Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ajumuika katika Iftar na Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ikulu.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewahimiza wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla kuyatumia mafunzo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuendeleza umoja, upendo na mshikamano walionao.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekitiwa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu aliyasema hayo katika futari maalum iliyoandaliwa na Rais kwa ajili ya wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa na serikali, iliyofanyika kwenye viwanja vya Ikulu  Mjini Zanzibar.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alihudhuria ambapo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae kwa upande wake aliungana pamoja na wananchi wa Mkoa huo pamoja na viongozi mbali mbali wanawake wa kitaifa katika futari hiyo maalum.

Dk. Shein alieleza imani yake kuwa umoja, upendo na mshikamano uliopo nchini iwapo utaendelezwa utaweza kuleta faida kubwa kwa wananchi wote pamoja na vizazi vijavyo.

Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa waalikwa wote waliofika katika hafla hiyo kwa kuitikia wito na mwaliko wake huo wa kuja na kutimiza kitendo cha  kufutari kwa pamoja.

Aliongeza kuwa shughuli hiyo ni mwendelezo wa kufutarisha wananchi wote wa Unguja na Pemba katika futari maalum anazoziandaa Alhaj Dk. Shein kwa ajili ya wananchi hao pamoja na viongozi mbali mbali ambao hufutari nao pamoja.

Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwatakia kila la kheri wananchi wote Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika kukamilisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasisitiza kuendelea kuiombea dua nchi na wale ambao watajaaliwa kumaliza salama  mwezi huo mtukufu aliwatakia Idd njema na yenye baraka tele.

Dk. Shein alianza ziara za kuwafutarisha wananchi pamoja na viongozi katika mikoa yote ya Zanzibar katika ziara zilizoanza kwenye Mkoa wa Kaskazini Pemba huko katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Michweni mnamo Juni 5, 2018 sawa na mwezi 20 Ramadhan na kumalizia jana katika Mkoa huo wa Mjini Magharibi hapo katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.