Habari za Punde

Tuhuma za wanafunzi skuli ya Muembeladu kutoleshwa pesa wakichelewa kuchunguzwa

Na Takdir Ali,                                                    11-07-2018.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Muhammed Mahmoud ameunda Tume  ya Watu 5 kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Wanafunzi wa Skuli ya Muembeladu ya kutoleshwa pesa wanapochelewa Skuli na kusahihishiwa Mabuku yao ili kuweza kubaini ukweli wa suala hilo.
Amesema Serikali imepiga marufuku Waalimu kuwachangisha wanafunzi michango ya aina yoyote lakini kuna baadhi ya Waalimu wamekuwa wakikaidi agizo hilo na kupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.
Ameyasema hayo huko ofisini kwake Vuga alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya Wanafunzi wa Muembeladu kusikika katika vyombo vya habari wakitoa malalamiko ya kutoleshwa michango na baadhi ya Waalimu.
Ayoub ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Mjini Magharibi amesema licha ya kuwa suala la elimu ya Sekondari lipo Wizara ya elimu lakini wao kama Mkoa wanahusika kwa namna moja au nyengine na ndio akaamua kuunda kamati hiyo itakayofanya kazi kwa muda wa wiki moja na kutoa ripoti juu ya suala hilo.
Amefafanua kuwa maba baada ya kamati kukamilisha kazi hiyo watakaa na Watendaji wa Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali ili kujadiliana na kuhakikisha kama kuna Mwalimu yoyote aliehusika na tendo hilo achukuliwe hatua zinzofaa kwa mujibu wa Taratibu na Sheria zilizowekwa.
Ayoub ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mjini Magharibi amesema imeshtushwa na tuhuma hizo,zinazoitia dosari Serikali kwani tayari imeshatangaza elimu bila malipo kwa hiyo kuwachangisha wanafunzi ni kuenda kinyume na maagizo ya Serikali.
“Tumechoka kila siku kusikia Waalimu wanawatolesha michango Wanafunzi , suala hili halivumiliki hata kidogo,Mimi kama Mkuu wa Mkoa nitalisimamia kuhakikisha haki inatendeka bila kumuonea Mtu,” Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Ameeleza kuwa Serikali imeamua kutangaza elimu bure baada ya kuona kuna baadhi ya Wananchi hawana uwezo wa kulipia huduma hizo hivyo kitendo cha baadhi ya Waalimu kuwatolesha michango Wanafunzi ni kukiukwa maadili na kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.
Hata hivyo amesema Kamati za Skuli zinaweza kutolesha michango kwa Wazazi kwa jambo makhsusi kama vile kutengeneza Vyoo vilivyoharibika baada ya kukaa pamoja na kujadiliana isiwe suala la lazima bali ni iwe ni hiari.
Kwa upande wake Mwenyeikti wa kamati ya kufuatilia malamiko hayo ya wanafunzi ambae ni Katinu Tawla wa Mkoa wa Mjini Hamida Mussa Khamis amesema wamelipokea jukumu hilo na kuahidi kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kufika katika Skuli hiyo na kufanya mazungumzo na Waalimu,Kamati ya Skuli na Wanafunzi ili waweze kufahamu ukweli wa jambo hilo.
Tume ilioundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mummed Mahmoud kinaundwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,Kamanda wa Usalama Mkoa na Mjumbe kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchimi Zanzibar (ZAECA).
                 Imetolewa na Idara ya Habar Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.