Habari za Punde

Hutuba ya Mkurugenzi Mundeshaji Wakati wa Uzinduzui wa Jengo la Treni Darajani (Chawl Building Darajani)leo 14 AGOSTI, 2018


Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Bi. Sabra Issa Machano akitowa maelezo ya Kitaalamu ya Ujenzi Mkubwa wa Jengo la Treni Darajani (Chawl Building Darajani)leo 14 AGOSTI, 2018

MHE.  RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI – DR. ALI MOHAMED SHEIN

MH. MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, BALOZI SEIF ALI IDDI

MHESHIMIWA JAJI MKUU WA ZANZIBAR, OMAR OTHMAN MAKUNGU,

MHE. SPIKA WA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZUBEIR ALI MAULID

MH. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, DKT KHALID SALUM MOHD

WAHESHIMIWA MAWAZIRI WA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

MHESHIMIWA  MKUU WA MKOA WA MJINI MAGHRIBI, AYOUB MOHAMMED MAHMOUD,

WAHESHIMIWA  WAKUU WA MIKOA.

WAHESHIMIWA WAWAKILISHI, WABUNGE NA 

VIONGOZI WOTE WA SERIKALI NA VYAMA VYA SIASA.

MAKATIBU WAKUU WA WIZARA ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR,

MWENYEKITI NA WAJUMBE WA BODI YA WADHAMINI YA MFUKO WA HIFADHI

WAKURUGENZI NA VIONGOZI WA SERIKALI

WAHESHIMIWA MABIBI NA MABWANA 

ASALAM ALEYKUM;

Awali ya yote napenda kuchukuwa nafasi hii adhimu  kumshukuru Allah Subhannahu Wataala  kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha  kushiriki katika sherehe hizi za uzinduzi rasmi wa Chawl Building au kama linavyofahamika na wengi “Jumba la Treni” baada ya matengenezo yaliyochukua takriban miezi ishirini  ikiwa ni sawa na mwaka mmoja na miezi minane.

Shukurani za pili zije kwako Mh.  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein kwa kukubali kwako kuwa  mgeni wetu rasmi wa shughuli  hii.  Tuna furaha kubwa  kuwa nawe kwani tunafahamu majukumu mazito na ratiba ngumu uliyo nayo ukiwa  ni Kiongozi  wetu na Mkuu wa  Nchi hii.  

Pia, nitoe shukurani zangu tena kwako kwa ushauri wako pamoja  na  maelekezo mbalimbali uliyotupatia, maelekezo ambayo lengo lake yalikuwa   katika kuhakikisha ZSSF inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio makubwa katika matengenezo haya,  ili ZSSF iweze kuchangia kwa kiasi katika kuleta maendeleo kwa nchi na wananchi wake. Lakini pia kwa kuwapatia wafanyabiashara mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao  baada ya kukamilika kwa matengenezo makubwa ya jengo mashuhuri la chawl (jumba la treni).

Shukurani nyengine ni kwa Makamo wa Rais wa Zanzibar Mh. Balozi Seif Ali Idd ambae mbali ya ushauri wake wenye dira lakini alikuwa nasi bega kwa bega tokea katika vikao mbalimbali lakini pia amefanya ziara kadhaa kuangalia hatua zinavyoendelea na kutupa ushauri wake ulioonesha ubobezi wake katika uongozi na maendeleo kwa ujumla, Shukurani Mh. Balozi Seif Ali Idd.

Mh. Mgeni Rasmi
Naomba  sasa kwa heshima na unyenyekevu mkubwa uniruhusu, nitoe taarifa fupi ya mradi huu wa jengo  la chawl maarufu kama jumba la treni.

Jengo la Chawl ambalo Shirika la UNESCO wanalitambua kama ni jengo la zamani ‘grade A’ awali lilijengwa na Sultan Barghash Mwaka 1880. Alilijenga ili lisaidie kukuza biashara katika mji huu lakini pia kusaidia kuchangia huduma za maji mji mkongwe lakini pia katika misikiti iliyowekwa wakfu katika mji huu kwa huduma mbalimbali.

Lilijengwa kwa kutumia boriti, mawe, udungo na chokaa na lilikuwa karibu na daraja lililounganisha sehemu mbili. Kutokana na kupitiwa na zaidi ya miaka mia moja jengo hili lianza kuchakaa.

Hata hivyo kutokana na umuhimu wake kijamii, kitalii na taswira yake katika mji mkongwe Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ilikabidhi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-Zanzibar jengo hili mnamo mwezi Juni 2016 ili kulifanyia matengenezo.

Awali, Kazi ya kulifanyia marekebisho ilikabidhiwa kwa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati chini ya usimamizi wa Shirika la Nyumba (ZHC) na Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe (STCDA) na hasa ukizingatia kuwa jengo hilo lipo ndani ya eneo la Mji Mkongwe na lina hadhi ya daraja la kwanza la uhifadhi wa kimataifa.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ulitakiwa kutoa fedha za mradi huo baada ya kuona kuwa mradi unaweza kujiendesha kibiashara na kukabidhiwa rasmi usimamizi wa mradi huo na umiliki wa jengo tarehe 6 Agosti 2015 kwa lease ya miaka sitini na sita (66), na kukabidhiwa rasmi Juni 2016 kuwa wamiliki wa jengo.

Mh Mgeni Rasmi
Kutokana na kuwa jengo hilo lilikuwa na wapangaji tofauti waliokuwa wakiishi  na wafanyabiashara katika milango mbalimbali ya maduka, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Kamati ya mawaziri watano walifanya kikao na wafanyabiashara hao na wakaazi kwa kuwafahamisha azma na  lengo la Serikali na kuwataka kuhama ili kupisha ukarabati, Pia ulazima wa wapangaji hao kuhama ulitokana na hali ya ubovu wa jengo wakati huo.

Hivyo, Wafanyabiashara hao walihama mnamo tarehe 5 Juni 2016 ili kupisha ujenzi wa jengo. Katika kufikia lengo la mradi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ulichukua hatua zifuatazo:-
·      Kuzungusha mabati eneo lote la mradi "hoarding" ili kuzuia wizi na uharibifu wa jengo pamoja na kuweka ulinzi wa kikosi cha Valantia.

·      Kutoa zabuni ya ushauri elekezi na kufanikiwa kuipata kampuni ya CONS AFRICA ya Dar-es-Salaam kuifanya kazi hiyo. Kampuni hiyo ilifanya kazi kwa karibu sana na Mamlaka ya Uhifadhi na uendelezaji wa mji mkongwe (STCDA) ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo na kuhakikisha kazi inaenda kwa mujibu wa taratibu na sheria za Mji Mkongwe.


·      Kushirikiana na Mamlaka ya Uhifadhi (STCDA) michoro iliochorwa na mshauri elekezi iliwasilishwa UNESCO kwa ajili ya kupata ridhaa ya ujenzi. UNESCO walitoa ridhaa ya kuendelea na ujenzi baada ya kufanya ziara katika mradi huo mwezi Oktoba 2017 [k1] pamoja na kutoa maelekezo machache ambayo mshauri na  mkandarasi aliyafanyia kazi.

·      Kutoa zabuni za mkandarasi mkuu (Main Contractor) na wakandarasi wadogo (Sub-Contractor), kampuni zilizofanikiwa kushinda kazi za ujenzi CRJE (EA) LTD – kama mkandarasi mkuu kwa gharama ya TZS 8.4 bilioni. CRJE (EA) LTD – pia akiwa mkandarasi mdogo wa huduma za maji safi, maji machafu na huduma za kujikinga na moto (Plumbing and Fire fighting) kwa gharama ya TZS 613,555,632. Gesap engineering group limited - mkandarasi mdogo wa huduma za Umeme (Electrical) kwa gharama ya TZS 984,374,998. Gesap engineering group limited - mkandarasi mdogo wa huduma za "ICT" kwa gharama ya TZS 292,908,332. Derm Elevators Limited - mkandarasi mdogo wa huduma za "Lifti" kwa gharama ya TZS 652,851,179. CITCC (Tanzania) Limited - mkandarasi mdogo wa huduma za "Air Condition" kwa gharama ya TZS 733,861,508 Gharama za mradi hadi kukamilika kwake zinatarajiwa kuwa ni TZS 11.8 bilioni

Mh Mgeni Rasmi
Kazi ya matengenezo ya jumba hili la treni ilianza rasmi tarehe 2, Novemba 2016 baada ya mkandarasi kukabidhiwa jengo. Kazi za mwanzo zilizofanyika ni kuliongezea umadhubuti jengo (strengthening of the building) kwa kulihami lisije likaanguka au kuleta madhara kabla na wakati wa ujenzi.
Hatua iliyofuata ni kuliezeka jengo kwa kutumia bati la Aluminium ambalo linastahamili upepo wa bahari tofauti na bati la kawaida na hivyo kukaa muda mrefu bila ya kuharibika na kufanya kutu.
Katika hali inavyoonekana sasa kazi ya ukarabati wa jengo ikiwa imekamilika ni pamoja na kuweka nguzo na bimu ili kuliongezea umadhubuti jengo na kuweza kubeba uzito mkubwa zaidi, kazi ya kurekebisha kuta zote, kutia plasta,  kupaka rangi ndani ya jengo, kufunga fremu mpya za milango na madirisha na kuweka dari "ceiling".

Ukarabati wa jengo pia ulihusisha kazi za kumalizia (finishing), ambapo kazi ya kutia rangi kuta za nje, kazi za kufunga miundombinu ya maji na umeme, uwekaji wa madirisha na milango, ufungaji wa ngazi, ujenzi wa mahodhi ya kuhifadhia maji safi, ujenzi wa mashimo ya maji machafu[k2]  (septic tank) ufungaji wa lifti na kupanda miti ya maua na majani katika eneo la bustani.
Mradi huu awali ulitarajiwa kukamilika ndani ya  kipindi cha miezi kumi na nane (18) ilipofikia  Mei 2018, ila badaa yake uliongezwa muda wa miezi miwili na kukamilka mwishi wa mwezi Julai, 2018.

Mh Mgeni Rasmi
Mradi huu wa kulifanyia matengenezo makubwa jumba la treni (Chawl Building) kwa kuliongezea ubora na haiba ya jengo hili umebadilisha kwa kiasi matumizi, ambapo Baada ya kukamilika kwake, jengo limekuwa na milango ya maduka 52, sehemu 2 za ATM, sehemu ya kuswalia wanawake, nyumba 10 za kuishi (2 za vyumba viwili na 8 za chumba kimoja) sehemu za ofisi, supermarket, sehemu ya kufanyia mazoezi (Gymnasium) na mkahawa (restaurant).
Mradi pia umezingatia uwepo wa watu wenye mahitaji maalum, hivyo umewekewa "ramp" itayowawezesha kufika katika ghorofa ya chini na pia umewekewa "lifti" ambayo itasaidia kuwafikisha katika ghorofa zilizobakia.
Mh. Mgeni Rasmi
Naomba ifahamike kwako kuwa Kampuni zote nilizozitaja zilipatikana kwa kuzingatia taratibu na sheria za manunuzi za Zanzibar kwa maana zilishindanishwa na kampuni nyingine kwa kuzingatia uzoefu, gharama na ubora wa kazi inayohitajika kufanywa.
Mh. Mgeni Rasmi
Uwekezaji huu wa ukarabati wa jengo la treni ni mkubwa kwa ZSSF na kukamilika kwake unaashiria kuanza kuingiza mapato, hivyo kutokana na uchambuzi uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa ZSSF, mradi huu utakuwa na tija kifedha, kiuchumi na kijamii. Kwa kuzingatia vyanzo vya mapato vilivyomo, ZSSF inatarajia mradi huu:

1. Utajilipa ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo.

2. Aidha, Serikali kupitia vyombo vyake vya kukusanya kodi itanufaika na biashara zitakazoendeshwa  na wananchi mbalimbali katika jengo hili ambalo imezikosa kwa muda.
3. Taasisi za Serikali kama Shirika la Umeme, Mamlaka ya maji wataweza kunufaika na mauzo ya  umeme na maji yenye kutumika katika jumba hili.
4. Nadhani pia mtakubaliana na mimi kuwa Haiba yake mpya itakuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii ambapo kila atayefika Unguja  hatakosa kutembelea hapa.
Mh. Mgeni rasmi
Matengenezo ya jumba hili ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, ambayo ni kuwatengenezea makaazi mazuri kama haya, pia kuwawekea mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao binafsi za kazi za kujitafutia riziki halali. Tunaimani kuwa chini ya uongozi wako mahiri na makini Rais wetu wa Zanzibar lakini pia ukiwa ni Makamo Mwenyekiti wa Chama tawala Serikali yetu itapindukia yale yote yaliyopangwa katika ilani hiyo hadi kufikia mwaka 2020.
Mh. Mgeni rasmi
Naomba nimalizie maelezo yangu mafupi kwa kukushukuru tena  Mh. Rais kwa busara na maelekezo yako yanayosaidia kutupa dira ya utekelezaji wa majukumu yetu. Mwisho napenda kuwashukuru   viongozi wangu kutoka  Wizara ya Fedha, Mwenyekiti na Bodi ya Wadhamini ya ZSSF,  Menejimenti na wafanyakazi wote wa ZSSF kwa mashirikiano na utendaji  wa kupigiwa mfano.
Lakini pia nimshukuru kwa kiasi kikubwa na kwa dhati kabisa Nd. Abdulwakil Haji Hafidh Mkurugenzi Mwendeshaji aliyestaafu ambaye taasisi yetu hii kwa mafanikio makubwa kabisa ikiwemo kuanzisha mradi huu.
“Wito kwa wadau na wananchi wote kwa ujumla ni tulitunze jengo letu kwani waswahili walisema kitunze kidumu”.

 “Maendeleo ya Zanzibar yataletwa na Wazanzibari wenyewe”

ZSSF OYEEE

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.