MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amefungua mkutano wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na kuwapongeza wajumbe wa mkutano huo kwa
kuchaguliwa na kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.
Mwenyekiti huyo wa CCM
aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa (NEC) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ikulu Jijini
Dar-es-Salaam.
Katika maelezo yake,
Rais Magufuli aliwahakikishia Wajumbe hao kuwa ataendelea kushirikiana nao kwa
maslahi ya CCM katika kuhakikisha chama hicho kinazidi kupata mafanikio na
maendeleo zaidi.
Aidha, Rais Magufuli
alitumia fursa hiyo kueleza mafaniko yaliopatikana katika utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Katika kikao hicho, Rais
Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein waliwahakikishia viongozi hao wa NEC pamoja na wananchi wote
wa Tanzania kuwa wataendelea kuusimia na kuuimarisha Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar kwa nguvu zao zote.
Viongozi hao walitumia
fursa hiyo kuwaeleza Wajumbe hao wa NEC kutumia muda wao kuwaelimisha viongozi
wa CCM pamoja na wananchi wote wa Tanzania juu ya umuhimu, malengo na faida za
Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika Mkutano huo,
Wajumbe wa NEC waliridhia majina ya Wajumbe wapya wawili aliowateuwa na Rais
Magufuli hivi karibuni kutokana na nafasi zake katika wadhifu wake wa
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambao ni Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda na
Charles Makongoro Nyerere.
Rais Magufuli alitumia
fursa hiyo kueleza uzoefu wa Wajumbe hao wapya ndani ya chama hicho na kueleza
jinsi walivyoweza kukitumia hadi hivi leo.
Pia, katika Mkuno huo wa
NEC, Wajumbe walifanya uchaguzi wa kuwachagua wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (CC) kwa upande wa
Tanzania Bara na Zanzibar.
Wajumbe waliokuwemo
katika kinyanganyiro hicho jumla yao walikuwa tisa kwa kila upande wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara aliekuwemo ni
Burton Kihaka Lumuliko, Charles Makongoro Nyerere, Ernest Samson Sungura.
Wengine ni Jackson
William Msome,Komanya Eric Kitwala, Mizengo Kayanza Peter Pinda, Richard
Bundala Charles, Khadija Shabaan Taya (Keisha) na Theresia Adriano Mtewele.
Kwa upande wa Zanzibar waliekuwemo
katika kinyanganyiro hicho ni Afadhali Taibu Afadhali, Bakar Hamad Khamis,
Cassin Galos Nyimbo, Kombo Hassan Juma, Ramadhan Abdalla Shaaban, Ramadhan
Shaibu Juma, Kidawa Hamid Saleh na Lailah Burhan Ngozi.
Waliochaguliwa kwa
upande wa Tanzania Bara kuwa Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (CC) ni Mizengo Kayanza Peter Pinda, Charles
Makongoro Nyerere na Khadija Shaban Taya (Keisha).
Kwa upande wa Zanzibar
waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (CC) ni Kombo Hassan
Juma, Afadhali Taibu Afadhali, Lailah Burhan Ngozi na Waride Bakari Jabu.
Mapema Mwenyekiti wa CCM
Taifa Dk. John Pombe Magufuli alieleza kuwa CCM ni chama cha watu wote wa rika zote, jinsia zote wakiwemo wakulima na wafanyakazi.
Pia, Rais Magufuli alieleza
kuwa Tanzania iko vizuri katika uchumi wake ambapo kwa mwaka 2018 hadi 2030 ni
miongoni mwa nchi nne duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kuelekea
uchumi wa kufikia asilimia 7.1 ambapo kwa hivi sasa tayari umeshafikia asilimia
7.
Nae Makamo Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein aliwahakikishia Wajumbe wao wa NEC kuwa ataendelea kushirikiana
nao, kuwatumikia wao pamoja na kuwatumikia
wanaCCM na wananchi wote wa Tanzania.
Dk. Shein pia, alitumia
fursa hiyo kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuimarisha uchumi wa
Zanzibar na juhudi zinazoendelea katika kuhakikisha uchumi huo unaimarika
zaidi.
Wakati huo huo, Wajumbe
hao wa NEC waliridhia kustaafu wa Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdulrahman Kinana
ambaye amemuomba Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa kustaafu.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa
na Katibu Mkuu huyo wa CCM na kusomwa na
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Magufuli mbele ya Wajumbe hao wa NEC,
Katibu Kinana alieleza sababu zilizompelekea kustaafu kwake ambazo zilikubaliwa
na Mwenyekiti huyo, Makamu wake wote wawili pamoja na Wajumbe hao wa NEC.
Akimpongeza Katibu Mkuu
huyo kwa ujasiri wake mkubwa wa kukipenda Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais
Magufuli alieleza kuwa Katibu Mkuu huyo aliyestaafu amejituma sana na ameonesha
jinsi anavyokipenda chama hicho na katika maisha yake yote amekuwa akihakikisha
CCM inashinda na inaendelea kubaki madarakani.
Mwenyekiti huyo wa CCM
Taifa alieleza kuwa CCM haitamsahao Katibu huyo mstaafu na wala haitomtupa na
itaendelea kushirikiana nae katika kuhakikisha chama hicho kinaimarika zaidi.
Nae Katibu Mkuu huyo
Mstaafu akitoa neon la shukurani, alimpongeza Rais Magufuli, aliwapongeza Makamu
Wenyeviti wote wa CCM wa Bara na Zanzibar, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
pamoja na wanachama wote wa CCM kwa kufanya kazi nao vizuri katika wakati wake
wote wa kazi.
Alieleza jinsi alivyojitolea
na kusafiri masafa marefu Bara na Zanzibar katika kukimarisha chama hicho na
hatimae kuendelea kupata ushindi na kuwataka Wajumbe hao wa NEC kuisoma sana
Katiba ya CCM, Kanuni na miongozo mbali mbali inayotolewa na Chama hicho.
Sambamba na hayo, alisisitiza
kuwa nguvu ya CCM ipo kwenye umoja na kueleza haja ya kuimarisha umoja na
kuwataka viongozi wa CCM kutambua kuwa ndani ya CCM kuna kundi moja tu ambalo
ni CCM huku akitumia fursa hiyo kuwapongeza wanahabari kwa ushiriki wao mzuri
katika kutoa habari juu ya chama hicho hasa pale alipozunguka nchi nzima katika
kukiimarisha.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment