Habari za Punde

Makamu wa Rais akagua ujenzi wa Skuli ya Sekondari Micheweni

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki ujenzi wa skuli ya Sekondari Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba kushirikiana katika shughuli za maendeleo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Afya cha Huduma ya Mama na Mtoto Shumba Vyamboni wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kituo hicho cha Mama na Mtoto cha Shumba Vyamboni kitatoa huduma za Mama na Mtoto ambapo jumla ya Wananchi 5,593 wakiwemo wanawake wenye uwezo wa kuzaa 1543 na watoto chini ya umri wa miaka mitano 984 watapata huduma bora ya uzazi, lishe na ustawi wa mama na mtoto.

Vijiji vitakavyofaidika na huduma ya kituo hicho ni pamoja na Kibubunzi, Kikunguni, Mihogoni, Nyuma ya Mti, Mgeninje, Utaani, Shumba vya Mboni, Uwondwe, Mamoja, Gombe, Uwaani na Bule.
Katika ziara hiyo yenye lengo la kuhimiza shughuli za maendeleo 

Makamu wa Rais alikagua ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Micheweni pamoja na kumtembelea Muasisi wa Chama Cha Mapinduzi Bi. Mrashi ambapo alimkabidhi mabati ya kuezekea nyumba yake inayojengwa na wanachama wa chama cha Mapinduzi katika eneo la Sizini.

Mwisho Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Tawi la CCM la Ukunjwi ambapo aliwaambia wakina Mama kuwa mstari wa mbele katika kuonesha njia ya kuwa kiongozi bora.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.