Habari za Punde

Kampuni ya kimataifa ya uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia kutoka China yakutana na Waziri Salama Aboud

 Waziri wa Ardhi Maji Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib kulia akizungumza na Ujumbe kutoka kampuni ya CNOOC ya China kuhusiana na masuala mbalimbali ya Mafuta pamoja na Mafunzo mkutano uliofanyika Ofisini kwake Forodhani mjini Unguja.

Waziri wa Ardhi Maji Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib wapili kulia akiwa katika Picha ya pamoja  Ujumbe kutoka kampuni ya CNOOC ya China uliofika Ofisini kwake Forodhani mjini Unguja. kuzungumzia  masuala mbalimbali ya Mafuta pamoja na Mafunzo  Zanzibar.

PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

Na Maryam Kidiko – Maelezo.                
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea ujumbe kutoka Kampuni ya Kimataifa ya China ijulikanayo kama China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) inayojishughulisha na uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia.
Viongozi wa Kampuni hiyo wamefika katika Wizara ya Ardhi,Maji,Nishati na Mazingira Forodhani mjini Zanzibar kwa ajili ya kuzungumza mambo mbali mbali na Viongozi wa Wizara hiyo.
Akizungumza kuhusu ziara ya CNOOC hapa nchini Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Maji,Nishati na Mazingira Ali Khalili Mirza alisema ujumbe huo ni utekelezaji wa makubaliano ambayo Kampuni hiyo ilitiliana saini na Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar.
Katibu Mirza alisema kampuni hiyo kubwa inayoshuhulikia mambo ya utafiti na uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia, imekuja kwa lengo la kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika suala hilo.
Alifahamisha kuwa katika hati ya makubaliano waliyoawekeana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kampuni hiyo itafanya kazi zake Zanzibar sambamba na kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wataalamu wa Zanzibar wataoshughulika na sekta ya Gesi na Mafuta.
Aidha Wataalamu hao kutoka Zanzibar pia watapata nafasi ya kwenda nchini China kupata mafunzo zaidi kuhusiana na Mafuta na gesi asilia.
 “ kampuni ya (CNOOC) imeweza kuonana na Waziri na wamekuja hapa kuweza kusalimiana nae kama nyumbani na baadae wataweza kuonana na viongozi mbali mbali wanaohusika na sekta ya Mafuta na Gesi ”alisema Katibu Mkuu.
Kuhusu hatua ya uchimbaji wa Mafuta iliyofikiwa hapa Zanzibar Katibu Mirza alisema bado suala hilo lipo katika hatua ya utafiti na kwamba Wataalamu watakapomaliza taarifa ya matokeo ya utafiti itatolewa kwa Wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.