UONGOZI wa Kampuni
ya Kimataifa ya Ujenzi ya China (CRCC) kupitia Tawi la Kampuni yake ya Uhandisi
wa Ujenzi ya nchini humo (CCECC) imeahidi kujenga barabara ya
Bububu-Mahonda-Mkokotoni kwa wakati uliopangwa na kwa ubora zaidi ili
kuendeleza sifa ya kuwa Kampuni yenye ubora duniani.
Rais wa Kampuni hiyo Zhuang Shangbiao aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, kiongozi huyo ambaye
amefuatana na Rais wa Kampuni ya (CCECC) Zhao Dianlong alimuhakikishia Rais Dk.
Shein kuwa Kampuni yake ya (CCECC), itaijenga kwa kiwango stahiki barabara hiyo
yenye urefu wa kilomika 31 kutokana na uzoefu mkubwa uliyonao.
Kiongozi huyo pia, alimueleza Rais Dk.Shein azma
ya Kampuni yake ya kuanzisha kiwanda kikubwa cha kusarifu samaki huko kisiwani
Pemba.
Pamoja na hayo, uongozi huo ulitoa shukurani kwa
kupata fursa ya kujenga barabara hiyo pamoja na kuahidi kufanya vizuri ili
utakapotokea mradi mwengine kampuni yake iweze kushinda na kuendelea na miradi
ya ujenzi hapa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa azma yao ni kufanya kazi hapa
Zanzibar na kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja
na kuendelea kuiunga mkono jamii ya watu wa Zanzibar huku akitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe
wake.
Alieleza kuwa Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka
1948 ina ofisi zake mjini Hong Kong na Shanghai China ina matawi 500 ya
Makampuni yake duniani na tayari imeshaekeza katika nchi 118 duniani ambapo
kazi yake kubwa ni ujenzi wa nyumba, reli, ujenzi wa miundombinu kama vile
barabara ambapo tayari kwa upande wa Bara la Afrika wana matawi katika nchi
zote.
Aliongeza kuwa Kampuni hiyo tayari imejenga
barabara ya kurukia na kutulia ndege pamoja na sehemu ya maegesho katika kiwanja
cha ndege cha Kimataifa cha Angola, km 700 za reli kutoka Addis Ababa hadi
Djibout pamoja na kilimota 1300 za reli katika nchi mbali mbali za Bara la
Afrika.
Kwa maelezo ya kiongozi huyo, Kampuni hiyo pia
ndiyo iliyojenga reli ya pamoja ya (TAZARA) yenye urefu wa kilomita 1,860
ambapo ukaguzi wa awali wa ujenzi wa njia ya reli hiyo ulifanywa mwaka 1968 na
ujenzi ulianza mwaka 1970 hadi Julai mwaka 1976 kutoka bandari ya Dar-es-Salaam
Tanzania hadi New Kapiri Mposhi Zambia.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa mbali ya ujenzi
wa reli hiyo, Kampuni hiyo imejenga majengo makubwa barabara, madaraja huko
Tanzania Bara.
Mbali ya ujenzi wa barabara hiyo ya
Bububu-Mahonda-Mkokotoni yenye kilomita 31 pia, Kampuni ya CCECC itajenga
barabara ya Matemwe-Muyuni yenye km 7.58 na barabara ya Fuoni-Kombeni km 8.59 pamoja na barabara ya Pale hadi
Kiongele km 4.61.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimpongeza kiongozi huyo pamoja na ujumbe wake
kwa kufanya uwamuzi wa kuja Zanzibar na kuekeza kuwa hiyo ni ishara nzuri ya
kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa China na Zanzibar
zina historia tokea karne ya 11 na 12 ambapo wananchi wa nchi hiyo walifika
Zanzibar na kuanza kuishi hadi hivi leo hatua ambayo iliimarika zaidi mara
baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo nchi hiyo ilianza
kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuanza kuleta Madaktari kutoka Jimbo
la Nanjing.
Dk. Shein aliongeza kuwa Zanzibar na China si
marafiki tu bali ni ndugu kutokana na historia iliyopo ya pande mbili hizo
kwani China imeweza kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za
maendeleo ikiwemo sekta ya viwanda, kilimo, habari, afya, michezo na nyenginezo.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa
na azma ya Kampuni hiyo ya kutaka kujenga kiwanda cha kusarifu samaki kwani
muelekeo na Sera ya Zanzibar katika uchumi wake ni kuimarisha uchumi wa Bahari (uchumi
wa buluu).
Aliongeza kuwa Zanzibar ina rasilimali nyingi sana
za bahari lakini bado haijawa na uwezo wa kuvua samaki kwa njia za kisasa kwani
samaki wengi wako katika bahari kuu ambapo kutokana na kutokuwepo kwa vifaa na
nyenzo zikiwemo boti za kisasa bado hawajaweza kuvuliwa.
Hivyo, alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa
kiasi kikubwa kuifanya Zanzibar iweze kutekeleza uchumi wa viwanda kama ilivyo
jiwekea kwa upande wake na Tanzania Bara katika kutekeleza uchumi huo wa
viwanda kwa kuweka mikakati maalum.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliuahidi uongozi
huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari na inaikaribisha kuja
kuekeza katika sekta hiyo ya uvuvi ambayo pia, itakuwa ndio njia pekee ya
kuendeleza miradi mengine kwa Kampuni hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment