WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, limefanikiwa kuuzima na kuudhibiti moto mkubwa
uliotokea jana asubuhi, kwenye jengo la biashara la ghorofa mbili linalomilikiwa na Ndugu
Jonasi Nyagawa katika eneo la Kariakoo kwenye Makutano ya Mtaa wa Agrey na Livingstone
jijini Dar es Salaam.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kuudhibiti na kuuzima moto huo kwa asilimia 100,
hivyo kuzuia madhara na hasara kubwa ambayo ingeweza kutokea kwa wafanyabiashara
wanaolizungula eneo hilo, pamoja na eneo la chini la jengo ambalo lina maduka ya
wafanyabiashara.
Moto huo ulioanza majira ya saa 4:05 asubuhi, ulianzia kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo
hilo na kusambaa hadi ghorofa ya pili. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji baada ya kupata taarifa
lilifika eneo la tukio na kuudhibiti na kuuzima moto huo, ili usiweze kusambaa sehemu nyingine.
Hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
linaendelea na Uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.
Moto ni tukio la hatari sana, hivyo watu wanatakiwa kukaa mbali wanapoona tukio la moto,
kwani kusogea karibu na moto unapotokea kunaweza kuwasababishia madhara makubwa
kutokana na moshi, kuangukiwa na kuta pamoja na kutokea kwa milipuko inayotokana na
bidhaa mbalimbali zinazoweza kusababisha milipuko.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa wito kwa wamiliki na wafanyabiashara wote nchini,
kuzingatia kanuni za kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwenye maeneo yao, ili kuzuia
majanga ya moto kutokea pamoja na kutoa taarifa mapema ya matukio ya moto au maokozi,
kwa kupiga simu ya dharura namba 114 ambayo ni bure kwa mitandao yote nchini.
Imetolewa na:
Joseph K. Mwasabeja
Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
No comments:
Post a Comment