Habari za Punde

Fainali Kombe la FA: Antonio Conte asema ana 'uhusiano wa kawaida' na Jose Mourinho

Meneja wa Chelsea Antonio Conte amesema atamsalimia Jose Mourinho kwa mkono watakapokutana Chelsea wakikabiliana na Manchester United katika fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley Jumamosi.
Mameneja hao wawili wamekuwa na uhasama kila klabu zao zinapokabiliana Ligi ya Premia.
Lakini Ijumaa, Conte alisema: "Kesho, nitamsalimia kwa mkono na sote wawili tutafikiria kuhusu mechi."
"Si muhimu yale yaliyopita awali. Kuna uhusiano wa kawaida kati yangu naye."
Uhasama kati ya wawili hao ulianza Oktoba 2016, msimu wa kwanza wa Conte ligi kuu England pale Mwitaliano huyo alimpomshambulia Mourinho akisherehekea baada ya Chelsea kuwalaza United 4-0.
januari, Conte alimweleza Mreno huyo kama "mwanamume mdogo" baada ya kurushiana maneno kupitia vyombo vya habari.
Conte anaondoka?
Conte anatarajiwa na wengi kuondoka Chelsea majira ya joto na alipoulizwa kuhusu mustakabali wake, aliwachezea wanahabari na kusema: "Ninaweza kusema kwa kweli kwamba mechi hii itakuwa yangu ya mwisho, msimu huu.
"Kwangu na wachezaji, itakuwa mechi yetu ya mwisho. Kisha, kama mjuavyo vyema sana, nina mkataba na nimejitolea kwa klabu hii."
Mourinho alikataa kuzungumzia mustakabali wa Conte akisema: "Hadi iwe rasmi kwamba Antonio ameondoka, sijui. Kwa kweli, mkiniuliza kama nafuatilia hili - ni hamu tu ya kutaka kujua.
"Kuhusu mechi ya kesho (Jumamosi), iwapo itakuwa mechi yake ya mwisho au la, sifikiri hilo litabadilisha mtazamo wake kwa mechi hii na hamu yake ya kutaka kushinda."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.