Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akiagana na Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Balozi Seif Ali Iddi (kulia) katika Uwanja wa Ndge wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume alipokuwa akiondoka Nchini leo kuelekea Indonesia katika ziara ya Kikazi akifauatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein (hayupo pichani) pamoja na Watendaji wengine wa Serikali,[Picha na Ikulu.] 30/07/2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein anaondoka nchini leo kuelekea Indonesia kwa
ziara ya wiki moja kufuatia muwaliko wa Makamo wa Rais wa Nchi hiyo Muhammad Jusuf
Kalla.
Ziara hiyo ya Dk. Shein inatarajiwa
kuanza Agusti 1 na kumaliza Agusti 5 mwaka huu katika nchi hiyo ambapo
anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake
Makamo wa Rais wa nchi hiyo Muhammad Jusuf Kalla pamoja na viongozi
wengine mbali mbali wa ngazi za juu wa Serikali na sekta binafsi wa nchi hiyo.
Katika ziara hiyo Dk.
Shein anatarajiwa kutembelea katika kisiwa cha Bali ambacho ni kisiwa maarufu kwa
utalii duniani na kufanya mazungumzo ya pamoja na viongozi wakuu wa kisiwa
hicho.
Rais Dk. Shein akiwa nchini
Indonesia atapata fursa ya kukutana na Wafanyabiashara na Wenyeviwanda kupitia
Jumuiya yao ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda wa nchi hiyo huko mjini Jakarta katika
mkutano maalum uliotayarishwa kwa ajili ya Rais Dk. Shein na ujumbe wake na Jumuiya
hiyo.
Pia, Rais Dk. Shein
anatarajiwa kutembelea Kampuni ya Uvuvi pamoja na Hospitali ya Harapan Kita
iliyopo mjini Jakarta.
Akiwa katika kisiwa cha
Bali Rais Dk. Shein atapata fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Udayana,
Jimbaran kiliopo mjini Bali pamoja na kutembelea kituo Kikuu cha Utalii katika
mji huo.
Rais Dk. Shein pia, atatembelea
katika kiwanda cha mafuta ya nazi na kutembelea eneo la mashamba ya mpunga huko
Tabanan pamoja na kutembelea maeneo ya utamaduni pamoja na kutembelea kiwanda
cha kusarifu mwani.
Katika
ziara hiyo, Dk. Shein amefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mke wa Rais wa
Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Biashara na
Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk. Susan Alphonce Kolimba, Mshauri wa Rais Masuala ya
Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Fedha Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine
ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam Saadalla,
Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ofisi ya Zanzibar pamoja na Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis
Nassor na
watendaji wengine wa Serikali.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa
kurejea nchini Jumatatu ya tarehe 6 Agosti, 2018.
Katika
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Dk. Shein aliagwa na viongozi
mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali, viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na
Usalama pamoja na wananchi ambao
waliongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment