Na.Abdi Shamnah.
WASHIRIKI wa
mkutano uliotathmini juhudi za viongozi wa Dini katika mapambano dhidi ya
vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto, wamesema kuwepo kwa
kumbi za starehe katika maeneo ya kambi za vyombo vya Ulinzi na Usalama,
kunachochea ongezeko la vitendo vya udhalilishaji miongoni mwa jamii.
Wamesema kuwepo
kwa kumbi huru zenye kutowa fursa ya watu wote kuingia na kustarehe, ikiwa
pamoja na kunywa pombe na kucheza disco, kumeongeza chachu ya kufanyika vitendo
vya udhalilishaji, ikiwemo ubakaji.
Changamoto
hiyo imeibuliwa na Masheikh na viongozi wa dini ya Kikristo katika mkutano wa robo mwaka (April hadi Juni,
2018) uliotathmin juhudi ya viongozi wa dini
katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji katika Wilaya zote za
Unguja.
Mkutano huo
umefanyika katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe, ukiwa chini ya uratibu wa
Idara ya Wanawake.
Wamesema
uwepo wa Baa katika maeneo ya Dunga, Mtoni, Entebe na kwengineko nchini,
kumekuwa chachu inayochochea ongezeko la vitendo vya udhalilishaji, kwa msingi
kuwa wanaozuru maeneo hayo hawazingatii maadili ya dini zao.
Wamesema
kumbu kumbu znaonyesha kuwa kumewepo matukio mengi ya udhalilishaji na hata mauaji
, ambapo baadhi ay watu wanaokwenda kwenye kumbi hizo huwasibu, hususan nyakati
za usiku wa manane pale wanaporejea nyumbani.
Washiriki
hao wameitaka Serikali kuingilia kati na kurejesha mfumo wa zamani, ambapo
vikosi hivyo vya ulinzi na usalama, vilikuwa na utaratibu maalum wa raia
kuingia kambini, tofauti na ilivyo sasa.
“Masuala ya
udhalilishaji wa kijinsia, katika vyombo vya ulinzi ndiko yanakolelewa kupitia
kumbi za madisko na baa, yako huru kila mmoja anaingia na kufanya atakalo,
yafaa Serikali iingilie kati jambo hili’, alisema mmoja wa masheikh
walioshiriki mkutano huo.
Katika hatua
nyengine ,washiriki hao walieleza kujitokeza kwa matukio kadhaa ya
udhalilishaji katika Wilaya zao, huku walimu wa madrasa wakitajwa katika
matukio mbali mbali kuhusika na vitendo hivyo.
Aidha,
washiriki hao wakaiomba Serikali kupitia
Wizara ya Afya kufanya uchunguzi wa waathirika wa udhalilishaji kuambatana na
ukuaji wa tekonolojia.
Walisema
katika hali ilivyo hivi sasa, ni jambo lisilokubalika kwa madaktari
kuwachunguza waathirika wa udhalilishaji ama kwa kuwaangalia au kuwaingiza
mikono katika sehemu zao za siri.
“Hivi sasa
dunia imepiga hatua kubwa kiteknolojia, kiasi ambacho uchunguzi wa mtu
alieingiliwa au kunajisiwa hauhitaji tena
daktari kuanza kumchungulia au kumtia mikono mdhuriwa, hiyo ni kuendelea
kumdhalilisha, mtu ambae tayari ameshadhalilishwa’, alisema mmoja wa washiriki
hao.
Mapema,
akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya wanawake, Nasima Haji Chum
alisema dini ni zana muhimu katika kubadili tabia za waumini kutoka vitendo
viovu kuelekea vitendo vyema.
Aliwataka
masheikh na viongozi wengine wa dini kutumia nafasi zao kuendelea kuwaongoza
waumini wao kutekeleza vitendo vyema, ili kuwa na jamii iliostaarabika na yenye
kuishi kwa amani.
Aidha, aliwataka
washiriki hao kutumia mkutano huo kubadilishana uzoefu , sambamba na kila mmoja
wao kutambuwa jukumu lao na kuhakikisha yote wanayoazimia yanafanyiwa kazi, ili
kufikia malengo yaliowekwa.
“Ni vyema
mkaendelea kuvitumia vyombo vya habari kikamilifu ili kuitahadharisha jamii juu
ya athari za kuwepo unyanyasaji katika jamii”, alisema.
Pamoja na
mambo mengine, viongozi hao wa dini walikuwa na jukumu la kutoa taaluma kwa
wananchi juu ya kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika
maeneo yao, ambapo watu 15,504 walifikiwa kati yao wanawake 8,491 na wanaume
7,013 kutoka katika Wilaya zote za
Unguja.
No comments:
Post a Comment