Habari za Punde

Waandishi wa Idara ya Habari Zanzibar Wapigwa Msasa. Kufanya Kazi Zao Kwa Ufanisi.

Na Miza Kona.-Maelezo   Zanzibar. 23/06/2018
Wafanyakazi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar wametakiwa kufuata kanuni ya sheria za utumishi wa Umma ili kuweza  kutekeleza vyema majukumu yao kwa ufanisi.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo katika utendaji wa kazi Mkurugenzi wa Idara hiyo  Bw. Hassan Vuai  katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo amesema ni wajibu wa kila mfanyakazi kujua haki na wajibu ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake.
Amesema wafanyakazi wa Utumishi wa Umma ni lazima kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na Utumishi kwa lengo la kutekeleza vyema majukumu waliyopangiwa ili kuweza kufanyakazi kwa uelewa.
Nae Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mussa Suleima Muftah amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuelewa wajibu na haki zake pamoja na sheria na miongozo mbalimbali katika utendaji wake wa kazi.
Amefahamisha sheria zinaongoza kujua haki na wajibu kwa mfanyakazi pamoja na wafanyakazi kufanyakazi kwa bidii ili waweze kupata haki zao kwa kufuata miongozo ya sheria.
“Utii ni suala la msingi katika kufanikisha malengo ya kazi pamoja kuzielewa sheria za utumishi zinazomlinda na kumwongoza katika utekelezaji wa majukumu yake”, alifahamisha Mwezeshaji huyo.
Nae  Mwezeshaji kutoka Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Khamisuu Hamid Moh’d amesema nidhamu ni jambo muhimu katika utendaji kwani inaleta heshima na utekelezaji mzuri  wa kazi.
Amefahamisha kuwa wafanyakazi wana haki ya kupata taarifa ya kustaafu ndani ya miezi sita pindipo mfanyakazi hakupata taarifa mapema Idara ina haki ya kumlipa mshahara kwa kipindi ambacho hakupata taarifa hiyo.
Mwisho
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.