Habari za Punde

Uwezekano Mkubwa wa Zanzibar Kugeuka Kuwa Dubai ya Afrika Kutokana na Juhudi za Serikali ya SMZ. -Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia Bibi Donna Massie, alipomtembelea katika Ofisi yake Ndogo katika majengo ya Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar kwa mazungumzo leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia Bibi Donna Massie, alipokuwa na mazungumzo yao yaliofanyika katika Ofisi yake katika jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia Bibi Donna Massie, alipokuwa na mazungumzo yao yaliofanyika katika Ofisi yake katika jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar. kushoto Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe. Balozi Amina Salum Ali na Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Ndg. Juma Ali Juma. wakiwa katika mazungumzo hayo.
Maofia wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar wakifuatilia mazungumzo hayo  yaliofanyika katika Ofisi Ndogo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yaliofanyika katika majengo ya Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema upo uwezekano mkubwa wa Zanzibar kugeuka kuwa Dubai ya Afrika kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Miundombinu tofauti.
Alisema Sekta ya Utalii hivi sasa inaendelea kushamiri katika kuliongezea mapato Taifa licha ya upande mwengine kupanua fursa za ajira hasa kwa Vijana   ambao wengi kati  yao wanaendesha maisha  kupitia sekta hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia Bibi Donna Massie  kwenye Ofisi yake ndogo iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema fursa zinazoendelea kutolewa katika masuala ya kukaribisha Uwekezaji Vitega Uchumi ndani na nje ya Nchi zinaifanya Zanzibar kuelekea katika uchumi imara unaoweza kupunguza utegemezi wa Nje.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshauri Kamishna huyo wa Biashara na Uwekezaji Bibi Donna Massie kutoka Nchini Australia kuyashawishi Makampuni na Taasisi za Nchi hiyo kuzitumia fursa zilizopo Zanzibar katika kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi.
Alisema zipo Rasilmali nyingi kwenye Sekta ya Kilimo, Viwanda, Mawasiliano na hata Afya ambazo Makampuni na Taasisi za Nchi hizo zinaweza kuzitumia hata katika Mpango wa  Ubia katika kushirikiana na Taasisi za Kizalendo.
Balozi Seif alieleza kwamba Wataalamu wa Sekta ya Nishati  walipewa jukumu la kufanya utafiti wa upatikanaji wa Nishati Mbadala ya Umeme ili kuondokana na utegemezi wa mfumo mmoja tu wa upatikanaji wa huduma za Umeme kutoka Tanzania Bara.
Alisema ripoti za awali za utafiti huo uliogharamiwa na kusimamiwa na Umoja wa Ulaya {EU} zimeonyesha  uwezekano wa matumizi ya Umeme unaotokana na Nguvu za Jua pamoja na Upepo.
Hatuahiyo imechukuliwa na Serikali Kuu katika kuhakikisha kwamba changamoto zozote zitakazojitokeza katika miradi ya kiuchumi na ile ya Uwekezaji zisiweze kuteteresha  Miradi hiyo kutokana na hitilafu zinazoweza kujichomoza katika upatikanaji wa huduma za Umeme.
Naye kwa upande wake Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia Bibi Donna Massie aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa umakini wake wa kuhakikisha Taifa linaelekea katika mfumo wa kuondokana na Mpango wa utegemezi katika Uchumi wake.
Hata hivyo Bibi Donna alitanabahisha kwamba Teknolojia mpya iliyopo hivi sasa inakuwa kwa haraka Duniani kiasi cha kuishauri Zanzibar iwe makini katika muelekeo wake wa kutaka kuingia katika Miradi mipya ya Mafuta na Gesi Asilia  hasa ikizingatia zaidi suala la Mazingira.
Kamishna wa Biashara na Uwekezaji kutoka Nchini Australia yupo Zanzibar kuangalia fursa ambazo Makampuni na Taasisi za Uwekezaji za Nchini mwake zinaweza kutumia nafasi hiyo kuwekeza Miradi yao Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.