Habari za Punde

Hutuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Tanzania Mhe. Dkt.Phlip I. Mpango (MB), Akiwasilisha Bungeni Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi Kwa Mwaka 2018/19


Waziri wa Fedha na Mipango,Mhe. Dkt. Philip I. Mpango  (MB),Akiwasilisha Bungeni Hutuba ya Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019


I.      UTANGULIZI
1.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.

2. Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2018 ambayo ni sehemu ya bajeti hii.

3.  Mheshimiwa Spika, ni heshima kubwa na upendeleo wa hali ya juu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha bajeti ya tatu ya Serikali ya awamu ya tano. Hivyo, namshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu neema nyingi, utulivu na amani na kwa kuniwezesha kuwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa wananchi wa Tanzania kwa mara ya tatu. Pili napenda kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kiongozi wetu shupavu; kiongozi anayeaminiwa na kutumainiwa na wananchi, hasa wanyonge; kiongozi anayechukia na kupiga vita rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo; na Rais anayejipambanua kwa kufanya maamuzi magumu ya kulinda rasilimali za Taifa. Ninampongeza kwa kazi kubwa ambazo ameendelea kuzifanya tangu aliposhika hatamu za uongozi wa Taifa letu, ambazo zimepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa sana katika kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu tu ya utawala wake. Napenda niyataje mambo kumi tu aliyothubutu kutenda na kuiletea nchi mafanikio makubwa:


(i)         Kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma: Ametekeleza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uamuzi wa Chama Tawala wa mwaka 1972 wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma. Aidha, kwa mamlaka aliyo nayo amepandisha hadhi ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji kuanzia tarehe 26/4/2018;
(ii)       Kujenga ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani: Amejenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5 kuzunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya Simanjiro uliogharimu shilingi bilioni 5.42. Lengo likiwa ni kudhibiti uchimbaji na uuzaji holela wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee na kuliingizia Taifa mapato. Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2018 Serikali imefanikiwa kukusanya mrabaha wa shilingi milioni 714.6. Kati ya kiasi hicho, shilingi milioni 614.6 kilitokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo. Kiasi hicho kilichokusanywa kutoka kwa wachimbaji wadogo kinazidi jumla ya makusanyo ya mrabaha wa miaka mitatu iliyopita. Kiasi kilichokusanywa na Serikali kilikuwa shilingi milioni 116.8 (2015), shilingi milioni 71.8 (2016), na shilingi milioni 147.1  (2017);
(iii)     Kudhibiti uuzaji wa makinikia nje ya nchi na kutunga sheria kuwezesha nchi kunufaika na rasilimali zake: Amezuia usafirishaji wa makontena 277 ya makinikia nje ya nchi yenye thamani ya kati ya shilingi bilioni 829.4 na shilingi bilioni 1,438.8 na kuagiza kutungwa kwa sheria mpya za mfano katika Afrika kuwezesha nchi zenye maliasili kunufaika na rasilimali hizo. Sheria hizo ambazo zilipitishwa na Bunge lako Tukufu ni:
(a)       Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 (The Natural Wealth and Resources - Permanent Sovereignity Act, 2017);
(b)       Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017 (The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re- Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017; na
(c)       Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2017 (The Written Laws - Miscellaneous Ammendments ) Act, 2017.
(iv)     Kutoa elimu msingi bila ada na kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya mara nane: Ametoa elimu msingi bila ada ambapo kila mwezi Serikali inalipa shilingi bilioni 20.8. Kutokana na hatua hiyo, uandikishwaji wanafunzi wa darasa la kwanza umeongezeka kutoka watoto 1,568,378 mwaka 2015 hadi watoto 2,078,379 mwaka 2018. Aidha,  uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza nao umeongezeka kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 562,695 mwaka 2017. Kadhalika, ameongeza fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo mgao uliotolewa mwaka 2017/18 ni shilingi bilioni 409.9 ikilinganishwa na matumizi halisi ya shilingi bilioni 367.4 mwaka 2015/16. Idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo imeongeza kutoka wanafunzi 96,589 mwaka 2015 hadi 122,623 mwaka 2017. Katika sekta ya afya, amethubutu kuongeza bajeti kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kufikia shilingi bilioni  269 mwaka 2017/18  kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16, hivyo kuimarisha huduma za afya;

(v)       Ununuzi wa ndege mpya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Amefufua Shirika la Ndege la Tanzania kwa kufanya maamuzi magumu ya kununua ndege mpya tatu aina ya Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ambazo tayari ziko nchini na zinafanya safari za ndani. Aidha, ndege kubwa nyingine tatu (3), moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na ndege mbili  aina ya Bombardier CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja zitawasili nchini baadae mwaka huu. Kadhalika, Serikali imekamilisha taratibu za kupata ndege ya pili kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na malipo ya awali yamekamilika;
(vi)     Kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi: Amedhibiti matumizi yasiyo ya lazima hususan safari za watumishi wa Serikali nje ya nchi, kuondoa watumishi hewa 19,708 waliokuwa wanalipwa mshahara wa jumla ya shilingi bilioni 19.8 kwa mwezi, na watumishi 14,404 wenye vyeti vya kughushi waliokuwa wanalipwa mshahara wa jumla ya shilingi bilioni 15.5 kwa mwezi, ambazo zote hizo zimeokolewa. Aidha, chini ya utawala wake, nidhamu katika utumishi wa umma imeimarika na ameanzisha Mahakama ya mafisadi ili kupambana na mafisadi wanaonyonya uchumi wa nchi;
(vii)   Ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR): Ameanza ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR). Awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km 205) na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma (km 422) tayari zinatekelezwa. Awamu zote mbili zitagharimu takriban Dola za Marekani bilioni 3.14;
(viii)  Ujenzi wa mradi wa umeme katika bonde la mto Rufiji: Amefanya uamuzi wa kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao nao ulikuwa ndoto ya Baba wa Taifa utakaozalisha MW 2,100 utakapokamilika nao umeanza katika hatua za awali;
(ix)     Kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani: Ametekeleza ahadi yake kwa Watanzania kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ukwepaji kodi, hatua ambazo zimewezesha Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi tirioni 1.3 kwa mwezi;
(x)       Kuendeleza umeme vijijini na kusitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (IPPs): Ameendeleza utekelezaji wa mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini kupitia REA Awamu ya Tatu kwa ufanisi mkubwa, ambapo ndani ya miaka miwili na nusu ya utawala wake jumla ya vijiji 557 vimeunganishwa umeme. Vijiji hivyo vimetokana na utekelezaji wa miradi ya REA II na REA III ya kuongeza msongamano (densification), mkongo (backbone) na ule wa kusafirisha umeme Makambako - Songea. Aidha, amesitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (Independent Power Producers – IPPs) ambayo ilikuwa inaigharimu Serikali fedha nyingi. Vile vile, bila yeye mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga usingepatikana na tayari ujenzi unaendelea;

4.         Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi sana makubwa (barabara, meli, madaraja, maji, usimamizi wa sekta ya fedha n.k.) ambayo Jemadari huyu ametekeleza, lakini kwa uchache wa muda siwezi kuyataja yote. Haya yote ni ushahidi usio na mashaka kwamba Tanzania chini ya Rais Magufuli imeshika kasi ya maendeleo. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuchangia katika jitihada hizi za Mheshimiwa Rais kujenga Tanzania mpya. Maeneo matatu ya msingi sana kwa kila mwananchi kuwajibika ni: (i) uzalendo kwa nchi yetu; (ii) kupiga vita wizi, ubadhirifu na ufisadi; na (iii) kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi.

5.         Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo za dhati kwa Rais wetu, napenda kumshukuru kwa moyo wangu wote kwa kuendelea kuniamini na kuniongoza katika kazi zangu za Waziri wa Fedha na Mipango. Hata pale nilipoelemewa na kazi na kulaumiwa kwamba waziri huyu ni bahili mno katika kutoa fedha na baadhi wakinipaka tope la kiburi, alinitia moyo. Niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Rais kwa nini alinitwika mimi kazi hii nzito kama msalaba wa zege, tena bila matumaini ya kutokea mtu mfano wa Simon wa Kirene katika Biblia wa kuja kunipokea mzigo huu!. Yeye alinijibu kwamba “Mungu atawatuma malaika wake watakusaidia!” na akaongeza kwamba “lazima watu wachache tuwe tayari kuumia kwa faida ya Watanzania wengi maskini”. Naomba nikiri kuwa, majibu hayo yalinichoma na kunikumbusha sala ya wana “Opus Dei” katika mateso isemayo “Mapenzi ya Mungu, yenye haki na yanayopendeza sana, yafanyike, yatimizwe, yasifiwe na kutukuzwa kuliko vitu vyote milele. Amina. Amina.” Baada ya hapo, nilipata amani ya kuendelea katika utumishi huu. Asante sana Mheshimiwa Rais. Najua unasikiliza!.

6.         Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumsaidia Rais kuongoza Taifa letu kwa hekima na uadilifu. Kadhalika, ninatoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuiongoza Zanzibar kwa busara, jambo ambalo limepelekea wananchi wa Zanzibar kuishi katika hali ya amani na utulivu mkubwa kwa kipindi cha miaka saba na nusu sasa. Aidha, ninampongeza sana Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, kwa kuwa kapteni hodari wa timu ya Serikali hapa Bungeni na kwa kumsaidia Rais kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala CCM ya mwaka 2015 – 2020. Vile vile, ninawapongeza wakuu wa mihimili mingine ya dola, nikianza na wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa kwa kuliongoza Bunge kwa umahiri; na Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamis Juma,  Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kazi nzuri ya kuongoza chombo cha utoaji haki. Napenda vile vile kumpongeza Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri kwa utumishi uliotukuka.

7.         Mheshimiwa Spika, ni vema pia niwapongeze waheshimiwa wenza wa viongozi wakuu wa kitaifa kwa umuhimu wao wa kipekee. Niruhusu niwataje kwa majina yao Mwalimu Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir, Mama Mwanamwema Shein, Mwalimu Mary Majaliwa, Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga, na Mama Marina Papadopoulos Juma. Tunawapongeza na kuwashukuru kwa kuwawezesha viongozi wetu wakuu wa kitaifa kutekeleza vizuri majukumu yao kwa utulivu, hamasa na tabasamu kutokana na mapenzi makubwa wanayopata nyumbani.

8.         Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao ni Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Ali Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers William Sianga; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias Andengenye. Mimi na Watanzania wenzangu tunawapongeza kwa dhati kabisa viongozi hawa, pamoja na makamanda, askari na watumishi wote wa vyombo hivi nyeti kwa kuendelea kuilinda nchi yetu kwa ushupavu, kudumisha amani na usalama na kuwawezesha wananchi wote wa Tanzania kufanya shughuli za maendeleo kwa utulivu. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Dkt Adelardus Lubango Kilangi kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na ninamshukuru kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2018.

9.         Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii pia kutoa shukrani mahsusi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Jitu V. Soni, Mbunge wa Babati Vijijini. Maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya Bajeti wakati wa kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayoiwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, ulikuwa wa kizalendo na wenye tija. Aidha, ninawapongeza Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya kamati za kisekta katika kuboresha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19 ili kuwapatia wananchi wa Tanzania huduma bora zaidi.

10.    Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa mwaka 2017/18, dhima ya bajeti ya mwaka 2018/19 kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia uhalisia wa nchi yetu ambao sisi wote tunaufahamu, kwa maana ya changamoto kuu za kiuchumi na kijamii zinazotukabili, fursa tulizo nazo, mafanikio hadi sasa na malengo yetu kama Taifa. Naomba nifafanue haya kwa kifupi:


a)  Changamoto
(i)         Bado tuna kiwango kikubwa cha umaskini ambapo taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kiwango cha umaskini kimepungua kidogo kutoka asilimia 28.2 (2011/12) hadi asilimia 26.4 (2015/16). Matarajio ni kuwa Utafiti wa Matumizi ya Kaya unaoendelea hivi sasa utatupatia taarifa nzuri zaidi ya kuendelea kupungua kwa umaskini kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Taifa umeendelea kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.0 kwa mwaka katika miongo miwili sasa;
(ii)       Ukosefu wa fursa za ajira hasa kwa vijana, ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira. Vile vile kati ya vijana wanaohitimu masomo yao wapatao 800,000 kila mwaka, uwezo wa Serikali kuajiri ni wastani wa watu 40,000 tu;
(iii)     Sekta ya kilimo (inayojumuisha mazao, mifugo na uvuvi) ambayo inaajiri asilimia 66 ya Watanzania na inachangia asilimia 30 ya Pato la Taifa inaendelea kukua kwa kasi ndogo ya wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita kutokana na uwekezaji mdogo, tija ndogo na kutegemea mvua, sambamba na mchango mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa wa asilimia 5.5;
(iv)     Mahitaji makubwa ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii (hasa maji, afya na elimu bora) na yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu (asilimia 3.1 kwa mwaka). Aidha, hali ya miundombinu ya umeme, usafiri na usafirishaji (barabara, reli, usafiri wa anga na majini) bado haikidhi mahitaji ya uchumi kukua kwa kasi zaidi na kugusa wananchi wengi. Mathalani, mtandao wa barabara nchini ni kilomita 86,472 ambapo ni asilimia 9.7 tu ndiyo za kiwango cha lami. Aidha, mahitaji ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani bado ni makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji. Mitambo iliyopo kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha Megawati 1,424.6 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya Megawati 3,000 ili kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa viwanda; na
(v)       Wigo mdogo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo uwiano wa mapato ya ndani na Pato la Taifa ni takriban asilimia 15.0 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.0 kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
b) Fursa
11.    Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti hii pia yamezingatia fursa mbalimbali tulizo nazo katika Taifa letu hususan nguvukazi kubwa ya Taifa ambao ni vijana; rasilimali na fursa nyingi tulizonazo katika kilimo (mazao, mifugo, na uvuvi); madini; gesi; vivutio vya utalii; viwanda vya huduma za kilimo (agri-business); vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme; biashara na huduma za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.

c) Mafanikio
12.    Mheshimiwa Spika, bajeti hii pia imezingatia mafanikio tuliyopata hadi hivi sasa ambayo hatuna budi tuyaimarishe na nitayaeleza kwa muhtasari katika sehemu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti.
d) Malengo
13.    Mheshimiwa Spika, bajeti hii vile vile imeandaliwa kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020. Malengo makuu ni kuondokana na umaskini na kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati (Middle Income Countries) ifikapo mwaka 2025.

14.    Mheshimiwa Spika, changamoto, fursa mafanikio na malengo niliyoyaeleza sasa hivi lazima yaende pamoja na wajibu upande wa Serikali, sekta binafsi, wadau wengine na mwananchi mmoja mmoja, wa kuzipatia majibu changamoto hizo na kuchangia ipasavyo katika jitihada za kulipeleka Taifa letu mbele. Tutafanya hivyo ikiwa kila mwananchi atafanya kazi na kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya maendeleo yake na ya Taifa. Aidha, ni muhimu pia tuendelee kujenga na kutumia ubia wa kimkakati (harness strategic partnerships). Ujumbe wangu kwa Watanzania kupitia bajeti hii ni kuwa, lazima tuendelee kufanya chaguo gumu (tough choices) katika kuelekeza rasilimali kidogo tunazokusanya ili tuweze kuzishinda changamoto hizo zilizoko mbele yetu. Ukweli ni kuwa, mabadiliko ni magumu na mara nyingi yanapingwa!. Hivyo, lazima tuwe imara, tukusudie kufanikiwa na tutumie vizuri fursa na uwezo wa Watanzania, sekta binafsi na Serikali ili kufikia azma yetu.

15.    Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma leo asubuhi, nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka 2017, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, mafanikio yetu na changamoto tulizokumbana nazo na niliainisha pia maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2018/19. Katika hotuba hii nitajikita zaidi katika masuala ya kibajeti, nikianza na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18, hatua muhimu zitakazopewa msukumo zaidi upande wa matumizi katika mwaka ujao wa fedha, maboresho ya mfumo wa kodi na tozo mbalimbali na mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018/19.



II.      TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2017/18
Mwenendo wa Mapato
16.    Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi trilioni 21.89 sawa na asilimia 69 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi trilioni 31.71 Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:

A.                Mapato ya Ndani
17.    Mheshimiwa Spika, Mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi trilioni 14.84 ikilinganishwa na lengo la kukusanya shilingi trilioni 19.98 kwa mwaka sawa na asilimia 74.3. Kati ya kiasi hicho, makusanyo ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 12.61; makusanyo yasiyo ya kodi ni shilingi trilioni 1.79; na makusanyo ya Halmashauri ni shilingi bilioni 437.6. Kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji  kumetokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
(i)         Ukwepaji wa kodi;
(ii)       Ugumu wa kutoza kodi wafanya biashara walioko katika sekta isiyo rasmi kwa vile hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu;
(iii)     Mazingira yasiyo rafiki ya ulipaji kodi na mlolongo wa kodi na tozo, hasa  huduma zinazotolewa na mamlaka za udhibiti na usimamizi (zikiwemo TBS, TFDA, EWURA, TCRA, OSHA, Zimamoto), viwango vikubwa vya kodi; urasimu katika taratibu za kulipa kodi, na ugumu na gharama kubwa za kulipa kodi;
(iv)     Matumizi hafifu ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD);
(v)       Udhaifu katika usimamizi wa uvunaji wa rasilimali za nchi hasa madini, gesi asilia, misitu, rasilimali bahari, utalii na ardhi; na
(vi)     Mchango mdogo na utegemezi wa mashirika ya umma katika bajeti ya Serikali.

B.                Mikopo ya Ndani na Nje yenye Masharti ya Kibiashara
18.    Mheshimiwa Spika, Serikali ilikopa jumla ya shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 80 ya shilingi trilioni 6.17 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka 2017/18. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 4.13 zilikopwa kwa ajili ya kulipia dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva (rollover), na shilingi bilioni 832.3 zilikopwa ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, Serikali ilikopa kutoka soko la nje shilingi bilioni 224 sawa na asilimia 14 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 1.6. Fedha hizi zimeelekezwa kwenye utekelekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. Aidha, mwezi Mei, 2018, Serikali ilipokea mkopo wa kibiashara kiasi cha shilingi trilioni 1.13.

C.                Misaada na Mikopo Nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
19.    Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 1.87 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya mwaka ya shilingi trilioni 3.97. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 70.2 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti sawa na asilimia 7.5 ya makadirio ya shilingi bilioni 941.3, shilingi bilioni 182.9 ni misaada na mikopo nafuu ya Mifuko ya Kisekta sawa na asilimia 33 ya makadirio ya shilingi bilioni 556.1, na shilingi trilioni 1.61 ni misaada na mikopo nafuu ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 65 ya makadirio ya shilingi trilioni 2.47.

Mwenendo wa Matumizi
20.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili 2018, Serikali imetoa jumla shilingi trilioni 21.68 sawa na asilimia 68.4 ya lengo la mwaka la shilingi trilioni 31.71. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 16.56 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.63 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma na shilingi trilioni 8.42 kwa ajili ya kugharamia Deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.

21.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2018 Serikali imetoa jumla   ya shilingi trilioni 5.12 kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.35 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 775.8 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki hakijumuishi fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ambazo hazikupita kwenye mfumo wa malipo wa Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu ya kiuhasibu zitakapokamilika.

22.    Mheshimiwa Spika, naomba nieleze mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 katika kipindi cha Julai 2017 hadi Aprili 2018 kama ifuatavyo:
(i)         Jumla ya shilingi bilioni 59.0 zimetolewa katika Halmashauri za Wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, na shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za mikoa 24. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 125.7 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi;
(ii)       Kiasi cha shilingi bilioni 156.1 kimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini;
(iii)     Kiasi cha shilingi bilioni 409.9 kimetolewa kwa ajili ya miradi ya nishati vijijini, umeme wa jotoardhi, uzalishaji wa umeme katika vyanzo mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia;
(iv)     Katika kutekeleza azma ya kutoa elimumsingi bila ada na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali imetoa shilingi bilioni 618.0;
(v)       Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ili kupanua fursa za uchumi, kilimo, biashara na viwanda ikiwemo barabara zinazounganisha mikoa na nchi jirani, barabara zinazopunguza msongamano katika majiji, barabara za vijijini, reli, viwanja vya ndege, na bandari. Katika eneo hili kiasi cha shilingi trilioni 1.87 kimetolewa; na
(vi)     Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi umma, wazabuni, wakandarasi na watoa huduma ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.17 kimelipwa.

23.    Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kuchukua hatua nyingine zenye lengo la kuimarisha usimamizi wa bajeti ya Serikali kama ifuatavyo:

a) Deni la Serikali
24.    Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Deni la Serikali linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu, Serikali inaendelea kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Aidha, Serikali inatekeleza Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni unaotoa dira ya namna bora ya ukopaji ili kuepuka gharama na athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika kusimamia deni la Serikali. Katika kudhibiti kuongezeka kwa gharama za mikopo, Serikali ilijikita zaidi kukopa kwenye mikopo yenye masharti ya kati (Semi Concessional Loans) hasa mikopo inayowezesha uagizaji wa vifaa na mitambo kutoka nchi inayokopesha (Export Credit Agency - ECA) na pale ilipolazimu, mikopo ya masharti ya kibiashara ilikopwa kwa uangalifu mkubwa ikiwemo kuhakikisha kwamba mikopo hiyo inatumika kwenye maeneo ambayo yanachochea ukuaji wa uchumi.

25.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2018, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 49.65 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na shilingi trilioni 43.79 Aprili 2017.  Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 14.05 na deni la nje shilingi trilioni 35.60 sawa na asilimia 71.71 ya deni lote.  Ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo ya zamani na inayoendelea kupokelewa yenye masharti nafuu au kibiashara na malimbikizo ya riba ya Deni la Nje  hasa kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo Serikali bado inajadiliana nazo kuhusu msamaha wa madeni  kulingana na makubaliano na kundi hilo.

26.    Mheshimiwa Spika, Mikopo nafuu kutoka Mashirika ya Fedha ya Kimataifa imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha mikopo kutoka nje ambayo imechangia asilimia 59.6 ya deni lote la nje. Mikopo yenye masharti ya kibiashara imechangia asilimia 28.5, wakati mikopo kutoka nchi wahisani imechangia asilimia 11.9. Mikopo hii imetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

27.    Mheshimiwa Spika, Deni la Serikali limekuwa likiongezeka. Hata hivyo deni hilo limeendelea kuwa himilivu na ukuaji wake unawiana na kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2017 inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Uwiano wa deni kwa thamani ya sasa (present value) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani ya deni la nje kwa mauzo ya nje ilikuwa asilimia 81.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani asilimia 117.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250; ulipaji wa deni la nje kwa mapato yatokanayo na mauzo nje asilimia 9.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ulifikia asilimia 13.3  ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Napenda kusisitiza tena kwamba hakuna dhambi kwa nchi kukopa kwa busara (prudently). Mambo ya muhimu ya kujiridhisha nayo ni kuwa mikopo hiyo inatumika kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali (productive capacity) na kurejesha mikopo hiyo kwa kuzingatia uwezo wa uchumi kuhimili mzigo wa madeni (debt sustainability).

b) Kudhibiti Malimbikizo ya Madai ya Serikali
28.    Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kupunguza malimbikizo ya madai ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kila mwaka kwenye bajeti kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa; kuhimiza uzingatiaji wa sheria na kanuni zake kama vile, Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015; Sheria ya Ununuzi wa Umma SURA 410; Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na kanuni zake na kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali yakiwemo Waraka Na. 1 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali unaotolewa kila mwaka kuhusu utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Mpango na Bajeti unaotolewa kila mwaka.
 
29.    Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto hiyo ya malimbikizo ya madai, Serikali imeandaa Mkakati wa Kulipa Madeni na Kuzuia ulimbikizaji wa Madeni. Madai yanayohusika kwenye Mkakati huo ni yale yaliyozalishwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea (MDAs) na Sekretarieti za Mikoa (RSs) yakiwemo madeni ya Watumishi, Wazabuni na Watoa Huduma, pamoja na madai ya Wakandarasi. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa kwa kuzingatia mpango (roadmap) ulioandaliwa kulipa madeni hayo hadi yatakapofikia kiwango himilivu. Katika ulipaji wa madeni, kipaumbele kitatolewa kwa madeni yanayogusa watoa huduma wengi na yale ambayo yanaongezeka kutokana na riba.
30.    Mheshimiwa Spika, Mkakati huo unamtaka kila Afisa Masuuli kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kudhibiti malimbikizo ya madai na kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati. Hivyo, katika kuhakikisha kwamba hakuna madeni mapya yanayozalishwa, kila Afisa Masuuli atapaswa kuzingatia yafuatayo:
(i)         Mikataba yote ya ujenzi wa miundombinu inazingatia viwango vya bajeti vilivyowekwa katika kila Fungu. Aidha, Fungu husika lisiingie mikataba nje ya viwango hivyo bila kibali cha Mlipaji Mkuu wa Serikali; vile vile Kifungu cha 51(1) na (2) cha Sheria ya Bajeti ya 2015 kinaelekeza kwamba miadi yote ya miaka zaidi ya mmoja (Multi-year Commitments) lazima ipate idhini ya Waziri wa Fedha ikiwa imezingatia viwango vya bajeti, malipo ya miadi hii isizidi viwango/bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kulipa madai baada ya uhakiki;
(ii)       Kutoa kipaumbele kwa ukamilishaji wa miradi inayoendelea kabla ya kuanzisha miradi mipya, sambamba na kuhakikisha kwamba miradi inayoanzishwa inatengewa fedha katika bajeti;
(iii)     Maafisa Masuuli kutoingia makubaliano ya kupatiwa huduma au bidhaa bila ya kuwa na fedha au kibali cha maandishi kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali; na miadi yoyote ni lazima iingizwe kwenye mtandao wa IFMS;
(iv)     Madai ya watoa huduma wote na Wakandarasi lazima yafanyike baada ya kupata hati za ununuzi (LPO) kutoka kwenye mfumo wa IFMS iliyozingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kuwepo kwa ridhaa ya matumizi (Exchequer Issue Notification) kwa vifungu husika vya matumizi. Hivyo, Serikali inasisitiza kwamba, LPO zilizotoka kwenye mfumo wa Malipo ya Serikali (IFMIS) ndiyo zitumike kama msingi wa malipo kwa Watoa Huduma; na
(v)       Kuzingatia matumizi ya Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na  Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na waraka wa Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu utekelezaji wa bajeti.




III.      SERA ZA BAJETI  KWA MWAKA 2018/19
Shabaha za Uchumi Jumla na Bajeti
31.    Mheshimiwa Spika, Shabaha za uchumi jumla na bajeti katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
(i)         Pato la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2018 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.1 mwaka 2017;
(ii)       Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja;
(iii)     Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 15.6 mwaka 2016/17;
(iv)     Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.6 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 13.0 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 13.3 mwaka 2016/17;
(v)       Matumizi ya Serikali kufikia asilimia 24.5 ya Pato la Taifa  mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 23.0 mwaka 2017/18  na matumizi halisi ya asilimia 22.2 mwaka 2016/17; na
(vi)     Nakisi ya bajeti kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 2.1 mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 1.5 mwaka 2016/17.

Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
32.    Mheshimiwa Spika, ili kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, sera za mapato kwa mwaka 2018/19 zitalenga katika kuongeza wigo wa kodi, kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo hususan katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki na hatua nyingine za kiutawala.

33.    Mheshimiwa Spika, katika kuongeza wigo wa kodi, yapo maeneo makuu mawili yatakayozingatiwa na Serikali ambayo ni kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kupata vyanzo vipya vya mapato vitokanavyo na uwekezaji huo. Zipo hatua za urasimishaji zilizoanza kufanyika mfano uthaminishaji wa majengo, na upimaji wa viwanja, zoezi ambalo linaendelea nchi nzima. Serikali itaongeza kasi ya urasimishaji ikiwa ni pamoja na kuwepo na mbinu bunifu, rafiki, shirikishi na za kimkakati.

34.    Mheshimiwa Spika, mazingira bora ndio msingi mkuu wa kuvutia biashara na uwekezaji ikiwemo kuboresha miundombinu msingi, vivutio vya kikodi, sera zisizobadilika (policy consistency and predictability), upatikanaji wa ardhi na taratibu za kisheria na usimamizi. Pale mazingira yanapokuwa mazuri, uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya kibiashara inaongezeka na hivyo kupelekea kuongezeka kwa vyanzo vipya vya mapato.

35.    Mheshimiwa Spika, uchambuzi uliofanywa na Serikali mwaka 2017/18 ulibaini changamoto zifuatazo kuhusiana na mazingira ya biashara na uwekezaji :
(i)         Migongano ya sheria, kanuni na taratibu zinazotumiwa na mamlaka mbalimbali;
(ii)       Gharama kubwa za kuanzisha  na kuendesha biashara kutokana na wingi wa kodi, ada na tozo zinazoambatana na taratibu ngumu na nyingi zenye urasimu  usio na tija  na hivyo kutoa mianya na mazingira ya rushwa; na
(iii)     Muingiliano wa majukumu na wingi wa mamlaka za udhibiti katika kuidhinisha na kutoa hati, vibali na vyeti kwenye shughuli za uwekezaji na biashara.

36.    Mheshimiwa Spika, kutokana na uchambuzi huo, Serikali imeandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment for Tanzania). Miongoni mwa mapendekezo ya Mpango huo ambayo yatatekelezwa kwa nguvu zaidi kuanzia mwaka ujao wa fedha  (2018/19) ni kurahisisha taratibu za kulipa kodi, tozo na ada mbalimbali, na kupunguza muda na mlolongo mrefu wa kusajili makampuni na biashara. Serikali ya Awamu ya Tano inaamini kuwa maendeleo endelevu yatapatikana kwa haraka zaidi katika mazingira yenye ushirikiano wa kweli na wa dhati kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

37.    Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo, Serikali itaendelea na zoezi la uunganishaji wa Wizara, Idara, Wakala, taasisi na mashirika ya umma kwenye Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato (Government electronic Payment Gateway -GePG) ili kuboresha ukusanyaji na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali. Mfumo huu ulianzishwa mwaka 2017 na kupitishwa na Bunge kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 ambayo iliziagiza taasisi zote za Serikali kukusanya mapato kwa kutumia Mfumo wa GePG. Hadi mwezi Mei, 2018, jumla ya taasisi 234 zinazokusanya maduhuli zikijumuisha Halmashauri zote 185 zimeunganishwa kwenye Mfumo huu. Nachukua fursa hii kuagiza Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali zilizobaki zihakikishe kwamba zimeunganishwa na kuanza kutumia mfumo wa GePG kabla ya Juni, 2019. Mbali na Mfumo huu, ninawakumbusha Maafisa Masuuli wote kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa maduhuli unafanyika kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) pamoja na benki na siyo risiti za kuandikwa kwa mkono.

38.    Mheshimiwa Spika, kuhusu hatua nyingine za kiutawala za kuongeza mapato ya Serikali, ninaelekeza yafuatayo:
(i)         Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ichukue hatua za makusudi za kuboresha mahusiano kati yake na walipa kodi kwa lengo la kuondoa dhana  iliojengeka miongoni mwa walipa kodi kuwa TRA inatumia nguvu na vitisho kudai kodi;
(ii)       Ofisi ya Msajili wa Hazina iimarishe  usimamizi na ukaguzi  kwenye kampuni ambazo Serikali ina hisa ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata gawio stahiki katika uwekezaji wake; na
(iii)     Mamlaka za Serikali za Mitaa zijielekeze kwenye miradi itakayochochea upatikanaji wa mapato katika mamlaka hizo hususan viwanda, masoko na machinjio ya kisasa, stendi za mabasi, stendi za maegesho ya malori kwenye mipaka na nchi jirani na maghala ya kuhifadhi nafaka.

Kuimarisha Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo
39.    Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu imekuwa ikipungua kutoka wastani wa asilimia 26.3 ya bajeti halisi ya mwaka 2010/11 hadi asilimia 10.4 mwaka 2016/17. Kutokana na umuhimu wa kuwa na maendeleo endelevu na kuhakikisha kuwa misaada na mikopo nafuu inapatikana  kama ilivyoahidiwa na kwa wakati, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendelo na wadau wengine imekamilisha Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework - DCF). Mwongozo huo uliidhinishwa na Serikali mwezi Agosti 2017 na umebainisha:
(i)         Misingi ya jumla ya kuongoza ushirikiano ambayo ni pamoja na Serikali kuongoza michakato ya kuibua vipaumbele vya miradi ya maendeleo; na
(ii)       Mfumo wa majadiliano ambao uko katika ngazi tatu; Majadiliano ya Kitaifa ya Kimkakati, Majadiliano ya Kisekta na Majadiliano yenye Mwelekeo wa Kisiasa.


Sera za Matumizi
40.    Mheshimiwa Spika, sera za matumizi katika mwaka 2018/19 zitajumuisha:
(i)         Kudhibiti nakisi ya bajeti isizidi asilimia 3.2 ya Pato la Taifa;
(ii)       Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele na yenye tija ili kuchochea ukuaji wa kilimo na viwanda, kupanua fursa za ajira, kujenga na kuboresha miundombnu ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za jamii;
(iii)     Kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima; na
(iv)     Kudhibiti ulimbikizaji wa madai.

41.    Mheshimiwa Spika, Katika kusimamia sera hizi, Serikali itachukua hatua zifuatazo:
(i)         Kuwachukulia hatua za kisheria, kinidhamu na kiutawala wote watakaothibitika kwenda kinyume na sheria na kanuni zinazoongoza utendaji katika nafasi zao. Napenda niwakumbushe tena kuwa kula fedha za miradi ya wananchi ni sawa na kula sumu – wasijaribu!!
(ii)       Kuhakikisha kuwa Maafisa Masuuli hawaingii mikataba bila kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha au ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali na kuzuia matumizi na ahadi (commitments) za matumizi nje ya mfumo wa “IFMS”. Lengo ni kudhibiti ulimbikizaji wa madai;
(iii)     Kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi;
(iv)     Kulipa madai mbalimbali yaliyohakikiwa;
(v)       Kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unawiana na thamani ya fedha itakayotumika; na
(vi)     Kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

 Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2018/19
42.    Mheshimiwa Spika, kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 ambao niliuwasilisha leo asubuhi, bajeti ya matumizi katika mwaka 2018/19 itaweka mkazo zaidi katika uendelezaji wa miradi ya kielelezo; kufungamanisha maendeleo ya watu; na ujenzi wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji biashara.
43.    Mheshimiwa Spika, maeneo ya kipaumbele katika bajeti hii ni yafuatayo:
(i)         Kilimo: Fedha zitaelekezwa zaidi kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, maghala na masoko, kuimarisha upatikanaji wa  pembejeo na zana za kilimo, kupanua huduma za ugani, kuboresha mfumo wa utafiti na utoaji wa matokeo ya utafiti kwa wananchi, na uendelezaji wa sekta ndogo za uvuvi na mifugo. Mkazo umewekwa katika sekta hii kwa kuzingatia kuwa inategemewa na wananchi wengi na ndiyo itakayotupatia malighafi kwa ajili ya viwanda, kutuhakikishia usalama wa chakula na kuongezeka kwa kipato cha wananchi;
(ii)       Viwanda: Katika kuchochea ukuaji wa viwanda nchini, Serikali itaelekeza nguvu zake kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi hususan viwanda vya nguo, ngozi na nyama, samaki, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo, na katika sekta ya madini. Aidha, uendelezaji wa viwanda na kilimo utapaswa kuzingatia uendelevu wa mazingira;
(iii)     Huduma za Jamii: Maji: Eneo lingine muhimu ni kuongeza upatikanaji na usambazaji wa maji safi hasa vijijini na uondoshaji wa majitaka, uchimbaji wa visima katika maeneo kame nchini na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati.  Elimu: Serikali itaendelea kugharamia elimu msingi bila ada, kuongeza idadi ya wataalam katika fani adimu kwenye maeneo ya madini, mafuta na gesi, madaktari bingwa (moyo na figo) pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Afya: rasilimali fedha zitaelekezwa kuongeza usambazaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za rufaa. Vile vile katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaelekeza fedha zaidi za LGCD kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hususan miradi ya elimu na afya. Aidha, Serikali itaweka msukumo kuimarisha upatikanaji wa lishe bora kwa mama na mtoto hususan katika siku 1,000 za mtoto tangu kutungwa kwa mimba ili kuondokana na changamoto ya kuwa na watoto wenye udumavu na hivyo kukua vema kimwili na kiakili. Aidha, mahitaji ya makundi maalum katika jamii yetu (wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu na wazee) yataendelea kuangaliwa kipekee;
(iv)     Kujenga na kukarabati miundombinu wezeshi hususan kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, kuendelea na ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na zile za vijijini, na kuimarisha usafiri wa anga na majini; na
(v)       Maeneo mengine ya kipaumbele ni: kurahisisha umiliki wa ardhi,  kuimarisha huduma za mawasiliano,  kifedha na utalii na kuimarisha ulinzi, usalama, utawala bora, na utoaji haki.


IV.      HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI

Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo Mbalimbali

44.    Mheshimiwa Spika, napenda kuwasilisha mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya Viwanda, Utalii, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wenye kutabirika. Marekebisho hayo yanahusu Sheria zifuatazo:-

a.   Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.   Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c.   Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.   Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290;
e.   Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
f.     Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348; na Sheria ya Benki Kuu, SURA 197;
g.   Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
h.  Sheria zinazosimamia Bodi za Mazao;
i.     Sheria ya Michezo ya Kubahatisha SURA 41;
j.     Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
k.   Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.


a)       Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
45.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani,Sura 148 kama ifuatavyo:-

(i)         Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifungashio vya madawa ya binadamu vitakavyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha dawa hapa nchini. Aidha, vifungashio hivyo vitakuwa na machapisho ya majina ya kiwanda husika cha utengenezaji madawa ili kuhakikisha kwamba vinatumiwa na viwanda hivyo na siyo vinginevyo. Lengo la hatua hii nikupunguza gharama za uzalishaji na kuvilinda viwanda vinavyotengeneza madawa hapa nchini ili viweze kumudu ushindani na kuongeza uzalishaji;
(ii)       Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye virutubisho vinavyotumika kutengenezea vyakula vya mifugo (animal and poultry feeds additives) vinavyoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa wafugaji na kuhamasisha ufugaji bora ili kuongeza mchango wa Sekta hiyo katika Uchumi;
(iii)     Kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na maswala ya fedha  kutoa msamaha wa kodi kwa miradi ya Serikali inayotekelezwa kwa mikopo ya kibiashara. Hivi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani inakataza kusamehe kodi kwenye mikopo ya kibiashara hali ambayo imesababisha kukwama kwa utekelezaji wa miradi muhimu ya Serikali kama vile miradi ya Maji, barabara n.k. Hivyo, marekebisho yanayopendekezwa yatawezesha utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati uliopangwa;
(iv)     Kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kusamehe kodi hiyo pale ambapo kuna mkataba uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Fedha au Benki ambayo ni “mwakilishi” wa Serikali nyingine aliyepewa dhamana na Serikali hiyo kuingia mikataba na kusimamia utekelezaji wa miradi husika. Hivi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani inampa mamlaka Waziri huyo kusamehe kodi pale ambapo kuna mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya nchi nyingine unaotoa msamaha wa kodi. Hivyo miradi mingi inayohusisha mikataba ya misaada au mikopo kupitia mabenki na Taasisi za fedha imekwama utekelezaji wake. Kwa msingi huo, marekebisho haya yanalenga katika kuondoa ukwamishaji na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi mingi ya Serikali inayotekelezwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo kupitia mikataba inayosainiwa na Serikali yetu na Benki au Taasisi za Fedha za Serikali za nchi nyingine; na
(v)       Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za kike (sanitary pads) HS Code 9619.00.10. Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hii muhimu kwa bei nafuu kwa ajili ya kulinda afya ya mama na mtoto wa kike hasa watoto walio shuleni na vijijini. Ni matarajio ya Serikali kuwa wazalishaji na wauzaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi hii.

Hatua hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 219.1

b)       Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
46.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya   Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-

(i)         Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19 hadi mwaka 2022/23 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za  ngozi. Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (performance agreement) na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuongeza uwekezaji katika sekta ya madawa ya binadamu na usindikaji wa ngozi ambao kwa sasa haufanyiki nchini na pia kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Aidha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza dawa hizo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wa madawa mengi zaidi hapa nchini;
(ii)       Kufuta kifungu cha 10A cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinachomkataza Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha kutoa msamaha wa kodi kwenye miradi ya Serikali inayotekelezwa kwa fedha za mikopo ya kibiashara (non concessional loans). Lengo la hatua hii ni kumpa mamlaka Waziri huyo kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa miradi hiyo ambayo imekuwa na changamoto katika utekelezaji wakati Serikali inapopata mikopo ya aina hiyo; na
(iii)     Kurekebisha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kutoa msamaha wa Kodi ya zuio inayotozwa kwenye riba kwa mikopo inayotolewa kwa Serikali na Benki, Taasisi za Fedha na wahisani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 220.5.

c)       Sheria ya Ushuru wa Bidhaa,  SURA 147
47.    Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa (specific duty rates) zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, ili kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda, napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli zinazozalishwa hapa nchini na kuongeza viwango vya Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo:- 

(i)         Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 61 kwa lita;
(ii)       Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 61 kwa lita hadi shilingi 64.05 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji yanayozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha  sasa cha shilingi 58 kwa lita;
(iii)     Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini (local juices) hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 9 kwa lita;
(iv)     Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini (imported juices) utaongezeka kutoka shilingi 221 kwa lita hadi shilingi 232 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
(v)       Ushuru wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted Cereals) hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 450 kwa lita;
(vi)     Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka shilingi 765 kwa lita hadi shilingi 803.25 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 38.25 kwa lita;
(vii)   Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka shilingi 561 kwa lita hadi shilingi 589.05 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 28.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha shilingi 561 kwa lita;
(viii)Kuanzisha Ushuru wa Bidhaa wa shilingi 200 kwa lita kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na usindikaji wa matunda (kama ndizi, rozela/choya, nyanya, nk) yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75;
(ix)     Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 200 kwa lita;
(x)       Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka shilingi 2,349 kwa lita hadi shilingi 2,466 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 117 kwa lita;
(xi)     Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 3,481 kwa lita hadi shilingi 3,655.05 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 174.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 3,315 kwa lita;
(xii)   Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja;
(xiii)Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja;
(xiv) Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (xii) na (xiii) utaongezeka kutoka shilingi 53,235 hadi shilingi 55,896.75 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,661.75 kwa kila sigara elfu moja;
(xv)   Ushuru wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) inayoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 26,888 hadi shilingi 28,232.4 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,344.4 kwa kilo; na
(xvi) Ushuru wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.

48.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kuanzisha Mfumo Mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki utakaoanza kutumika tarehe 1 Septemba 2018. Mfumo mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki utaiwezesha Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani na kwa wakati (real time) zinazotumika kupanga mipango ya maendeleo ya Taifa. Pia mfumo huu mpya utaiwezesha Serikali kudhibiti uvujaji wa mapato na kutambua mapema kiasi cha Kodi ya Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Mapato na ile ya Ongezeko la Thamani itakayolipwa. Aidha, mfumo wa Stempu za Kodi za kielektroniki utadhibiti tatizo la uwepo wa stempu za karatasi za kugushi ambalo linachangia uwepo wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza kuathiri afya za binadamu. Mfumo huu mpya unatumika katika nchi nyingine ikiwa pamoja na Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Switzerland na umekuwa na mafanikio makubwa.

Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 119,456.6

d)       Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290.
49.    Mheshimiwa Spika napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kama ifutavyo:-

(i)         Kuongeza kifungu cha 37A kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa ili kumpa Mamlaka Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa Kuzitaka Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya fedha wanazokusanya kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya vijana na wanawake. Aidha asilimia 50 ya fedha hizo zitatengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana na asilimia 50 kwa vikundi vya wanawake. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI ataandaa Kanuni ambazo zitaweka utaratibu wa kusimamia utoaji wa fedha hizo kwa vikundi vya vijana na wanawake vilivyosajiliwa. Pia, fedha zitatolewa kwa kuwakopesha bila kutoza riba yoyote; na
(ii)       Kurekebisha kifungu cha 16(6) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ambacho kinatoa mwanya kwa Taasisi/Makampuni yanayolipa Ushuru wa Huduma kutolipa Ushuru wa Mazao. Mfano, Makampuni mengi yanayochakata zao la mkonge ili kuzalisha nyuzi za katani yanamiliki pia mashamba ya mkonge. Hivyo siyo busara kuwalipisha ushuru wa mazao na ushuru wa huduma. Hata hivyo, yapo makampuni yenye mashamba ya mkonge ambayo hayachakati mkonge, haya yanapaswa kulipa ushuru wa mazao badala ya ushuru wa huduma. Napendekeza kiongezwe kifungu cha 16(7) kwenye Sheria hiyo kuyataka Makampuni yanayozalisha mazao na hayachakati kwa ajili ya kuyaongezea thamani yawajibike kulipa Ushuru wa Mazao.

e)       Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438
50.    Mheshimiwa Spika, napendekeza Kurekebisha Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438, ili kuanzisha utaratibu maalum wa kusamehe kodi (Tax Amnesty) ambao unalenga kusamehe malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu (Interest and Penalties) kwa kiwango cha asilimia 100. Msamaha huo utatolewa kwa kipindi cha miezi sita (6) kinachoanzia tarehe 1 Julai 2018 mpaka tarehe 31 Desemba 2018. Aidha kwa kufanya hivyo, Serikali inatarajia kukusanya malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi (Principal Tax) pamoja na kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiyari kwa zaidi ya asilimia 10.

Hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 500,000.





f)         Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290, Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348 na Sheria ya Benki Kuu, SURA 197.

51.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kurekebisha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, Sheria ya Fedha za Umma Sura 348, na Sheria ya Benki Kuu, Sura 197 ili kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account) ambapo akaunti hii itatumika kupokea fedha zote za Serikali na kufanya malipo yote ya Serikali. Msingi wa kuanzishwa kwa akaunti hii ni kutekeleza makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyozitaka nchi wanachama kuanzisha akaunti jumuifu ili kuimarisha usimamizi wa fedha za Serikali. Uwepo wa akaunti hii pamoja na mambo mengine utarahisisha usimamizi wa fedha za Serikali kwa kupunguza idadi ya akaunti kwenye benki za biashara na Benki Kuu, kupunguza gharama za kibenki zinazolipwa hivi sasa na Serikali kufuatia huduma zinazotolewa kwa Serikali na Benki za Biashara, kupunguza nakisi kwenye mfuko Mkuu wa Serikali ambapo akaunti maalum zitajumuishwa kwenye ukokotoaji wa bakaa katika Mfuko Mkuu wa Serikali tofauti na utaratibu wa hivi sasa ambapo akaunti hizi hazijumuishwi katika ukokotoaji huo.

g)       Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya  mwaka 2004

52.    Mheshimiwa Spika, kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 4 Mei, 2018 mjini Arusha, Tanzania kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa Mwaka 2018/19. Mapendekezo hayo yanalenga kwa kiwango kikubwa katika kuchochea maendeleo ya viwanda ili kukuza ajira na ustawi wa jamii (Industrialization for Job Creation and Shared Prosperity).


53.    Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:-

(i)         Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano (HS Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuendelea kutoa unafuu kwa viwanda vya wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei kwa bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia ngano hiyo. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bado kiwango cha uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu ni kidogo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo hautoshelezi mahitaji. Ili kudhibiti uagizaji wa bidhaa hii, utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo viwanda vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji ndivyo vitakavyohusika na kutumia kiwango hicho cha msamaha wa Ushuru wa Forodha;
(ii)       Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwenye mashine za Kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Electronic Fiscal Devices) zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inatarajiwa kuendelea kutoa unafuu na kuhamasisha wafanyabiashara na walipa kodi kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na kuongeza ufanisi katika Usimamizi na Udhibiti wa kodi;
(iii)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 15  badala ya asilimia 25 kwenye karatasi zinazotambulika katika HS Codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.31.00; na 4804.41.00. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo wazalishaji wanaotumia karatasi hizo katika kutengeneza madaftari na vitabu ndio watakaofaidika. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa wazalishaji hao. Ni matarajio ya Serikali kwamba wazalishaji watauza bidhaa hizi kwa bei nafuu na hivyo kuwezesha watumiaji, hususan wanafunzi, kuzipata kwa gharama nafuu;
(iv)     Kutoza Ushuru wa forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazoingizwa kutoka nje kwa ajili ya utengenezaji wa gypsum board (Gypsum paper for manufacturing of gypsum board) zinazotambulika katika HS Code 4805.92.00;
(v)       Kutoza Ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 100 kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini. Hivi sasa sukari hiyo inatozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 100;
(vi)     Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye "Gypsum Powder" inayotambuliwa kwa HS Code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Marekebisho haya yanalenga katika kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini na kuhamasisha wawekezaji watumie "gypsum" inayopatikana hapa nchini kuzalisha "gypsum" powder. Aidha, hatua hii inatarajiwa kuongeza ajira na mapato ya Serikali;
(vii)   Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa ijulikanayo kama "Self-adhesive label" (HS Code 4821.10.90) ambayo hutumika kama alama ya kutambulisha aina ya bidhaa kwa watengenezaji wa dawa za meno. Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama ya uzalishaji kwenye viwanda vya dawa za meno kwa kuwa self-adhesive labels hazizalishwi hapa nchini;
(viii)Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates" (ABL) HS Code 3920.10.90 kwa mwaka mmoja. Aidha utaratibu wa “duty remission” utatumika ambapo hatua hii itawahusu wenye viwanda vinavyoagiza bidhaa hiyo kwa matumizi ya kiwandani. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama ya uzalishaji kwa viwanda vya dawa za meno. Aidha, ina lengo la kuvilinda viwanda hivi kutokana na ushindani na ajira;
(ix)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula ya mawese (Crude Palm Oil) yanayotambulika katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula hapa nchini kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo.    Aidha, lengo ni kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mafuta ghafi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa hapa nchini. Pia inatarajiwa kwamba uzalishaji wa mbegu utaongezeka na kuongeza ajira viwandani na mashambani pamoja na kuongeza kipato cha wakulima;
(x)       Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 au asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi, karanga, mahindi n.k). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uzalishaji wa mbegu na mafuta ya kula hapa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini. Aidha, inatarajiwa kwamba hatua hii italinda viwanda na ajira katika sekta ndogo ya mafuta ya kula, na kuongeza mapato ya serikali na wakulima;
(xi)     Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na cha mwisho (semi-refined, refined/double refined oil) mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi, karanga, mahindi n.k. Ongezeko hilo la Ushuru wa Forodha linatarajiwa kulinda uzalishaji wa mafuta ya kula na kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta zinazozalishwa nchini badala ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Aidha, hatua hii inatarajiwa kupunguza fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi;
(xii)   Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za misumari zinazotambulika katika HS Code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins, corrugated nails, staples other than those of heading 83.05). Hatua ya kuweka kiwango hicho cha Ushuru wa Forodha inalenga katika kulinda viwanda vya bidhaa hizo hapa nchini kutokana na uingizaji wa bidhaa kama hizo kutoka nje ya nchi;
(xiii)  Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety matches) vinavyotambuliwa kwenye HS Code 3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo wa kuzalisha viberiti na kutosheleza mahitaji katika soko hivyo kuwepo na umuhimu wa kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xiv) Nchi za Jumuiya zimekubaliana kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya kutengeneza bidhaa za rangi za kupaka nyumba ijulikanayo kama “polyvinyl Alcohol” (HS Code 3905.30.00). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hizo;
(xv)   Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwa utaratibu wa “duty remission” kwenye malighafi (inputs) zinazotumika katika kutengeneza dawa za kuua wadudu (pesticides, fungicides, insecticides na acaricides). Hatua hii itahusisha viwanda vinavyotumia malighafi hizo kutengeneza dawa za kuua wadudu. Aidha, viwanda vitakavyoagiza malighafi hizo vitatakiwa kupata kibali cha Wizara ya Kilimo. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda hivyo;
(xvi) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa utaratibu wa duty remission kwenye bidhaa ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama “RBD Palm Stearin” inayotambulika katika HS Code 1511.90.40. Hatua hii inahusisha viwanda vinavyotumia bidhaa hiyo katika kutengeneza sabuni. Aidha, hatua ya kupunguza ushuru huo imezingatia kwamba Serikali imeongeza ushuru wa forodha katika mafuta ghafi ya mawese;
(xvii)Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye viazi (potatoes fresh or chilled, other than seeds) vinavyotambulika katika HS Code 0701.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa viazi hapa nchini;
(xviii)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chingamu (Chewing Gum) zinazotambulilka katika HS Code 1704.10.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kwa kuwa kuna uwezo wa kuzalisha chewing gum katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xix) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye peremende HS Code 1704.90.00. Hatua hii inachukuliwa kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na ajira;
(xx)   Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chokoleti (chocolates) HS Code 18.06. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazalisha bidhaa hizi na zina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxi) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Biskuti (Biscuits) zinazotambullika kwa HS Code 1905. Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo wa kuzalisha bidhaa hiyo na kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxii)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauce) zinazotambulika katika HS Code 2103.20.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hiyo katika viwanda vya ndani na mashambani. Aidha, imezingatia kwamba nchi yetu inazalisha nyanya za kukidhi mahitaji na pia kuna umuhimu wa kusindika nyanya hizo hapa nchini ili kuongeza thamani na kuongeza ajira katika kilimo cha nyanya;
(xxiii)  Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS Code 2201.10.00. Hatua hii ni muhimu katika kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xxiv)  Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama (meat and edible meat offal in chapter 12) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya uchakataji wa nyama hapa nchini na hivyo kuongeza thamani yake. Aidha, itaongeza fursa za ajira na kipato katika sekta ya ufugaji na viwandani; na
(xxv) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo (HS Code 1601.00.00). Hatua hii ina lengo la kulinda na kuhamasisha Viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

54.    Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-

(i)         Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari yanayotumika kwenye mashindano ya mbio za magari (rally cars) na kuingiza pikipiki (motorcycles) ili nazo ziweze kupata msamaha huo. Aidha, magari na pikipiki husika hutengenezwa mahsusi kwa ajili ya mashindano hayo. Hatua hiyo inatarajiwa kuhamasisha mashindano hayo na kukuza sekta ya utalii;
(ii)       Kufanya marekebisho kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha kwa boti inayotumika mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa kwenye maji (Motor Boat Ambulance) inayotambulika katika HS Code 8903.99.10 kama vile yanavyosamehewa magari ya kutoa huduma kwa wagonjwa (Motor Vehicle Ambulance). Hatua hii ina lengo la kupunguza gharama na kuwezesha utoaji wa huduma za matibabu katika usafiri wa majini; na
(iii)     Kufanya Marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya kubebea watalii (Motor vehicle for Transport of Tourists). Magari haya yanajumuisha magari ya aina mbalimbali ambayo yametengenezwa mahsusi kwa ajili ya kubebea watalii (Motor sightseeing buses, overland trucks). Lengo la kutoa msamaha huo ni kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii, kuboresha huduma ya usafiri kwa watalii na kuongeza ajira na mapato ya Serikali.

55.    Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tumekubaliana kupunguza Viwango vya Ushuru wa Forodha (duty remission) kwenye malighafi na vipuri vinavyohitajika katika kutengeneza nguo na viatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, tayari nchi hizi zimewasilisha orodha ya malighafi na vifaa vitakavyopunguziwa Ushuru wa Forodha. Uamuzi huo utaanza kutekelezwa mwaka 2018/19.

Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,630.2

h)      Sheria zinazosimamia Bodi za Mazao.

56.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria zote zinazosimamia Bodi za mazao mbalimbali kwa lengo la kuwezesha ushuru wote unaokusanywa na bodi hizo kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na ushuru unaotozwa kwenye mazao mbalimbali yanasimamiwa ipasavyo na kutumika kwa ajili ya shughuli zilizokusudiwa. Aidha,  shughuli za kuendeleza mazao pamoja na gharama za uendeshaji wa Bodi zitagharamiwa kupitia Bajeti ya Serikali.



i)         Sheria ya Michezo ya kubahatisha, SURA 41

57.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko ya kiwango cha kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (sports betting) kutoka asilimia 6 ya mauzo ghafi hadi asilimia 10. Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali kutoka kwenye sekta ndogo ya michezo hiyo ya kubahatisha.

58.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine za michezo ya kubahatisha (slot machines) kutoka shilingi 32,000 hadi shilingi 100,000 kwa kila mashine kwa mwezi. Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.

59.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye michezo ya kubahatisha (Casino) kutoka asilimia 15 hadi asilimia 18 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross Gaming Revenue -GGR). Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu kiwango cha asilimia 15 kimedumu kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2012.

60.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine arubaini (Forty Machines Site) za michezo ya kubahatisha kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross Gaming Revenue -GGR). Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.

Hatua hizi za marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 21,198.8.

j)         Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na   Sheria nyingine mbalimbali.

61.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).


k)      Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.

62.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-

(i)         Kusamehe Kodi ya Ardhi kwa Taasisi za Serikali kwa sababu taasisi hizi ni za umma hazitengenezi faida. Aidha, marekebisho mengine ya ada na tozo mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi yalitangazwa na Waziri mwenye dhamana ya ardhi kwenye hotuba yake;
(ii)       Kufuta na kupunguza baadhi ya viwango vya tozo na ada zinazotozwa kwenye sekta ya uzalishaji wa Chumvi. Hatua hii imetokana na kuwepo kwa utitiri wa tozo na ada zinazotozwa kwenye Madini ya Chumvi hali ambayo inasababisha gharama za uzalishaji kuwa juu na kuwakatisha tamaa wazalishaji kuendelea na uzalishaji wa chumvi. Hivyo napendekeza kufanya marekebisho ya tozo na ada kwenye sekta ya uzalishaji chumvi kama ifuatavyo:-
a) Kufuta ushuru wa mazao ya chumvi unaotozwa na Halmashauri;
b) Kufuta ada ya ukaguzi wa madini ya chumvi (Inspection and Clearance fee) inayotozwa kwa kiwango cha asilimia moja (1%) ya thamani ya madini;
c)  Kufuta ushuru wa Mikoko (Mangrove Levy) unaotozwa kwenye maeneo ya uzalishaji wa chumvi kwa kiwango cha shillingi 100,000 kwa eka moja kwa mwaka;
d) Kufuta ada ya kupitia andiko la mradi kwenye sekta ya uzalishaji chumvi inayotozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira;
e)  Kufuta ada ya usajili wa Jangwa la Chumvi (Solar Salt Panel);
f)   Kufuta ada ya Usimamizi kwenye eneo la Chumvi (Supervision fee)  inayotozwa na Wakala wa Misitu Tanzania;
g)  Kufuta ada ya usajili wa mradi wa uzalishaji chumvi inayotozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira;
h) Kufuta ada ya Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Impact Assesment) inayotozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira kwenye sekta ya uzalishaji chumvi;
i)    Kupunguza ada ya gharama za ukaguzi wa usalama mahala pa kazi inayotozwa kwenye sekta ya uzalishaji chumvi kutoka shilingi millioni 2 hadi shilingi millioni 1 kwa mwaka; na
j)    Kupunguza ada ya kibali cha kusafirisha madini ya chumvi nje ya nchi kutoka Dola za Kimarekani 100 hadi shilingi 20,000 kwa mwaka.
(iii)     Napendekeza kufanya marekebisho ya ada na tozo zinazotozwa na Mamlaka ya Afya na Usalama (OSHA) mahali pa kazi kama ifuatavyo:-
a)         Kufuta ada inayotozwa kwenye fomu ya usajili sehemu za kazi;
b)         Kufuta tozo ya usajili sehemu za kazi;
c)          Kufuta faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto inayotozwa kwa kiwango cha shilingi 500,000;
d)         Kufuta Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya afya na usalama; na
e)          Kufuta tozo ya ushauri wa kitaalam ya usalama wa afya.

63.    Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi. Hii itajumuisha kupitia upya na kuvisawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada za usumbufu.

l)         Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
64.    Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2018, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.




V.      SURA YA  BAJETI KWA MWAKA 2018/19
65.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera za bajeti kwa mwaka 2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 32.48 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 20.89, sawa na asilimia 64.3 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 18.0 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato yasiyo ya kodi yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 2.16 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 735.6.

66.    Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.68 ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti yote. Misaada na mikopo hii inajumuisha misaada na mikopo nafuu ya miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.0; mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 125.9; na misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS) shilingi bilioni 545.8.

67.    Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 8.90 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Mikopo ya ndani inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.79, ambapo shilingi trilioni 4.6 ni kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na shilingi trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 3.11 kutoka soko la nje.

68.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20.47 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi trilioni 7.41 za mishahara na shilingi trilioni 10.00 kwa ajili ya kulipia deni la Serikali, michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na huduma nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi trilioni 12.01 sawa na asilimia 37 ya bajeti yote, ambapo shilingi trilioni 9.88 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.13 ni fedha za nje. Kiwango hiki cha bajeti ya maendeleo kimezingatia matakwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 wa kutenga bajeti ya maendeleo kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote.

69.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2018/19
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango


VI.      HITIMISHO
70.    Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, dhima ya bajeti ya mwaka 2018/19 ni kuendelea “kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Mageuzi haya ya uchumi wa viwanda yatajengwa kupitia ushiriki wetu katika shughuli za kiuchumi, ubia na kuunganisha juhudi zetu pamoja. Ili kufikia malengo tunayoyakusudia, maamuzi magumu ni lazima yafanyike katika kuelekeza rasilimali chache tulizonazo katika maeneo ya kimkakati. Mabadiliko yoyote ni vigumu kuyakubali na mara nyingi mabadiliko hupingwa. Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla tuunganishe nguvu zetu, vipaji vya wananchi wetu na biashara zetu ili kufikia malengo tunayoyakusudia. Hivyo, tunahitaji uzalendo na nidhamu ya kazi ya hali ya juu tukikusudia kuondoa umasikini, kuongeza ajira na kuwa na uchumi jumuishi.

71.    Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi kuongeza uzalishaji katika sekta za viwanda na kilimo na ukusanyaji wa mapato ya ndani yatakayowezesha ugharamiaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida na hivyo kupunguza utegemezi. Hatua hizo ni pamoja na: kuvutia uwekezaji; kuelekeza rasilimali kwenye maeneo machache yenye tija; kusimamia utekelezaji wa sheria za kodi; kurasimisha sekta isiyo rasmi ikiwemo usajili wa wamiliki wa ardhi na majengo katika mfumo wa walipa kodi; na kuhimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika miamala mbalimbali ikiwemo matumizi ya EFD na kadi za kielectroniki za benki (Debt/credit cards) katika maeneo yanayotoa huduma kama vile katika maduka makubwa, hoteli na vituo vya mafuta. Hivyo, napenda kuwahimiza Watanzania tuwajibike kulipa kodi na kuhakikisha tunatoa na kudai risiti  kulingana na muamala uliofanyika. Aidha, Serikali inawashukuru kwa dhati wananchi wote ambao wameonesha uzalendo kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari.

72.    Mheshimiwa Spika, kipaumbele kikuu cha Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi ili kupanua fursa za ajira, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii (maji, afya, elimu) na kupunguza umaskini. Aidha, Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti matumizi ya fedha za umma. Serikali pia itaongeza msukumo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Mpango huu, pamoja na mambo mengine unakusudia kuhuisha na kurahisisha taratibu za kulipa kodi, tozo na ada mbalimbali.

73.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano inalenga kujenga utamaduni  na nidhamu ya kukubali maoteo halisia ya ukusanyaji wa mapato ambayo yanapaswa kuwa  ukomo wa  matumizi (expenditure ceiling) badala ya utarabu uliozoeleka wa kuanza kupanga au kuorodhesha mahitaji kwanza. Hivyo, Serikali itajielekeza katika utekelezaji wa miradi michache ya kimkakati kwa namna ambayo itashirikisha sekta zote zinazotegemeana na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kabla ya kuanza miradi mipya.

74.    Mheshimiwa Spika, mimi ni mpenzi sana wa kujisomea kuhusu maisha na sifa za viongozi mashuhuri, viongozi bora na wa kipekee wa nchi mbalimbali waliofanikiwa kuongoza mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika nchi zao kama vile Deng Tsiaoping –Jamhuri ya Watu wa China; Dkt. Mahithir Mohamed – Malaysia; Lee Kuan Yew – Singapore; Park Chung Hee – Korea, Nelson Mandela –Afrika ya Kusini, Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, Quett Masire – Botswana nk. Nilichojifunza na nilieleza katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali  mwaka jana kuwa viongozi wa aina hiyo wana sifa muhimu zifuatazo:
(i)         Dira au maono dhahiri kuhusu maendeleo ya nchi zao;
(ii)       Hawasiti kutekeleza dira hizo kwa dhamira kubwa tena bila kusita au kubadili msimamo;
(iii)     Ni jasiri, shupavu na wenye kuthubutu kutekeleza jambo wanaloliamini bila kigugumizi;
(iv)     Wana kipaji cha kujali maumivu ya wanyonge;
(v)       Ni waadilifu, wanachukia rushwa na ufisadi na ni wenye nidhamu ya kazi ya hali ya juu;
(vi)     Wanaongoza kwa vitendo; na
(vii)   Huvumilia magumu ili kuiletea nchi mabadiliko chanya.

75.    Mheshimiwa Spika, ninapenda niwaambie tena Watanzania kwamba Mwenyezi Mungu ametutunukia kiongozi Mkuu wa nchi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye sifa hizo zote nilizotaja. Nilieleza  mwanzoni mambo machache ambayo amethubutu kutenda kwa kipindi kifupi kuthibitisha sifa hizo. Rai yangu kwa Watanzania wenzangu ni kuwa tutumie fursa hii adimu kwa kufanya kazi kama njia bora ya kumuunga mkono Rais wetu katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya, Tanzania ya Viwanda. Jambo hili ni muhimu kwa sababu kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alivyotabiri, katika safari ya maendeleo – ya kuelekea kujenga uchumi wa viwanda – kiongozi wetu atakumbana na vikwazo na kelele nyingi za kuzomea kutoka kwa wale wasiotutakia mema ili kutukatisha tamaa tusifikie malengo. Hivyo, Watanzania wote tunao wajibu wa kumtia nguvu Rais wetu ili asirudi nyuma katika safari aliyoianza na aweze kutuvusha kuifikia Tanzania ya viwanda. Niruhusu nimalizie rai yangu kwa nukuu ya mazungumzo ya Mwalimu Nyerere kwa “TANU study Group” tarehe 13 Juni, 1967:

Maendeleo na kazi ni kitu kile kile, hakuna namna nyingine sisi ya kuendelea, hatukupewa namna nyingine sisi ya kuendelea….. Huwezi kutenganisha vitu viwili hivi, kuendelea na kazi, kwani kazi ndiyo shughuli ya …..  kuondoa matatizo yanayomzuia binadamu hali yake kukamilika…. Hakuna njia nyingine lazima kufanya kazi…… na kila unavyozidi kufanya kazi kwa akili zaidi ndivyo mnavyozidi kwenda, ndivyo mnavyozidi kuendelea,….. Kazi ndio utu …kazi ndio maendeleo…kazi ndio maisha, ni uhai, kazi ndio civilization, ndio uungwana, ndio kula vizuri, ndio kuvaa vizuri, ndio kuishi katika nyumba nzuri,…. ndio kushinda matatizo yote tuliyo nayo duniani – namna ya kuyashinda ni kazi….”[1]

76.    Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa hotuba hii, napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo kwa misaada na mikopo wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini.  Wahisani hao wanatarajiwa kuchangia jumla ya shilingi bilioni 2,676.6 katika bajeti ya mwaka 2018/19 kama ifuatavyo: Benki ya Dunia/IDA shilingi bilioni 863.13; Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) shilingi bilioni 358.63; Global Fund shilingi bilioni 313.90; Sweden shilingi bilioni 179.80; Jumuiya ya Umoja wa Ulaya shilingi bilioni 158.40; India shilingi bilioni 104.57; Ujerumani (Kfw & GIZ) shilingi bilioni 81.31; Japan/JICA shilingi bilioni 76.96; Uingereza/DFID shilingi bilioni 71.21; Denmark shilingi bilioni 69.57; French/AFD shilingi bilioni 61.06; Canada shilingi bilioni 48.84; BADEA shilingi bilioni 40.01; Korea ya Kusini/EDCH shilingi bilioni 39.05; UNICEF shilingi bilioni 36.53; Finland shilingi bilioni 28.08; IFAD shilingi bilioni 26.82; Italy shilingi bilioni 22.05; Norway shilingi bilioni 20.04; Benki ya Uwekezaji ya Ulaya shilingi bilioni 17.88; Uswisi shilingi bilioni 15.74; UNDP shilingi bilioni 12.34 ; Ubelgiji shilingi bilioni 11.08; Saudi Arabia/Saud Fund shilingi bilioni 4.81; USAID shilingi bilioni 4.20; OPEC/OFID shilingi bilioni 2.75; na UNFPA shilingi bilioni 2.56. Ni matarajio yetu kuwa fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kama nilivyozisoma na kwa wakati muafaka. Sisi kama Serikali tunaahidi kuwa fedha watakazotupatia zitatumika kama ilivyokusudiwa.

77.    Mheshimiwa Spika, ninakiri kuwa bajeti niliyowasilisha isingekuwa hivi ilivyo bila kupata michango mizuri ya kuboresha kutoka kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Sekretariaeti ya Baraza la Mawaziri na wataalam wa wizara zote na taasisi za Serikali. Ninatoa shukrani kwa kila mmoja wenu kwa michango mliyotoa katika mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti hii.

78.    Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, nikianza na Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji, Mbunge wa Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, pia Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu, na Bibi Susan B. Mkapa. Wote hawa kwa pamoja wamenipatia ushirikiano na msaada wa hali ya juu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na wameratibu vizuri maandalizi ya bajeti hii. Aidha, ninampongeza Profesa Florens Dominick Makinyika Luoga kwa kuteuliwa na Rais kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania na kwa kusimamia vema majukumu makubwa ya mhimili huo wa sekta ya fedha akisaidiwa na Naibu Gavana watatu, Wakurugenzi na watumishi wote wa Benki Kuu ya Tanzania. Vivyo hivyo, napenda kutambua kazi nzuri ya viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa na Bw. Charles E. Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Profesa Musa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Aidha, nampongeza Bwana Athumani Selemani Mbuttuka aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni kuwa Msajili wa Hazina (Treasury Registrar).

79.    Mheshimiwa Spika, vile vile, ninawashukuru Wakuu wengine wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikijumuisha Mabenki (TADB, TIB-DFI, TIB-CBL,TPB Bank); Mifuko ya hifadhi ya jamii (PSPF, GEPF, PPF); Rufani za kodi (TRAB, TRAT); Huduma za bima (TIRA,NIC); Mitaji na dhamana (CMSA, TCEM, DSE); Dhamana za uwekezaji (UTT-MFI, UTT-AMIS,UTT-PID); Bodi ya michezo ya kubahatisha; Taasisi za mafunzo (IFM, IRDP, IAA, TIA, EASTC); na Mfuko wa huduma ndogo za fedha (SELF Microfinance Fund). Nawashukuru pia Wakuu wa Idara na Vitengo, bila kuwasahau wataalam, makatibu muhtasi, watunza kumbukumbu, madereva, wahudumu na walinzi wa Wizara yetu na taasisi zake kwa kazi kubwa walizofanya katika mwaka 2017/18 na katika kukamilisha Bajeti hii.

80.    Mheshimiwa Spika, nashindwa kumaliza hotuba hii bila kumtaja mke wangu na rafiki yangu mpenzi Mbonimpaye. Moyo wake wa ibada kwa Mungu na uaminifu wake vimekuwa ndiyo nguzo yangu kuu katika utumishi wangu. Ninamshukuru sana yeye pamoja na watoto na wajukuu wetu wote tuliopewa na Mungu na familia nzima. Aidha, ninawiwa kuwashukuru wananchi wote wa Tanzania (wakulima, wafanyakazi, na wafanyabiashara). Ninawashukuru sana kwa uzalendo wao wa kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Ninawashukuru pia wanafunzi wote wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo wanaosoma kwa bidii maana miongoni mwao tutapata viongozi na nguvukazi bora ya Taifa. Ninawashukuru pia Wazee wetu ambao walitoa mchango mkubwa kwa Taifa letu katika umri wao wa kufanya kazi. Aidha, siwezi kuwasahau wananchi wa wilaya za Buhigwe na Kasulu, na mkoa wetu wa Kigoma kwa ujumla. Ninyi ni fahari yangu maana mlinikuza. Ninawapenda! Vile vile ninawashukuru wananchi wenzangu wa Nzinje hapa Dodoma (Zuzu kwa jina la zamani), kwa kunipokea vizuri mimi na familia yangu.

81.    Mheshimiwa Spika, kwa kuwa inatarajiwa leo itakuwa siku ya mwisho wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, naomba nihitimishe hotuba hii kwa kuwatakia Waislamu wote Eid Mubarak.

82.    Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema ASANTE SANA MUNGU” kwa baraka zako zilizoniwezesha kukamilisha kusoma hotuba hii. Na kwenu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote …….
(i)         “SANDENYI SANA”!
(ii)       “NGW’ABHEJA SANA”
(iii)     “WAITU MWAKORA”
(iv)     “OKORREE BHUYA”
(v)       “HAIKENI SANA”
(vi)     “MSENGWILE”
(vii)   “NDAGHA FIJO”
(viii)  “HEWELA”
(ix)     “KAJEKAJE”
(x)       “MURAKOZE CHANE”
(xi)     “ASANTENI SANA”

83.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja


Jedwali Na 1: Mwenendo wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali: 2011/12 -2018/19        Shilingi  Milioni

2012/13
2013/14
2014/15
2015/16
2016/17
2017/18
2017/18
2018/19

Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Bajeti
Matarajio
Bajeti
Jumla ya Mapato (Yakijumuisha Halmashauri)
8,442,611
11,537,523
10,957,765
14,139,230
16,639,933
19,977,001
18,692,251
20,894,578


A. Mapato yanayotokana na Kodi
7,729,986
10,395,440
9,908,996
12,525,378
14,126,590
17,106,336
15,312,632
18,000,219

 1.  Ushuru wa Forodha
584,137
852,199
748,961
880,296
998,164
1,231,135
1,077,034
1,204,090

 2.   Ushuru wa Bidhaa
1,258,242
1,908,857
1,742,721
2,144,395
2,106,442
2,776,302
2,248,954
2,541,287

 3.   Kodi ya Ongezeko la Thamani
2,146,337
2,590,291
2,488,066
2,992,835
3,912,674
4,767,853
4,390,218
5,463,990

 4.   Kodi ya Mapato
3,034,360
3,656,506
3,716,685
4,594,971
5,117,862
5,997,039
5,556,523
6,540,038

 5.   Kodi Nyingine
706,910
1,387,587
1,212,563
1,912,880
1,991,449
2,334,006
2,039,904
2,250,814


B. Mapato yasiyotokana na Kodi
683,362
869,936
1,048,769
1,613,852
2,513,343
2,870,665
3,379,619
2,894,358

 1.   Michango na Gawio la Mashirika
47,602
110,014
161,234
388,551
893,935
529,583
646,415
597,770

 2.   Wizara Nyingine na Mikoa
414,925
444,694
527,451
799,449
1,107,690
1,653,776
2,183,359
1,561,000

 3.   Mapato ya Halmasahuri
220,835
315,228
360,084
425,852
511,718
687,306
549,845
735,589

Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango






Jedwali 2a: Mfumo wa Bajeti 2011/12-2018/19                                                                                   Shilingi  Milioni


2010/11
2011/12
2012/13
2013/14
2014/15
2015/16
2016/17
2017/18
2017/18
2018/19

Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Bajeti
Matarajio
Matarajio
I. Mapato Yote
10,202,603
12,171,877
15,404,216
15,667,535
17,488,626
22,543,664
25,417,791
31,711,986
28,619,612
32,475,949
Mapato ya Ndani
5,577,986
7,025,884
8,221,776
9,867,227
10,597,681
13,622,182
16,128,215
19,289,695
17,639,052
20,158,989
Mapato ya Halmashauri
158,280
195,525
220,835
315,228
360,084
425,852
511,718
687,306
549,845
735,589
Misaada na Mikopo ya Bajeti
900,825
967,163
894,955
1,040,659
757,016
291,381
342,785
941,258
684,227
545,765
Misaada na Mikopo ya Miradi
1,013,078
1,207,445
1,423,579
1,194,930
1,154,909
1,186,982
1,857,399
2,473,770
1,804,663
2,005,016
Mikopo ya Kisekta (Basket Loans)
220,681
172,212
186,336
207,665
163,177
161,842
104,991
355,454
355,454
33,701
Misaada ya Kisekta (Basket Grants)
334,609
301,152
280,936
188,623
127,637
86,199
168,984
200,621
177,799
92,163
MCA (T) USA
196,114
221,601
220,350
213,612
0
0
0
0
0
0
Mikopo ya Ndani (Rollover)
720,249
1,326,852
1,734,535
1,528,153
2,064,756
3,005,789
4,615,670
4,948,229
4,835,199
4,600,000
Mikopo  ya Ndani (Financing)
1,244,330
334,864
1,069,321
976,712
799,776
2,299,151
1,300,000
1,220,668
1,199,373
1,193,669
Marekebisho
-317,498
-382,101
88,588
-1,059,790
408,786
1,010,781
-838,731
0
0
0
Mikopo ya kibiashara
153,948
801,282
1,063,006
1,194,516
1,054,803
453,504
1,226,760
1,594,985
1,374,000
3,111,058











II. Matumizi Yote
10,202,602
12,171,877
15,404,216
15,667,535
17,488,626
22,543,664
25,417,791
31,711,986
28,619,612
32,475,950
Matumizi ya Kawaida
7,453,565
8,397,155
10,904,521
11,741,493
13,778,397
18,204,111
18,144,967
19,712,394
19,302,746
20,468,676
CFS
1,625,883
2,518,207
3,383,124
3,666,799
4,724,910
6,480,906
8,643,560
9,461,433
9,892,197
10,004,480
Kulipa Madeni
1,116,572
1,843,666
2,627,946
2,686,455
3,552,426
5,047,764
7,234,530
7,829,918
8,260,682
8,372,951
Malipo Mengine
509,311
674,541
755,178
980,344
1,172,484
1,433,142
1,409,030
1,631,515
1,631,515
1,631,529
Matumizi ya Kawaida (Bila CFS)
5,827,682
5,878,949
7,521,397
8,074,693
9,053,487
11,723,205
9,501,407
10,250,961
9,410,549
10,464,196
o/w   Malipo ya Mishahara
2,346,378
2,722,084
3,349,959
3,969,108
4,617,648
5,627,497
5,599,246
6,276,267
5,962,454
6,386,265
 Mishahara ya Mashirika
457,665
455,006
518,755
568,708
637,711
925,760
767,901
929,501
883,026
1,023,687
 Fedha ya Halmashauri
158,280
195,525
362,206
315,228
170,627
170,340
251,484
274,922
274,922
389,862
 Matumizi Mengine
3,628,554
2,506,333
3,290,477
3,221,649
3,627,501
4,999,607
2,882,775
2,770,270
2,290,147
2,664,382
Matumizi ya Maendeleo
2,749,037
3,774,722
4,499,695
3,926,042
3,710,228
4,339,553
7,272,824
11,999,592
9,316,866
12,007,273
Fedha za Ndani
984,555
1,872,312
2,314,718
2,121,212
2,264,506
2,904,530
5,141,451
8,969,747
6,978,950
9,876,393
Fedha za Nje
1,764,482
1,902,410
2,184,977
1,804,831
1,445,722
1,435,023
2,131,374
3,029,845
2,337,916
2,130,880
Pato la Taifa
48,607,221
57,098,397
66,193,721
75,197,863
85,153,090
97,304,216
106,589,234
120,866,799
118,737,328
132,629,849

Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
Jedwali 2b: Mfumo wa Bajeti 2010/11 - 2018/19
Asilimia ya Pato la Taifa

2011/12
2012/13
2013/14
2014/15
2015/16
2016/17
2017/18
2017/18
2018/19

Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Halisi
Bajeti
Matarajio
Bajeti
Mapato Yote
21.3%
23.3%
20.8%
20.5%
23.2%
23.8%
26.2%
24.1%
24.5%
Mapato ya Ndani
12.3%
12.4%
13.1%
12.4%
14.0%
15.1%
16.0%
14.9%
15.2%
LGAs own source
0.3%
0.3%
0.4%
0.4%
0.4%
0.5%
0.6%
0.5%
0.6%
Misaada na Mikopo ya Bajeti
1.7%
1.4%
1.4%
0.9%
0.3%
0.3%
0.8%
0.6%
0.4%
Misaada na Mikopo ya Miradi
2.1%
2.2%
1.6%
1.4%
1.2%
1.7%
2.0%
1.5%
1.5%
Mikopo ya Kisekta (Basket Loans)
0.3%
0.3%
0.3%
0.2%
0.2%
0.1%
0.3%
0.3%
0.0%
Misaada ya Kisekta (Basket Grants)
0.5%
0.4%
0.3%
0.1%
0.1%
0.2%
0.2%
0.1%
0.1%
MCA (T) USA
0.4%
0.3%
0.3%
0.0%
0.0%
0.0%
0.0%
0.0%
0.0%
Mikopo ya Ndani (Rollover)
2.3%
2.6%
2.0%
2.4%
3.1%
4.3%
4.1%
4.1%
3.5%
Mikopo  ya Ndani (Financing)
0.6%
1.6%
1.3%
0.9%
2.4%
1.2%
1.0%
1.0%
0.9%
Marekebisho
-0.7%
0.1%
-1.4%
0.5%
1.0%
-0.8%
0.0%
0.0%
0.0%
    Mikopo yenye masharti ya kibiashara
1.4%
1.6%
1.6%
1.2%
0.5%
1.2%
1.3%
1.2%
2.3%










II. Matumizi Yote
21.3%
23.3%
20.8%
20.5%
23.2%
23.8%
26.2%
24.1%
24.5%
Matumizi ya Kawaida
14.7%
16.5%
15.6%
16.2%
18.7%
17.0%
16.3%
16.3%
15.4%
CFS
4.4%
5.1%
4.9%
5.5%
6.7%
8.1%
7.8%
8.3%
7.5%
Kulipa Madeni
3.2%
4.0%
3.6%
4.2%
5.2%
6.8%
6.5%
7.0%
6.3%
Malipo Mengine
1.2%
1.1%
1.3%
1.4%
1.5%
1.3%
1.3%
1.4%
1.2%
Matumizi ya Kawaida (Bila CFS)
10.3%
11.4%
10.7%
10.6%
12.0%
8.9%
8.5%
7.9%
7.9%
o/w Malipo ya Mishahara
4.8%
5.1%
5.3%
5.4%
5.8%
5.3%
5.2%
5.0%
4.8%
Mishahara ya Mashirika
0.8%
0.8%
0.8%
0.7%
1.0%
0.7%
0.8%
0.7%
0.8%
Fedha za Halmashauri
0.3%
0.5%
0.4%
0.2%
0.2%
0.2%
0.2%
0.2%
0.3%
Matumizi Mengine
4.4%
5.0%
4.3%
4.3%
5.1%
2.7%
2.3%
1.9%
2.0%
Matumizi ya Maendeleo
6.6%
6.8%
5.2%
4.4%
4.5%
6.8%
9.9%
7.8%
9.1%
Fedha za Ndani
3.3%
3.5%
2.8%
2.7%
3.0%
4.8%
7.4%
5.9%
7.4%
Fedha za Nje
3.3%
3.3%
2.4%
1.7%
1.5%
2.0%
2.5%
2.0%
1.6%










Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango

Jedwali Na. 3 Misaada na Mikopo Nafuu kutoka Nje 2014/15 - 2018/19
Shilingi Milioni

2014/15
2015/16
2016/17
2017/18
2017/18
2018/19

Halisi
Halisi
Halisi
Bajeti
Matarajio
Bajeti








Misaada ya Kibajeti
Misaada
546,709
0
190,303
190,023
190,613
236,264
Mikopo yenye Masharti Nafuu
375,459
291,381
152,482
751,235
493,614
309,501

Jumla
922,168
291,381
342,785
941,258
684,227
545,765


Mifuko ya Kisekta
Misaada
       189,112
        86,199
       168,984
       200,621
       177,799
        92,163
Mikopo yenye Masharti Nafuu
84,975
161,842
104,991
355,454
355,454
33,701

Jumla
274,087
248,041
273,975
556,075
533,253
125,864


Miradi ya Maendeleo
Misaada
       745,344
       409,157
       733,208
       853,815
       607,101
          752,982
Mikopo yenye Masharti Nafuu
    1,000,000
       777,825
    1,124,190
    1,820,576
    1,197,563
    1,252,035

Jumla
  1,745,344
  1,186,982
  1,857,399
  2,674,391
  1,804,663
  2,005,016

Jumla Kuu
2,941,599
1,726,404
2,474,159
4,171,723
3,022,143
2,676,645






Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango



Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango


















[1] Insha Tatu za Kifalsafa, Julius Nyerere, Kivazi Occassional Papers, No. 3, 2016









No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.