Habari za Punde

SMZ Yatangaza Miongozo Kuelekea Ugatuzi

Na Maryam Kidiko, Maelezo Zanzibar, 13 Febuari, 2018
KATIKA hatua ya ugatuzi iliyoanza kutumika rasmi hapa Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ,Mhe. Haji Omar Kheri, amesema serikali imeandaa miongozo miwili kwa ajili ya mabaraza ya Wadi na Kamati za mashauriano za shehia.
Akizungumza leo na waandishi wa habari katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Unguja kuhusu na kuanzishwa kwa mabaraza ya kamati hizo, Waziri Kheri amesema miongozo hiyo itarahisisha utendaji kazi, kuimarisha utoaji huduma bora kwa wananchi pamoja na kukuza kiwango cha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi.
Alieleza kuwa, miongozo hiyo iliyozinduliwa rasmi leo, utekelezaji wake utaanza kwa kuwapa taaluma masheha na Madiwani wote Unguja na Pemba itakayowawezesha kuzungumza na wananchi wa maeneo yao ili kuwahamasisha katika kushiriki na kuomba nafasi za kuteuliwa kwenye mabaraza hayo.
Aidha alifafanua kuwa ushiriki katika mabaraza hayo ni haki ya kila mwananchi kwa kuzingatia masharti ya miongozo iliyotolewa.
“Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ haitarajii wananchi kubabaishwa katika kupata haki hii kwa sababu yoyote isiyokobalika,” aliongeza Waziri Kheri.
Alifahamisha kuwa miongozo hiyo imetayarishwa kwa lugha nyepesi ambayo itakayoweza kueleweka na kila mtu kwa urahisi.
Waziri huyo alisema ni imani yake kwamba kila muhusika ambaye ametajwa katika muongozo huo atatekeleza wajibu wake kwa uaminifu na uadilifu ili lengo la kupeleka madaraka kwa wananchi lifanikiwe.
Alisema mpango huo wa kupeleka madaraka kwa wananchi unalenga kukuza uchumi na kupunguza umaskini, hivyo jambo muhimu ni ushirikiano ili lengo hilo liweze kufikiwa.
“Nawaomba wananchi na wahusika wengine katika maeneo ya mamlaka ya serikali za mitaa washiriki kikamilifu katika kuharakisha maendeleo ya jamii ili kuweza kupunguza umaskini,” aliongeza Waziri huyo.
Sambamba na hayo alisema kuwa Ofisi yake inaendelea na taratibu za kuandaa ofisi za masheha ili kuepuka changamoto zinazojitokeza katika utaratibu wa sasa kufanyia kazi katika nyumba zao.

            IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO  ZANZIBAR.                           

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.