Habari za Punde

Maoni ya kamati ya Fedha, Biashara ba Kilimo kuhusu makadirio na mapato na matumizi ay Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi 2018/2019



HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA FEDHA, BIASHARA NA KILIMO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019

Mheshimiwa Spika,

Kwa heshima kubwa natanguliza shukurani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambae ametujaalia kufika hapa kwa mara nyengine tukiwa wazima na wenye afya njema. Namuomba tena Mwenyezi Mungu akuzidishie wewe Mheshimiwa Spika busara, hekma na uadilifu katika kutuongoza na sisi pia atujaalie tuendelee kuwa  na nguvu na ari ya kuitekeleza vyema Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020 pamoja na malengo tuliyojipangia ili tuweze kutoa huduma bora kwa  Wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika,

Kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ujasiri wake wa kutekeleza vyema jukumu zima la uongozi wa nchi hii sambamba na jitihada anazochukua za kuendeleza sekta ya kilimo na sekta nyengine hapa nchini. Aidha, tunatoa shukurani za dhati kwa Makamo wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa busara zake na ushauri anaompatia Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa mambo mbali mbali kwa ustawi wa nchi na wananchi wetu. Kadhalika, tunamshukuru Mheshimiwa Balozi kwa kusimamia vyema shughuli za Baraza hili akiwa ni kiongozi wa shughuli za Serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Spika,

Nitakuwa mkosefu wa shukurani iwapo nitashindwa kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi hususan kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa kukusanya zaidi ya asilimia 165 ukilinganisha na mwaka uliopita. Hili limechangiwa zaidi na usimamizi mzuri wa kuhakikisha uvujaji wa mapato unadhibitiwa hususan mapato ya uchimbaji mchanga. Kamati inaisisitiza Wizara isije ikalewa sifa wanazopewa na badala yake kuongeza juhudi na maarifa ya kuibua mbinu mbadala zitakazohakikisha zinawafikisha katika malengo yaliyopangwa kwa mwaka huu wa fedha wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika,

Kwa huzuni kubwa napenda kuwapa pole Wananchi wetu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na maafa ya mvua za msimu huu wa Masika zilizoathiri mali, Makaazi ya Wananchi wetu pamoja na kusababisha baadhi ya Watu kupoteza maisha. Kwa niaba ya Kamati yetu ya Fedha, Biashara na Kilimo nasi hatuna budi kuwaomba Wananchi hao wawe na moyo wa subira na uvumilivu hasa katika kipindi hiki kigumu. Aidha, naiomba Serikali na Taasisi binafsi kuendelea kuchukua juhudi za kuwajali na kuwathamini Wananchi hao kwa kuwapatia misaada ya hali na mali.

Mheshimiwa Spika,

Kwa heshima na taadhima, kwa kutambuwa mchango na ushauri mkubwa katika kutekeleza kazi za Kamati hii, naomba sasa niwatambue kwa kuwataja majina yao Waheshimiwa Wajumbe wafuatao wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo:-

1.
Mheshimiwa Yussuf Hassan Iddi
-
Mwenyekiti;
2.
Mheshimiwa Hamida Abdalla Issa
-
Makamo Mwenyekiti;
3.
Mheshimiwa Hamad Abdalla Rashid
-
Mjumbe;
4.
Mheshimiwa Moh’d Mgaza Jecha
-
Mjumbe;
5.
Mheshimiwa Ali Salum Haji
-
Mjumbe;
6.
Mheshimiwa Ussi Yahya Haji
-
Mjumbe; na
7.
Mheshimiwa Bihindi Hamad Khamis
-
Mjumbe.

Aidha, Kamati yetu pia inafanyakazi kwa kusaidiana na makatibu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitusaidia kutekeleza majukumu yetu, kwa heshima naomba niwatambue makatibu hao ni:


1.
Ndugu Asma Ali Kassim
-
Katibu
2.
Ndugu Said Khamis Ramadhan
-
Katibu
Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu ilipitia, kujadili na hatimae kupitisha Makadirio ya Fungu L01 la Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi tarehe 04/05/2018 baada ya kuelekeza kufanyiwa marekebisho kutokana na kuwepo utofauti katika jumla ya Makadirio ya Matumizi ya shilingi 2.54 bilioni ambapo jumla ya shilingi 65.16 bilioni yaliainishwa katika Makadirio ya Matumizi ya Kitabu cha Mswaada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 ambacho Kamati ilikabidhiwa na Ofisi katika ngazi ya Kamati na jumla ya shilingi 62.62 bilioni iliyoainishwa ndani ya kitabu cha Hotuba ya Waziri, Tofauti hiyo imesababishwa zaidi na fedha hizo kuhamishiwa Serikali za Mitaa kwa ajili ya ulipaji wa maslahi ya wafanyakazi waliogatuliwa kutoka Wizara hii ya Kilimo. Kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo naomba niwasilishe mbele ya Baraza Lako Tukufu maoni ya Kamati yetu kuhusiana na Programu Kuu na Programu ndogo za Wizara hii kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika,

Kiujumla, bajeti ya makusanyo ya mwaka huu ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imeongezeka maradufu ukilinganisha na bajeti ya mwaka jana. Kwa mwaka 2017/2018, Wizara hii ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 4.93 bilioni ukilinganisha na makadirio ya mapato ya shilingi 12.50 bilioni ya mwaka ujao 2018/2019 sawa na ongezeko la shilingi 7.57 bilioni ya makadirio ya mapato. Hii inaonesha wazi kwamba kiwango cha makadirio ya makusanyo waliyopangiwa Wizara hii ni kikubwa sana kwani ni zaidi ya mara mbili ya kile kiwango walichopangiwa mwaka jana ukiachia mbali kuvuka lengo la mkusanyo kwa kukusanya shilingi 7.7 bilioni. Kamati inaishauri Serikali iangalie vizuri makadirio ya makusanyo waliyoipangia Wizara hii kwani inaonekana wazi sio rahisi kufikia lengo hilo kwa asilimia mia moja hasa ukizingatia hakuna vyanzo vipya vya mapato ilivyoongezeka. 

Mheshimiwa Spika,

Lakushangaza, pamoja na kuongezewa kiwango cha mapato yanayohitajika kukusanywa na Wizara hii lakini wamepunguziwa matumizi. Mwaka huu Wizara hii imepangiwa kutumia jumla ya shilingi 62.62 bilioni ukilinganisha na shilingi  70.61 bilioni za mwaka jana. Hii ni sawa na punguzo la shilingi  bilioni 8. Kwa vile Wizara ya Kilimo ndio uti wa mgongo unaotegemewa na wananchi wetu katika sekta husika za kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, punguzo hilo litakuwa na athari kwa kipato cha wananchi wetu na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,

Sambamba na hilo, Kamati yetu ilipata mashaka kidogo ilipokuwa ikipitia kwa undani makadirio ya mapato ya Mauzaji ya Mazao na Miche kinachokusanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo - Kizimbani (kifungu 1423002). Chanzo hiki kilipangiwa shilingi 20,000,000 milioni kwa mwaka jana ambapo mwaka huu kimepangiwa kukusanya shilingi 70,000,000 milioni sawa na ongezeko la shilingi 50,000,000 milioni, baada ya kukitathmini chanzo hiki cha mapato, Kamati iliona Wizara imepangiwa fedha nyingi kuliko uhalisia wake. Kamati inaishauri Serikali kuyaangalia upya makadirio ya makusanyo ya chanzo hicho cha mapato kwa kupanga kiwango kinacholingana na uhalisia wa upatikanaji wa mapato kupitia chanzo hicho.

PROGRAMU KUU YA MAENDELEO YA KILIMO

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu imegundua kwamba kuna wakulima wengi wameathiriwa na mvua za masika zilizokuwa zikiendelea kwa kuharibu maeneo wanayatumia kwa kilimo pamoja na mazao yao kutokana na kujaa kwa maji. Aidha, kuna miundombinu mingi ya barabara ambayo nayo imeharibika inayowasaidia wakulima wetu kusafirishia mazao yao kutoka maeneo wanayolima. Kamati yetu inaishauri Wizara hii ya Kilimo kukaa na Taasisi zinazoshughulikia Maafa na utengenezaji wa miundombinu ya barabara ili kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwapatia wakulima wetu fedha kidogo kufidia athari waliyoipata ili wakulima wetu waweze kupata faraja kutokana na hasara waliyoipata.

Mheshimiwa Spika,

Suala la uimarishaji wa kilimo cha umwagiliaji maji katika nchi yetu ni jambo la msingi ambapo Wizara ya Kilimo imekuwa ikilifanyia kazi kwa juhudi kubwa hususan katika kuimarisha kilimo shadidi. Kamati inaipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 2.5 kwa mwaka jana hadi tani 6.8 mwaka 2017/2018 kwa hekta kwa kutumia kilimo cha teknolojia ya Shadidi. Kamati inaishauri Wizara hii kuendelea na juhudi hizo za kuwahamasisha wakulima wetu ili waweze kuhamasika na kulima zaidi kilimo hicho cha kibiashara.

Mheshimiwa Spika,

Licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Wizara hii ya Kilimo ya kununua matrekta mapya 20 na kupokea matrekta mengine 10 kutoka nchi ya Libya, bado wakulima wetu wanakabiliwa na changamoto ya kutolimiwa eka zao za mpunga kwa wakati na hatimae huambulia kupata mavuno machache. Kamati imeelezwa na wataalamu wa Kilimo kwamba, ili sekta ya kilimo ipige hatua kwa kuwa na matrekta ya kutosha basi kunahitajita yapatikane matrekta 80 ambapo Serikali yetu tayari imeshaingia Mkataba na Kampuni ya kutengeneza Matrekta (Mahindra) iliyopo nchini India wa kuipatia nchi yetu Matrekta 100. Hivyo, tunaiomba Serikali yetu sikivu kuharakisha upatikanaji wa nyenzo hizo ili wakulima wetu waepukana na kilimo cha jembe kongoroka mpini.

Mheshimiwa Spika,

Wakati Kamati yetu ilipokuwa ikipitia Makadirio ya Matumizi ya Programu hii ya Maendeleo ya Kilimo iligundua kwamba Wakala wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo haikupangiwa pesa, Kwa kuthamini na kutambua umuhimu wa Wakala huo hususan katika kuwasaidia wakulima wetu kulimiwa na kuburugiwa mashamba na eka zao za kilimo cha mpunga, Kamati iliishauri Wizara hiyo kuipangia pesa za kutosha Wakala huo ili uweze kuleta faraja kwa wananchi wetu. Hatimae Wakala huo ulipangiwa jumla ya shilingi 1.38 bilioni ambazo japo kwamba hazitoshi lakini angalau wataweza kuendelea kutekeleza majukumu yao waliyojipangia.

Mheshimiwa Spika,

Katika Programu Kuu ya Maendeleo ya Kilimo kuna Programu Ndogo ya Umwagiliaji Maji ambayo imepangiwa kutumia fedha kidogo shilingi 10.11 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ukilinganisha na shilingi 27.15 bilioni za mwaka 2017/2018. Kamati ilielezwa kwamba fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya maji. Hata hivyo, Kamati yetu ilitaka kujua miundombinu hiyo itajengwa wapi na kwanini kifungu hicho kimepungua kwa takriban shilingi 17.04 bilioni. Punguzo hili ni kubwa pamoja na kwamba fedha nyengine zitafidiwa kupitia mradi wa Maendeleo unaofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo ambapo utegemezi wa fedha hizo hauna uhakika zaidi. Kwa kuelewa umuhimu uliowekwa na Serikali yetu ya kuhimiza kilimo cha kibiashara cha umwagiliaji maji, ni busara kifungu hicho kikaongezewa bajeti ili kiedane na utekelezaji wa azma hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu pia ilihoji kifungu kinachotoa Huduma za Utibabu wa Mimea na Karantini na Ukaguzi wa Mazao (HL01010303) kwamba kimepangiwa fedha nyingi mno shilingi 113.11 milioni kwa mwaka huu 2018/2019 ukilinganisha na shilingi 3.06 milioni za mwaka jana 20017/2018 sawa na tofauti ya shilingi 110.04 milioni. Fedha hizo zinaonekana kuwa nyingi pamoja na kwamba matibabu hayo yanafanyika nchi nzima. 

 Mheshimiwa Spika,

Wakulima wetu ni masikini sana ambao wanahitaji msukumo wa hali ya juu kutoka Serikalini ili kuimarisha kilimo kwa lengo la kujipatia kipato bora kitakachowasaidia wao wenyewe, familia zao na Taifa letu. Katika kuhakikisha hilo linafanyika, Kamati yetu inaendelea kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa utekelezaji mzuri wa shabaha ya ununuzi wa tani 900 za mbolea ya kupandia mpunga na tani 900 kwa ajili ya kukuzia mpunga, tani 170 za mbegu na lita 17,400 za dawa ya kuulia magugu ambazo zimesambazwa Unguja na Pemba. Pamoja na juhudi hizo, bado kuna changamoto kubwa inayowakabili wakulima wetu ya kukosa baadhi ya pembejeo hizo. Kamati yetu ilithibitisha hilo ilipotembelea bonde la Pangeni na kukuta msongomano wa wakulima wakifuatilia ugawaji wa dawa za kuulia magugu. Kamati yetu haikuridhishwa na utaratibu uliokuwa ukitumika kwani dawa hizo zilikuwa zikitolewa kwa wakulima wa Pangeni na kuwaacha wakulima wa Kilombero na Upenja wakilalamika. Aidha, hao wakulima waliopatiwa dawa hizo walipatiwa nusu ya mahitaji yao.

PROGRAMU KUU YA MAENDELEO YA MIFUGO

Mheshimiwa Spika,

Programu Kuu hii inayo Programu Ndogo ya Wakala wa Tafiti za Mifugo inayohusiana kufanya Tafiti za Mifugo (kifungu kidogo SL010303). Mwaka 2017/2018 kifungu hicho kinaonekana hakijapangiwa fedha lakini mwaka 2018/2019 kimepangiwa shilingi 829 milioni. Kamati ilitaka ufafanuzi na kuelezwa kwamba masuala ya tafiti za mifugo zimeundiwa Idara yake na fedha za kutekeleza shughuli hiyo zitapatikana katika Idara husika. Kamati inashauri Idara hiyo ipangiwe fedha za kutosha kwani bila ya kufanyika tafiti za mifugo, Wizara haitoweza kupiga hatua mbele kwa vile mifugo yetu inasumbuliwa na maradhi ya aina tofauti.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu imeshangazwa na kusikitishwa sana na vitendo vya baadhi ya watendaji wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kushindwa kutekeleza baadhi ya maagizo na maelekezo ya Kamati na Viongozi wao, Hili limetokea baada ya Waziri wa Kilimo aliyepita Mheshimiwa Hamad Rashid Mohammed kuridhia na kukubali kuipeleka Kamati Bagamoyo kwenda kuliangalia Shamba la Serikali lililobadilishwa matumizi yake kutoka shamba la Mifugo na kuwa Maeneo yaliyopimwa, kuchorwa na kugaiwa kwa kazi za Maendeleo. Ni matumaini ya Kamati kwamba kama ingepata fursa ya kwenda kuliona shamba hilo, baadhi ya changamoto zingeweza kutatuka kutokana na maelekezo na ushauri ambao Kamati ingeutoa.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu inaendelea kuitaka Wizara kwamba bado haja ya Kamati kulitembelea shamba hilo ni ya msingi ili kuweza kujua rasilimali za Serikali zinatumikaje, zinahifadhiwa vipi na kuendelezwa katika mazingira ya aina gani. Kwa vile Kamati yetu inafikia ukingoni, tunaishauri Kamati ijayo ya Fedha, Biashara na Kilimo iitake Wizara ikamilishe ahadi hiyo ili Kamati hiyo iweze kupata fursa ya kulitembelea eneo hilo na kuishauri Serikali yetu ipasavyo kwa kile watakachokiona na sio kukaa na kusubiri maelezo ya watendaji wa Wizara pekee. Tunaitanabahisha Wizara kwamba fedha nyingi za Wakulima na Wakwezi wa nchi hii zimetumika na zinaendelea kutumika katika uimarishaji wa shamba hilo.

PROGRAMU KUU YA MAENDELEO YA UVUVI

Mheshimiwa Spika,

Katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa na wavuvi wenye ujuzi wa kuweza kuvua uvuvi wa Bahari Kuu, Wizara imefanikiwa kuwaingiza katika meli za kigeni vijana 26 ili kupata uzoefu wa namna ya uvuvi huo unavyofanyika. Aidha, wavuvi vijana 25 wamepelekwa Chuo cha Uvuvi Mbegani - Bagamoyo kujifunza mbinu za uvuvi wa kisasa. Huu ni mwanzo mzuri ambao Wizara yetu ya Kilimo inahitaji kupongezwa ili rasilimali tulizonazo Zanzibar ziweze kuvunwa na kutumiwa kwa kuwanufaisha Wazanzibari wenyewe na sio kuwaachia watu wengine kunyonya utajiri wetu. Kamati inaitaka Wizara kuwatumia ipasavyo vijana hao kwa maslahi ya Taifa letu na sio kuwawacha wakazagaa mitaani baada ya kupata ujuzi wao.

Mheshimiwa Spika,

Kamati yetu inaipongeza Wizara ya Kilimo kupitia Kampuni ya Uvuvi kwa kuanza vyema utekelezaji wa majukumu yake kwani tayari Bodi imeshaundwa na kuingiziwa shilingi 2.2 bilioni kati ya jumla ya shilingi 7.0 bilioni za mtaji kutoka kwa Washirika wake yaani ZSSF, ZSTC, Shirika la Bima la Zanzibar na Shirika la Bandari kulingana na mgao waliokubaliana. Fedha hizo zimeelekezwa katika ununuzi wa Meli mbili za uvuvi zitakazokuwa na uwezo wa kuchukua wavuvi sita na kubeba tani 43 za samaki. Wizara tayari imeanza taratibu za zabuni na ‘quotation’ tayari zimeshatolewa. Kamati inaendelea kuisisitiza Wizara kuwa makini katika ununuzi huo kwa kununua meli zitakazokuwa mpya zenye thamani halisi ya fedha zinazohitajika.  

Mheshimiwa Spika,

Wizara ya kilimo imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalishia vifaranga vya samaki kiliopo hapo Maruhubi. Kuwepo kwa kituo hicho kutaleta faraja kubwa kwa wafugaji wetu wa samaki kuweza kupata vifaranga vya uhakika kwa lengo la kuwafuga kibiashara. Mradi huu ni mkubwa uliogharimu dola za kimarekani 943.94 milioni na unauwezo wa kuzalisha vifaranga milioni 10 vya samaki, majongoo 70 elfu na kaa 50 elfu. Kamati inashauri kwamba kwa vile huu ni mradi unaohitaji kuendelezwa hata baada ya kuondoka wawezeshaji, ni vyema Serikali ikahakikisha inakuwa na watendaji pamoja na wataalamu wa kutosha watakaomudu kuvaa viatu vyao ili mradi uweze kuishi na kutupatia faida kwa kipindi kirefu zaidi.

Mheshimiwa Spika,

Katika utekelezaji wa kazi za Kamati kwa mujibu wa kanuni zetu, Kamati ilitembelea kikundi cha wafuga pweza kiliopo Mtende Mkoa wa Kusini Unguja na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi hao kwa kuwachangia shilingi 1,500,000/- ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili. Kamati iligundua kwamba changamoto kubwa iliyopo katika kikundi hicho ni kukosa shughuli ya kufanya baada ya kumaliza uvunaji wa pweza wanaowafuga.  Kamati yetu imekichangia kikundi hicho na kuwashauri waanzishe utaratibu utakaowawezesha kupata shughuli ya kufanya baada ya kufunga uvunaji wa pweza ikiwemo kulima kilimo cha migomba na mazao mengine.  

PROGRAMU KUU YA MAENDELEO YA RASILIMALI ZA MISITU NA MALIASILI ZISIZOREJESHEKA

Mheshimiwa Spika,

Kamati imeridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Wizara kwa upande wa Unguja za kuanzisha na kuuendeleza utaratibu mpya na mzuri wa kulipia malipo ya Mchanga Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ). Kupitia utaratibu huo, Kamati inawataka Viongozi na Watendaji wa Wizara hii kuanzisha utaratibu huo katika Kisiwa cha Pemba. Kadhalika, Kamati imeitaka Wizara kuutumia utaratibu huu katika Rasilimali nyengine za mawe, kifusi na kokoto ili mianya ya uvujaji wa mapato ipungue kama si kuondoka kabisa na Serikali kujiongezea mapato kwani inaonekana mapato mengi yanapotea katika eneo hilo. Aidha, Kamati yetu inaiomba Serikali iwe inazifuatilia Bei Elekezi za Mchanga inazozitoa ili ziweze kufuatwa kikamilifu na wauzaji pamoja na wanunuzi wa mchanga huo.

Mheshimiwa Spika,

Kamati imeshuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya kuni linalotokana na ukataji mkubwa wa miti. Pamoja na juhudu za Wizara za kutoa mafunzo ya kuhimiza matumizi ya nishati mbadala pamoja na kufanya doria 104 zilizopelekea kukamata matukio 92 ya ukataji miti, matukio 13 ya ukamataji misumeno ya moto, kuwasilisha kesi mbili Mahakamani pamoja na kukamata misumeno ya moto 233 Unguja na Pemba lakini bado miti inakatwa sana kwa kutumia misumeno ya moto. Takwimu zinaonesha matumizi ya nishati ya kuni kwa mwaka huu yamefikia mita za ujazo 23,114 ukilinganisha na mita za ujazo wa 19,532.25 za mwaka jana. Kwa kweli takwimu hizo zinatishia kupotea kwa uoto wetu wa asili. Sambamba na hilo, Kamati katika kutekeleza majukumu ya kikanuni, ilitembelea msitu wa mikoko uliopo Ukongoroni na kushuhudia magogo ya mikoko iliyokatwa na kuona eneo hilo limebakia kuwa tupu. Hali hiyo inasababisha maji ya bahari kupata mwanya wa kuvamia katika maeneo ya ardhi yanayotumiwa kwa kilimo na makaazi ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika,

Lakushangaza, baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo Sheha wa Shehia ya Ukongoroni alikuwa mbele kutetea wananchi wake kwamba hawana kazi ya kufanya isipokuwa kujihusisha na ukataji wa mikoko kwa ajili ya utengenezaji wa kuni na tanu za mkaa. Viongozi wa namna hii ndio wanaoisababishia Serikali yetu kuonekana haichukui juhudi yoyote katika harakati za kupambana na uharibifu wa mazingira. Kamati yetu inaishauri Wizara inayoshughulikia Tawala za Mikoa kumchukulia hatua stahiki Sheha huyo wa Ukongoroni. Aidha, Kamati inaitaka Wizara ya Kilimo kuchukua hatua za kudhibiti matumizi ya Misumeno ya moto kama ilivyofanya Kisiwani Pemba. Kadhalika, Wizara isimamie ipasavyo Sheria ya Uhifadhi wa Maliasili za Misitu namba 10 ya mwaka 1996 pamoja na Kanuni zake ikiwemo kupiga marufuku usafirishaji wa kuni kutoka shamba kuja mjini. Hatua hizo kama zitatekelezwa kikamilifu, basi uteketezaji wa mikoko Zanzibar utabakia kuwa historia.

PROGRAMU KUU YA UENDESHAJI NA URATIBU WA WIZARA YA KILIMO

Mheshimiwa Spika,

Katika programu hii, kuna kifugu kinachotoa Huduma ya Ununuzi wa Vifaa vya Ofisi (HL01050101) ambacho mwaka jana kilipangiwa pesa nyingi shilingi 269.63 milioni ambazo hazikukidhi kikamilifu mahitaji ya upatikanaji wa vifaa vya kutosha katika Wizara hii, lakusikitisha mwaka huu ndio kimezidi kupunguziwa bajeti. Wakati Kamati yetu ilipokuwa ikipitia kifungu hiki kilikuwa kimepangiwa shilingi 10.31 milioni sawa na upungufu wa shilingi 259.32 milioni. Tunaishukuru Wizara kwa kukiangalia upya kifungu hicho na hatimae kukiongezea fedha hadi kufikia shilingi 50.32 milioni kama inavyoonekana katika kitabu tulichokabidhiwa. Pamoja na marekebisho hayo, Kamati yetu bado inaieleza Wizara kwamba kifungu hicho kinahitaji kuongezewa tena bajeti vyenginevyo Wizara inaweza ikakosa hata fedha za kununnulia vifaa vya kutosha vya kuandikia na kuishia kukopa jambo ambalo litaleta picha mbaya kwa Wizara hii na Serikali kwa ujumla.  

Mheshimiwa Spika,

Kamati inaipongeza tena Wizara hii kwa kufufua matumaini mapya ya kuyaendeleza mashamba ya mpira ambayo yalikuwa yanatumika kiholela na kuikosesha Serikali mapato. Kwasasa Wizara ya Kilimo imepanga kuyaendeleza mashamba hayo kwa kupanda mazao mbadala yakiwemo pililimanga na vanila na kuondosha dhana iliyokuwepo kwamba mashamba hayo yamezeeka na mipira iliyopo inahitaji kukatwa. Matumizi mapya hayo yatayaongezea thamani mashamba hayo na kuweza kutumika tena kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika,

Kwa namna ya pekee naomba kutumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Rashid Ali Juma; Naibu Waziri Mheshimiwa Dr. Makame Ali Ussi; Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Watendaji wengine wote wa Wizara hii kwa juhudi wanazozichukua katika kutekeleza majukumu yao pamoja na mashirikiano yao ya dhati waliyotupatia wakati wote wa kupitia na kujadili Bajeti ya Wizara hii. Kwa vile wao ni Viongozi wapya katika Wizara hii, Kamati inawaeleza kwamba “wasiwe na sifa kama ya muhogo ambapo ukiwa mtamu sana watu watautafuna mpaka waumalize na ukiwa mchungu sana watu watashindwa kuutumia”.
Mheshimiwa Spika,

Mwisho kabisa, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa kunisikiliza kwa utulivu wa hali ya juu wakati wote nilipokuwa nikiwasilisha hotuba hii. Kwa vile Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo imepitia, imejadili na kuyakubali mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hii ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na uvuvi. Sasa naomba nichukue fursa hii kwa mara nyengine nikuombeni nyinyi Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili muijadili, mutoe ushauri pamoja na mapendekezo yenu na hatimae muiunge mkono bajeti hii ili tumuwezeshe Waziri kwenda kutekeleza na kufanikisha yale waliyojipangia katika mwaka wa Fedha wa 2018/2019 na baadae nasi tupate fursa ya kuja kumuhoji kwa kile alichoingiziwa na matokeo halisi ya kile alichokitekeleza.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kusema hayo machache, Kwa niaba ya Mwenyekiti na Kamati yetu ya Fedha, Biashara na Kilimo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika,

Naomba kuwasilisha.
Asante sana,

……………………..,
Hamida Abdalla Issa,
Makamo Mwenyekiti
Kamati ya Kudumu ya Fedha, Biashara na Kilimo,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.