Habari za Punde

ZEC MPYA, MATUMAINI MAPYA

Na. Mwandishi Wetu.
Kuundwa upya kwa Tume ya  Uchaguzi Zanzibar kumetoa matumaini mapya kwa wananchi hasa wapigakura waliowengi kwamba  itasimamia misingi ya sheria na utawala bora katika shughuli za Uchaguzi Zanzibar.

Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe Hamid Mahmoud ambaye kila mmoja anakiri na kukubali uwezo, uzoefu wake na uzalendo kwa nchi yake.

Amekuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania, amebobea katika Utumishi wa Umma na ni mtu mzima mwenye busara na hekima. Tunaamini chini ya uongozi wake katika ZEC, vile visa na vitimbi vya baadhi ya wanasiasa sasa vimepata tiba.

Wajumbe wengine wa ZEC nao ni watu wenye kuheshimika, kukubalika katika jamii na hakuna anaewatilia shaka juu ya uzalendo wao kwa Nchi, ijapokuwa wapo wachache ambao wao kila jambo lazima wapinge tusiwatarajie kufurahia Tume mpya ya Uchaguzi Zanzibar hasa baada ya kuwaona wajumbe waliokuwa makini na weledi ambao hawataweza kuwasaliti Wazalendo wenzao wa Nchi hii.

Wale wanaopinga au kukosoa Tume mpya eti kwa sababu ya sura, kutokumpenda mtu kwa ubinafsi au kwa sababu za kiitikadi za kisiasa nadhani tuwasamehe kwa sababu binadamu hatuwezi kufikiri sawa na kwa sababu ya ukweli huo kuna jambo hapa nalikumbuka.

Wale waliokula chumvi nyingi na hasa wale manazi wa muziki wa dansi bado wanaikumbuka ile bandi maarufu iliyowahi kutamba siku hizo Dar Jazz au almaarufu pale Jijini Dar es Salaam, kama “Majini wa Bahari” ambao waliimba wimbo wao wa “Mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe”.

Wimbo huo ni kibwagizo chenye ujumbe mahsusi ambao uliotungwa na kupigwa na bendi hiyo, mwishoni mwa miaka ya sitini.

Simulizi zinaeleza kuwa Dar Jazz walitunga na kuuimba wimbo huo uliokuwa mashuhuri sana enzi zake kama kijembe kwa wapinzani wao Western Jazz (Wana Saboso) kutokana na upinzani uliokuwepo baina ya bendi hizo, kila moja ikijinadi kuwa bora kuliko mwenzake.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafanyika mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria, tunaamini kuwa Tume mpya ya Uchaguzi itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na sio vyenginevyo, hivyo hakuna sababu yoyote ya mtu au kikundi au Chama cha siasa kuanza kuingia woga.

Tuna kila sababu kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mhe Dk Ali Mohamed Shein kwa hekima na busara kubwa kumteua Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchagizi.

Uteuzi uliofanywa na Mhe Rais Dk Shein umeakisi dhamira za Uongozi wake, Uzalendo wake na uaminifu wake, uadilifu wake. Sote tumpongezeni Rais wetu Dk Shein.
Kwaheri Jecha, Karibu Jaji Hamid Mahmoud!

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.