Habari za Punde

Balozi Seif atembelea maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Kati.


 Balozi Seif akilakiwa na Viongozi wa Mkoa Morogoro akishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa huo Dr.Kebwe Stephen Kebwe Kati kati. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa Mkoa Morogoro alipowasili kwa ajili ya kuyatembelea Maonyesho ya Siku ya Nane Nane Kanda ya Kati Mkoani humo.
 Mkuu wa Mkoa Morogoro  Dr.Kebwe Stephen Kebwe Kati kati akitoa taarifa fupi ya Ziara ya Balozi Seif  aliyekaa kwenye Kochi wa kwanza kushoto aliyefika kuyatembelea maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Kati.
Katibu Talawa wa Mkoa Morogoro Bwana Clifford Katondo akimueleza Balozi Seif mfumo wa uendeshaji wa maonyesho ya Nane Nane yanayofanyika Mkoani humo hapo Ikulu ndogo ya Mkoa wa Morogoro.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mfumo wa uwepo wa maonyesho mahali popote pale ni moja ya njia muwafaka inayomuwezesha Mwanaadamu kujifunza mbinu mbali mbali za kuendesha maisha yake kitaalamu zaidi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo baada ya kupokea taarifa  fupi ya Ratiba aliyopangiwa na Uongozi wa Mkoa Morogoro kwenye Ikulu ndogo Mkoani humo ya kutembelea Maonyesho ya Siku ya  Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika katika Uwanja wa Nane Nane Mkoani Morogogoro.
Balozi Seif  alisema mabadiliko ya uzalishaji katika Sekta ya kilimo ambayo ndio inayochukuwa idadi kubwa ya Wananchi Tanzania yameanza kuonekana kutokana na Wakulima wengi  Nchini hivi sasa wameamua kuzingatia  mfumo wa Elimu kwa Wakulima unaowapa uwezo wa kuzalisha mazao mengi kwa kutumia Ardhi ndogo.
Alisema upo mfano hai unaoendelea kushuhudiwa wa Kilimo cha  Kisasa cha Mpunga  Maarufu Shadid ambacho kimeonyesha mafanikio makubwa Tanzania Bara na hata upande wa Zanzibar  kimeanza kutumika na kuleta faida kubwa kwa Wakulima walioamua kukitumia.
Alisema wakati umefika kwa Vijana waliowengi Nchini hasa wale wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na Vyuo Vikuu kujikita katika Sekta ya Kilimo yenye uwezo wa kutoa ajira pana yenye faida ya haraka tofauti na mawazo ya Watu wengi.
Balozi Seif alieleza kwamba Vijana wanapaswa kuanza mapema kujifunza mbinu za Kilimo cha Kisasa suala ambalo alisema tayari ameshalisisitiza wakati akiyafungua Maonyesho ya Siku ya Nane Nane Upande wa Zanzibar hapo Juzi  eneo la  Kizimbani Wilaya ya Magharibi “A”.
Akitoa Taarifa fupi ya Ratiba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  ya kutembelea Maonyesho ya Siku ya Nane Nane Kanda ya Kati Mkoani Morogoro Mkuu wa Mkoa  huo Dr. Kebwe Stephen Kebwe alisema Uwanja wa Nane Nane Kanda ya Kati Mkoani Morogoro umeamuliwa kufanywa kuwa eneo la Kiuchumi.
Dr. Kebwe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hilo litaendelea kutoa huduma za mafunzo pamoja na mauzo ya bidhaa zinazozalishwa na Taasisi, Makampuni na Wajasiri Amali mbali mbali Nchini kwa Mwaka mzima ambapo JKT pamoja na baadhi ya Taasisi nyengine tayari zimeshaonyesha mfano wa kuanza kwa mpango huo.
Alieleza kwamba Maonyesho hayo yaliyolenga zaidi kwenye Sekta za Kilimo na Mifogo yamekadiriwa kukusanya jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 385,000,000/-  kunakotarajiwa kuwa na ongezeko la Shilingi Milioni 39,000,000/- ikilinganshwa na Maonyesho yaliyopita ya Mwaka 2017 ambapo zilikusanywa shilingi Milioni 246,000,000/-.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bwana Clifford Ktondo alisema asilimia 74 ya Wazee wa Morogoro ndio wanaojishughulisha na Sekta ya kilimo ambapo Kundi kubwa la Vijana limejitumbukiza katika biashara ya Boda boda isiyo na hatma njema kwao.
Bwana Clifford alisema juhudi kubwa zimeanza kuchukuliwa na Serikali Kuu katika kuimarisha  miundombinu ya Sekta ya Kilimo sambamba na  upatikanaji wa zana bora na za kisasa za Kilimo zitakazowashawishi moja kwa moja Vijana kujiingiza katika Sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Morogoro alimfahamisha Balozi Seif  kwamba jitihada hizo ni pamoja na Tanzania kushirikiana  na Nchi za Vietnam na Ethiopia ziklizopiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao ya Mpunga ili kuendeleza Kilimo cha Mpunga maarufu Shadidi.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Jijini Dar es saam kuwajuilia haji Waziri wa Mali Asili na Utalii wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Khamid Kigwangala pamoja na Msanii Maarufu Afrika Mashariki Mzee Majuto {Maarufu King Majuto}.
Balozi Seif aliwaombea Dua Waziri Kigwangala apone haraka kufuatia mtihani wa ajali ya gari iliyomtokezea juzi Mkoani Arusha akielekea Mkoani Dodoma Kikazi na Mzee Majuto anayekabiliwa na Matatizo ya Mgongo kwa muda mrefu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wagonjwa hao kwamba mitihani iliyowafika ni kudra ya Muumba wao ambayo wanalazimika kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kizito kwao.
Alisema maradhi na ajali ni majaribu ya Mwenyezi Muungu aliyowaumbia Viumbe wake kuwaangalia endapo  watamshukuru au kumkufuru. Na hayo yaliyowapata wagonjwa hao ni miongoni mwa majaribu hayo ambapo wanapaswa kuyakubali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.