lengo moja tu: Kujenga Zanzibar yetu katika maendeleo iwe ya
kiuchumi, kisheria na hata kisera.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Kauli mbiu ya Mwaka huu ni “ Imarisha Utawala wa Sheria
kwa Kukuza Uchumi wa Nchi”. Niwapongeze
wote waliokuja na wazo la kauli mbiu hii maana imekuja katika wakati muafaka
kwa mahitaji ya Wakati tulionao. Imekuja katika wakati ambao serikali yako
inafanya kila aina ya jitihada katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuwakomboa
wananchi kutoka kwenye dimbwi la umasikini. Imekuja katika wakati ambao Nchi
yetu ipo kwenye utekelezaji wa mipango na mikakati mbali mbali ya utafutaji wa
Rasilimali mafuta na Gesi ambazo kama itagundulika kuwepo katika Nchi yetu basi
kutakuwa na transformation kubwa ya aina ya uchumi tulionao na kuiweka nchi
yetu na watu wake katika kundi la Kati la kipato (Middle income state).
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Mipango na mikakati yote hii haitaweza kuwa endelevu na
yenye maslahi kwa Nchi yetu ikiwa hatutakuwa na Sheria Nzuri lakini pia hata
Sheria Nzuri zikiwepo, hatutakuwa na watu au taasisi zinazoheshimu Sheria
ziliopo. Hivyo Kauli mbiu yetu hii ya Leo inaweza kutafsiriwa na kujadiliwa katika
muktadha wa aina mbili. Kuwepo kwa Sheria zenye kuchochea uchumi wa Nchi na
Kuheshimu Utawala wa Sheria ili tukuze uchumi wa Nchi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Wote tukubaliana kuwa kama Nchi tuna changamoto katika
maeneo yote mawili. La Sheria ambazo utumikaji wake zinazorotesha ukuaji wa uchumi
wa Nchi na watu ama Taasisi ambazo ni wagumu kufuata Sheria na hatimae
kuzorotesha Uchumi wa Nchi. Lakini pia Kinyume chake ni Sahihi, yaani tunazo
Sheria ambazo ni bora na nguzo muhimu katika ukuzaji wa Uchumi na wapo watu na
taasisi ambazo siku zote wanajitolea katika kufata Sheria ili kulinda Uchumi na
Maslahi ya Nchi. Hawa wanahitaji kupongezwa na kutiwa moyo.
Mheshimiwa Rais
Ni dhana inayokubalika duniani kote na hata Serikali
yako kuwa pale fursa za kiuchumi na utulivu wa kisiasa unapokuwepo, na mfumo wa
sharia unaoheshimu utawala wa Sheria basi huvuta wawekezaji wa Kigeni na
Biashara za kimataifa. Utawala wa Sheria ni muhimu katika uchumi wa soko kwa
sababu kigezo cha msingi ambacho wanaohusika katika uwekezaji wanaweza kufanya
makubaliano ya kibiashara na kujenga imani kuwa pale panapokuwa na migongano
basi wanaweza kutatua kwa njia ya ufanisi, uwazi na usawa. Pale tunapokuwa na
Sheria ambazo zenye kueleweka na kutabirika, zenye kuainisha Haki na wajibu wa
kila mtu katika shughuli za uwekezaji na uchumi, basi ni rahisi kuvutia
wawekezaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi nchi kwetu na kinyume chake ndio
hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Ni miaka nane sasa tangu report ya Bank ya Dunia kuhusu
urahisi wa kufanya Biashara Zanzibar imetoka. Katika report hiyo, mamlaka 183
za kiuchumi (world economies) zililinganishwa na Zanzibar ambapo vigezo 9
viliangazwa na Zanzibar kushika nafasi ya jumla 155 kati ya chumi 183. Katika
vigezo vilivyoangazwa, vipo ambavyo moja kwa moja vinahusu sheria na sera na
vipo ambavyo vinahusu utendaji tu wa kila siku. Ni jambo la faghari kwetu kuwa
Zanzibar tulifanya vizuri sana kwatika baadhi ya vigezo kama vile utiliaji
nguvu wa utekelezaji wa mikataba ambapo tulishika nafasi ya 37 kati ya 183 huku
tukiwa wa pili kati ya 35 kwa uchumi mdogo wa visiwa tukiwa nyuma ya Singapore.
Vipo vigezo vengine kama vile Vibali vya Ujenzi,
ulipaji kodi, uanzishaji wa biashara, ulindaji wa wawekezaji, upatikanaji wa
mikopo na ufungaji wa biashara. Vyote
hivyo, performance yetu imekuwa ikitofautiana kwa sababu mbali mbali.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Napenda kuchukua fursa kuipongeza Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa hatua madhubuti walizochukua katika kuboresha yale maeneo
ambayo report imeonesha hatukufanya vizuri lakini pia kutobweteka katika maeneo
ambayo report imeonesha Zanzibar inafanya vizuri. Hatua zenyewe ni kama vile
kuanzisha Sheria mpya ya Makampuni na usajili wa Biashara, Kuanzisha kitengo
cha Mahakama ya Biashara cha Mahakama Kuu, kuanzisha mamlaka ya usimamizi wa
mamlaka za leseni na kadhalika. Jitihada zote hizi zipo zilizotoa matunda ya
wazi wazi na zipo ambazo bado zinakubwa na changamoto katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Mathalan katika kigezo cha kuanzisha Biashara
(registering business) ambacho report ilionesha kuwa Zanzibar inashika nafasi
ya 162 kati ya 183 kwa kuanisha ugumu wakati wa kuanzisha biashara na baada ya
uanzishaji wake, binafsi kama mtaalamu wa sharia za makampuni na Biashara
(Corporate Lawyer), napenda kukuthibitisha kwa dhati Mheshimiwa Rais kuwa
tumepiga hatua kubwa sana tangu kutungwa kwa sharia mpya ya Makampuni na ambayo
nafahamu Kanuni zake zipo tayari. Ushuhuda wangu unakwenda katika zama ambazo
kusajili kampuni kulikuwa kunachukua hadi wiki mbili na wakati mwengine
inachelewa kwa sababu printer ya kutolea cheti cha usajili haina wino, lakini
leo binafsi nimeshuhudia kampuni ikisajiliwa ndani ya masaa mawili kutoka muda
ambao nyaraka zimewasilishwa. Ninaamini ikiwa leo Bank ya Dunia watatufanyia
tena tathmini, basi Zanzibar itashika nambari moja.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza kwa dhati kabisa
Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) hasa kitengo cha usajili wa
makampuni kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji wanayoyafanya. Ni matumaini
yangu vitengo vyengine hasa kile cha usajili wa asasi za kiraia kitabadilika
katika utendaji wake wa kazi. Utendaji kazi wa namna ya Wakala wa Usajili wa
Biashara na Mali Zanzibar ukiigwa na taasisi nyengine basi ni wazi kuwa ukuaji
wa Uchumi wa Zanzibar utakuwa katika nafasi nzuri Zaidi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Pamoja na Report ya Bank ya Dunia kutuweka katika
nafasi za juu katika eneo la enforcement of legal contracts na serikali
kuchukua hatua ya kuanzisha Mahakama ya Biashara, bado tuna changamoto ya
utendaji katika Mahakama yetu hii. Mahakama ya namna hii duniani kote inahitaji
vifaa vya kisasa katika uendeshaji wa mashauri yake ili kuitofautisha na
Mahakama nyengine. Naomba nichukue fursa hii kuiomba serikali yako kuitupia
jicho Mahakama hii na kuijengea uwezo na nyenzo ili ijitofautisha na kuvutia wawekezaji
wengi Zaidi kuona ndio mahakama sahihi kwa utatuzi wa migogoro yao wakiwa na
uhakika kuwa mashauri yataenda kwa kasi na uwazi ili mipango yao ya uwekezaji
isikwame kwa kigezo cha kuwa na kesi mahakamani.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Kama nilivyosema awali, kuwa kauli mbiu yetu inaweza
kutafsiriwa katika muktadha wa aina mbili, ule wa kuwa na sheria zenye
kuchochea kukuza uchumi na muktadha wa pili ni ule wa kuwa na watu au taasisi
ziwe za serikali au binafsi zenye utamaduni wa kufata sheria ili kukuza uchumi.
Zipo baadhi ya Taasisi au wakuu wa Taasisi ambao kwao
wao kufuata Sheria zilizowekwa wamekuwa wagumu na matokeo yake wanazorotesha
ukuaji wa uchumi. Kwa mfano, baadhi ya watendaji wa mamlaka ya serikali za
mitaa na wakati mwengine hata serikali kuu wamekuwa na tabia ya kuwabughudhi
wawekezaji kwa sababu ambazo nyengine hazipo kisheria au wangekuwa na njia bora
ya kuzitatua kwa kutumia mamlaka waliyonayo kwa mujibu wa sheria lakini wao
wamekuwa ama sehemu ya migogoro ama kichocheo cha migogoro na hatimae kupelekea
kuibuka migogoro ya kisheria inayokwenda Mahakamani huku aidha ikisitisha
shughuli za kiuchumi au kuzizorotesha.
Wapo wengine hawaoni tabu hata kuagiza kufutwa kwa
vibali vya uwekezaji na kupendekeza Mwekezaji aondoshwe nchini bila ya kufata
utaratibu uliowekwa na sheria au kufanya mashauriano na mamlaka nyengine
zinahusika za kiuchumi kama vile za kodi au uwekezaji. Mara nyingi utasikia
Muekezaji huyu hana maelewano na wananchi lakini ukichunguza pengine
sintafahamu ipo baina ya kikundi kidogo kwenye jamii husika ambacho
kinaushawishi katika mamlaka Fulani.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Hali hii isipodhibitiwa, itajenga hofu kwa watu
wanaotaka kuekeza kwenye Nchi yetu maana hawatojua siku wala saa watakayoambiwa
waondoke nchini kwa kigezo cha “kutotakiwa na wananchi wanaozunguka miradi”
Zanzibar Law Society hatukusudii kusema kuwa wawekezaji waachiliwe hata pale
wanapokuwa kero kwa wananchi wenzetu, HAPANA! Tunachokisisitiza ni umuhimu wa
kufuata utaratibu wa Sheria katika kukabiliana na kero za namna hiyo. Nchi yetu
inaongozwa na Katiba lakini pia kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tumeridhia mikataba mbali mbali ya Kimataifa yenye kulinda Wawekezaji na
Uwekezaji. Si vyema jithada za Serikali katika kuwaalika wawekezaji kuja nchini
zikatiwa doa na watu wachache ambao hawajui athari za matendo yao.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Mifano ya changamoto za namna hii ipo mingi na sio
rahisi kuieleza yote kwenye jukwaa hili, jambo la muhimu kwa wadau wote wa
Sheria waliopo hapa na wanaofatilia kwenye vyombo vya habari kutafakari kwa
kina maana ya Kauli mbiu yetu ya leo na kuitafsiri kwa muktadha wa maeneo yao
ya kazi na shughuli zao za kiuchumi iwe serikalini ama sekta binafsi kwa lengo
moja tu, nalo ni kuangalia maslahi mapana ya Nchi yetu.
Nimalizie kwa kunukuu maneno ya aliyekuwa waziri wa
Mambo ya Nje wa Marekani Bi Hillary Clinton ya mwezi August 2009 wakati
anazindua Makubaliano ya Uwekezaji baina ya nchi yake na Nchi ya Mauritius
alipoimwagia sifa nchi hiyo kwa kusema
“Mauritius has
taken steps in recent years to attract investment by enacting reforms that
protect investors and promote business. They have made it easier to launch
start-ups, to access credit and to register property. They have demonstrated a
commitment to transparency. Accountability and good governance. Mauritius has
attracted more investment in the last three years than it did in the preceding
twenty years”
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Zanzibar haina tofauti sana na
Mauritius, sifa wanazomwagiwa na Jumuiya ya kimataifa tunaweza kuzipata na
sisi. Inawezekana ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake.
Ahsante
kwa kunisikiliza
Omar
Said Shaaban
Rais
– Zanzibar Law Society
No comments:
Post a Comment