Habari za Punde

Mwananchi wa Shehia ya Kiungoni Atuhumiwa Kubaka.


Na.Zuhura Juma -Pemba.
ALI Suleiman Hemed ,Mkaazi wa Shehia ya Kiungoni anatuhumiwa kumbaka mtoto wa mjomba wake mwenye umri wa miaka 13 mkaazi wa shehia hiyo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari mtoto anaetuhumiwa kufanyiwa kitendo hicho ,  alisema tukio hilo lilitokea saa 2:00 usiku wakati akirudi dukani.

Alisema kijana huyo mwenye mke na mtoto mmoja, alimfuata nyuma bila yeye kujua, ambapo alipofika sehemu yenye kiza cha Miembe alimkamata na kumvua nguo kisha kumbaka.

“Kila siku alikuwa ananiambia ananitaka lakini mimi nilikataa, siku ya tukio nilitumwa dukani usiku nikiwa na ndugu yangu, wakati wa kurudi nilikuwa peke yangu maana ndugu yangu alikwenda kuangalia televisheni”, alisema mtoto huyo.

Alieleza   alipofika sehemu ya Miembeni  alimuona mtuhumiwa anamfuata ambapo alimwambia “kila siku nakutafuta lakini leo hutoki” ambapo alimkamata na kuchukua kanga aliyokuwa amevaa na kumtia mdomoni mwake, kisha kumbaka.

“Niliporudi nyumbani ilikuwa nalia tu sijamwambia mama, ndipo ilipofika asubuhi akanipeleka Hospitali Micheweni kunipima ujauzito, lakini daktari alinihoji na nikamwambia kuwa nimebakwa”, alieleza mtoto huyo.

Mtoto huyo alisema, anamchukia sana kijana huyo na hataki hata kumuona kutokana na kitendo cha ukatili alichomfanyia na kuiomba Serikali kupitia vyombo vya Sheria kumchukulia hatua za kisheria, ili iwe funzo kwake na kwa wengine.

“Kwa kweli naumia sana kila ninapokumbuka, kwani wazazi wangu hawasemi chochote juu ya hili kwa sababu ya kuogopa hasama ndani ya familia, naomba Serikali inisaidie, kutokana na kitendo nilichofanyiwa”, aliomba msaada mtoto huyo.

Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo, alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa mwezi wa tano, ingawa hawezi kwenda kuripoti popote kutokana na kile alichosema kuwa analinda ndoa yake.

“Nina watoto watano, hapa wanafamilia wananitafutia sababu tu niachwe na mimi nawaonea huruma kuwaacha watoto wangu wadogo, nimeona bora nikae kimya nivumilie machungu haya”, alisema mama huyo.

Nae Baba mzazi wa mtoto huyo, alieleza   kutokana na kuogopa kususiwa na wanafamilia, wanaogopa kwenda kwenye vyombo vya Sheria kuripoti na kuomba Serikali kuwasaidia, ili mtoto wake aweze kupata haki yake.

“Siku ninayomuona huyo kijana mtaani, basi hata kufutari siwezi kutokana na machungu yaliyonijaa kwenye moyo wangu, lakini sina la kufanya, maana hapa Kiungoni ukishitaki tukio kama hili, unasusiwa na watu wote”, alisema baba huyo.

Babu wa mtoto huyo alisema, wanaogopa hasama katika familia na ndio maana wamekaa kimya bila kwenda kuripoti kwenye vyombo vya sheria.

Sheha wa shehia hiyo, Omar Khamis Othman, alisema   alipata taarifa siku nne zilizopita kwamba mtoto huyo alifanyiwa kitendo cha ubakaji, ingawa wazazi hawako tayari kufika kwenye vyombo vya sheria kuripoti,kutokana na kile wanachodai wanaogopa uhasama ndani ya familia yao.

“Kutokana na taarifa za mtoto mwenyewe ,tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa mwezi wa tano, lakini familia ilinyamaza kimya kutokana na rushwa muhali iliyowatawala, mpaka nazungumza na nyiyi hawako tayari kwenda kuripoti kunakohusika”, alisema Sheha.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Kisiwani Pemba, Asha Mussa , alisema   watashirikiana na wazazi pamoja na viongozi wa shehia katika kuhakikisha tukio hilo linaripotiwa na mtoto anapata haki zake za msingi.

Mkuu wa Dawati la kijinsia la Wanawake na Watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba, Khamis Faki Simai, alisema   bado hawajapokea taarifa za mtoto huyo katika dawati hilo.

Matukio ya udhalilishaji yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na wanajamii kuwa na muhali kwa kuogopa Uhasama katika kuripoti matukio hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.