Habari za Punde

Waziri Mwakyembe amtaka Msanii Roma Mkatolilki kujisajili BASATA ili aweze kuendelea na shughuli za Sanaa


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya kufanya kikao na wasanii wa mziki Roma Mkatoliki na Pretty Kind jana jijini Dar es Salaam. Pembeni kwa waziri ni Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza


Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kulia) akifafanua jambo wakati wa kikao na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na wasanii Roma Mkatoliki na Pretty Kind jana Jijini Dar es Salaam. Katikati ni mwakilishi kutoka Bodi ya Filamu Bw. Benson Mkenda na kushoto ni msanii wa mziki Pretty Kind


 Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kushoto) akiwaonyesha waandishi wa habari nakala ya cheti cha usajili cha msanii Pretty Kind kutoka BASATA wakati wa kikao na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe


 Msanii wa mziki wa bongo fleva Roma Mkatoliki (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya kikao na Waziri pamoja na Naibu Waziri ambapo alitangaza kuufuta na kuviomba vyombo vya habari kutoucheza tena wimbo wake wa kibamia. Kushoto ni Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza


Msanii wa mziki wa bongo fleva Pretty Kind (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam baada ya kufunguliwa kifungo alichokua amefungiwa cha kutojihusisha na mziki kwa miezi sita na kuahidi kuwa balozi mwema wa maadili kwa wasanii wenzake. Kulia ni Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza


Mwakilishi kutoka Bodi ya Filamu Bw. Benson Mkenda (kulia) akifafanua jambo wakati wakati wa kikao na waandishi wa habari baada ya kuzungumza na wasanii Roma Mkatoliki na Pretty Kind jana Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe katika picha ya pamoja na Msanii Roma Mkatoliki (wapili kushoto) na msanii Pretty Kind (kulia) baada ya kuzungumza nao na kurekebisha tofauti zilizopelekea kufungiwa kwa wasanii hao jana Jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza

Picha na: Genofeva Matemu - WHUSM



Na: Genofeva Matemu – WHUSM. 30/03/2018
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amemtaka Msanii wa muziki wa bongo fleva Roma Mkatoliki kujisajili BASATA ili aweze kuondolewa kwenye kifungo chake cha kutokufanya shughuli za sanaa kwa miezi sita alichofungiwa mwanzoni mwa mwezi machi mwaka huu.

Hayo ameyasema wakati wa kikao na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam baada ya kikao na wasanii wa mziki Roma Mkatoliki na Pretty Kind ambapo Wizara ilimtaka msanii Roma kubadilisha wimbo wake wa kibamia na kujisajili BASATA ili aweze kuondolewa katika kifungo hicho ambapo msanii huyo alitangaza kuufuta wimbo huo na kuahidi kujisajili BASATA ili aweze kuendelea na mziki.

“Kwa kuwa msanii Roma Mkatoliki ameamua kuufuta kabisa wimbo wa kibamia na kuvitaka vyombo vya habari kutokuucheza tena wimbo huo Wizara inamfungulia kifungo chake mara tu baada ya kujisajili BASATA atakuwa huru kuendelea na kazi zake za sanaa” amesema Mhe. Mwakyembe

Aidha Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Msanii Suzan Michael (Pretty Kind) ametambua kosa alilolifanya na kukiri kosa hilo kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandika barua ya kuomba msamaa na kujisajili BASATA kuwa msanii halali hivyo Wizara kwa kushirikiana na BASATA imeridhia kumfungulia adhabu aliyopewa ya miezi sita ambayo kimsingi ilitakiwa kuisha tarehe moja julai mwaka huu.

“Kuanzia sasa msanii Pretty Kind yupo huru kuendelea na kazi zake za sanaa kutokana na yeye kutimiza matakwa aliyoagizwa kuyafanya na kuahidi kuwa balozi mwema wa masuala ya maadili kwa wasanii wenzake” amesema Mhe. Shonza

Hali kadhalika Mhe. Shonza amewaomba wasanii wengine nchini kuiga mfano wa msanii Pretty Kind wa kujisajili BASATA ili waweze kutambulika rasmi katika tasnia ya sanaa na kuweza kuendana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika tasnia hiyo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Naye msanii wa muziki nchini Roma Mkatoriki ameviomba vyombo vya habari nchini kuufuta, kuuondoa sokoni na kuacha kuucheza wimbo wake ujulikanao kwa jina la kibamia kwani wimbo huo umekua ukileta ukakasi katika jamii kutokana na maneno pamoja na picha jongevu zilizotumika katika wimbo huo.

Sanjari Msanii chipukizi wa bongo fleva Bi. Suzan Michael (Pretty Kind) ameishukuru Wizara ya Habari kwa kuweza kumweka sawa na kwenye mstari ulionyooka kwa kufuata taratibu za kujisajili kwani sanaa ni kazi kama vile zilivyo kazi zingine hivyo kuwaomba wasanii wenzake kubadilika na kusimamia ndoto zao ili waweza kuleta sifa nzuri kwa nchi ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.