RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali
ya Kuwait kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali
mbali za maendeleo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jasem Ibrahim Al-Najem aliyefika Ikulu
kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini Tanzania.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Jasem Ibrahim Al-Najem kuwa Zanzibar inathamini
sana hatua za Kuwait za kuendelea kuiunga mkono katika kuimarisha sekta mbali
mbali za maendeleo.
Kutokana na juhudi
hizo, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar itaendeleza
uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya pande mbili hizo huku akieleza
kuwa Kuwait imekuwa mshirika mzuri wa Tanzania.
Alieleza kuwa hatua
hizo zimepelekea kuimarisha na kukuza diplomasia kwa pande mbili hizo ambayo
ina historia kubwa ambayo imetokana na wananchi wa Kuwait na ukanda mzima wa
Gulf waliweza kufika Zanzibar.
Rais Dk. Shein
aliongeza kuwa Kuwait imeweza kuimarisha na kukuza uhusiano na Zanzibar kwa
kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ya kilimo, afya, miundombinu
ya barabara ikiwemo Barabara ya Chake Chake Wete, maji na mengineyo.
Dk. Shein pia alitumia
fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Kuwait kwa kuiunga mkono Zanzibar kwa
kusaidia vifaa mbali mbali kwa ajili ya sekta ya kilimo na sekta ya afya ambavyo
vilikabidhiwa leo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk.
Shein aliipongeza Serikali ya Kuwait kwa
kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya
kupitia Jumuiya yake ya ‘Kuwait Red Crescent Society’ huku akitoa shukurani na
pongezi kwa nchi hiyo kwa azma yake ya kusaidia ukarabati wa hospitali Kuu ya
MnaziMmoja na Mwembeladu.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo wa Kuwait na Serikali yake kwa azma yao ya
Shirika la Ndege la nchi hiyo ‘Kuwait Airways’ kuanza safari zake hapa nchini
na kusema kuwa hatua hiyo itaimarisha uhusiano na ushirikiano sambamba na
kuimarisha sekta ya utalii.
Dk. Shein alimpongeza
Balozi huyo kwa juhudi zake kubwa alizozichukua katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya
nchi yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar unaimarika, jambo ambalo amefanikiwa kwa
kiasi kikubwa.
Nae Balozi wa Kuwait
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jasem Ibrahim Al-Najem alimpongeza Rais Dk. Shein kwa mashirikiano
makubwa aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
wananchi wake.
Balozi Jasem Al-Najim
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Kuwait itaendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa azma ya
kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.
Katika maelezo yake
Balozi Jasem Al-Najem alimueleza Dk. Shein, kuwa Shirika la Ndege la nchi hiyo
‘Kuwait Airways’ linatarajia kuanza safari zake hivi karibu hapa nchini hatua
ambayo itazidi kuimarisha sekta ya utalii.
Aliongeza kuwa idadi
ya watalii wanaokuja kutoka nchini Kuwait imeongeza kwa kiasi kikubwa hivyo
kuanza kwa safari kwa ndege za Shirika hilo moja kwa moja kati ya Kuwait na
Tanzania ikiwemo Zanzibar kutasaidia kuongeza ujio wa watalii kutoka nchi hiyo
ambao kwa hivi sasa wamekuwa wakitumia mashirika mengine ya ndege.
Aidha, Balozi Jasem
Al-Najim alimueleza Rais Dk. Shein kuwa vifaa mbali mbali vilivyotolewa na
Serikali yake ambavyo vimekabidhiwa leo vikiwemo vifaa kwa ajili ya sekta ya
kilimo yakiwemo matrekta na vifaa kwa ajili ya sekta ya afya vikiwemo vifaa kwa
ajili ya Benki ya Damu ambayo ni ishara tosha ya kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo
kati ya pande mbili hizo.
Balozi huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Serikali ya Kuwait inathamini uhusiano
uliopo na kuahidi kuuimarisha huku akitumia futrsa hiyo kueleza kuwa Balozi
anayekuja ataendeleza yale yote yaliyoanzushwa pamoja na mengine mapya kutoka
nchini humo.
Nae Makamo Mwenyekiti
wa ‘Kuwait Red Crescent Society’ Anwar
Abdullah Al-Hasawi ambaye alifuatana na Balozi huyo, alimuhakikishia Rais Dk.
Shein kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kuiunga mkkono Zanzibar na kuendeleza miradi
mbali mbali waliyoianza pamoja na kuanzisha mipya ambapo miongoni mwa miradi
inayoiendelea hivi sasa ni mradi wa ‘Mama na Mtoto’.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment