Habari za Punde

Obama Asema Mfumo wa Dunia Unafeli Kutimiza Wajibu Wake

Obama amesema wanasiasa wanaoeneza siaza za hofu, wanaongezeka kwa kasi isiyofikirika ikilinganishwa na miaka michache iliyopita.

Rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama amehutubia umati wa watu 15,000 nchini Afrka Kusini, katika maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa hayati Nelson Mandela.
Barrack Obama amesema ulimwengu unaelekea katika njia isiyo ya kawaida na ambayo ni ya kuhofisha. Akihutubia umati mkubwa katika maadhimisho ya kila mwaka ya hayati Nelson Mandela katika uwanja wa kriketi mjini Johannesburg-Afrika Kusini, Obama amesema kila siku matukio yanayogonga vichwa vya habari ni ya kushangaza.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (Kushoto) akisima na rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (aliyesimama kushoto) akisima na rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama (aliyesimama kulia)
Obama pia amesema kuwa mfumo wa kiulimwengu umeshindwa kutimiza wajibu wake."Tunahitaji kutambua kuwa mfumo wa kiulimwengu umekosa kutimiza ahadi yake. Ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kufeli kwa mfumo wa kiulimwengu ni kushindwa kwa serikali mbalimbali kuwajibika, na watu wenye ushawishi kushindwa kusuluhisha tofauti na mapungufu katika jumuiya ya kimataifa, hivi kwamba sasa tunaona kitisho cha kurudia njia hatari ya zamani ya kutatua shida."
Japo Obama hakumtaja moja kwa moja mrithi wake Rais Donald Trump, hotuba yake imezungumzia masuala kadhaa yanayogusia sera kadhaa za Donald Trump, huku akiwahimiza watu kuendeleza mawazo ambayo Nelson Mandela alipigania ikiwemo demokrasia, utangamano na elimu bora kwa wote. Ameongeza kuwa
"Lazima tuanze kwa kufahamu kuwa licha ya sheria nzuri zilizoko kwenye katiba, au vipengee vizuri kwenye katiba au kauli nzurinzuri kuwahi kutolewa katika majukwaa ya kimataifa au Umoja wa Mataifa katika miongo ya hivi karibuni, unyanyasaji na dhuluma za kale hazitoweki."
Obama amesema wanasiasa wanaoeneza siaza za hofu, uhasama na kubana matumizi wanaongezeka 
kwa kasi isiyofikirika ikilinganishwa na miaka michache iliyopita.
Mchoro wa hayati Nelson Mandela
Mchoro wa hayati Nelson Mandela
Mandela aliyefariki dunia mwaka 2013, amesalia kuwa shujaa duniani kote kufuatia mapambano yake ya muda mrefu kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi ulioendelezwa na wazungu walio wachache nchini humo na ujumbe wake wa amani na maridhiano alipoachiliwa huru baada ya kufungwa gerezani kwa miaka 27.
Hotuba ya Obama inajiri siku moja tu kabla ya siku kamili ijulikanayo kama Mandela Day yaani Siku ya kuzaliwa kwa Mandela ambayo huadhimishwa duniani kote Julai 18.
Mwandishi: John Jma/DPAE/APE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.