Habari za Punde

Mawaziri Waidhinisha Kuundwa Kwa Baraza la Taifa la Kiswahili Nchini Kenya

Baraza la Mawaziri nchini Kenya limeidhinisha kubuniwa kwa Baraza la Taifa la Kiswahili ambalo litatwikwa jukumu la kukuza na kuendeleza lugha hiyo nchini humo.
Pendekezo hilo linafuata kipengee 137 cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambacho kinasema kwamba lugha ya Kiswahili itaimarishwa, kukuzwa na kutumika kama lugha ya Jumuiya hii.
Baraza hilo litatumika kutoa ushauri, na vile vile kuimarisha maongozi ya serikali kuhusiana na kukuza, kulinda na kuunga mkono matumizi ya lugha ya Kiswahili na kushirikisha kazi ya mashirika ya kitaifa, kandaa hii, kitamaduni, mashirika ya elimu na mashirika mengine yanayohusika na lugha ya Kiswahili.
Wasomi wa Kiswahili na wadau wengine wamekuwa wakihimiza kuundwa kwa baraza hilo kwa muda mrefu.
Prof Hezron Mogambi ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema hatua hiyo ni ya kupongezwa sana.
"Tumekuwa tukiingoja kwa muda mrefu kwa sababu maendeleo na makuzi ya Kiswahili yamekuwa yakikwazwa kwa sababu ya kukosa baraza kama hili. Matumizi sawa ya Kiswahili yamepigwa jeki," amesema.

Kutetea hadhi ya Kiswahili

Miongoni mwa mwengine, anasema baraza hilo litasaidia sana katika kuhakikisha kuwa hadhi ya Kiswahili kama lugha rasmi na ya taifa nchini Kenya na kwamba lugha hiyo "inazingatiwa na kuheshimiwa."
"Kwa sasa hakuna chombo cha kufanya hivyo. Kiswahili kimekuwa kikitumiwa nchini Kenya katika hafla na shughuli mbalimbali kwa njia isiyofaa. Hakuna wa kukosoa na kuelekeza. Matumizi sawa na upotoshaji utazuiwa kwa kuwa na chombo cha kufanya kazi hii," anasema.
Prof Mogambi anaeleza kuwa kutokana na kutukuwepo kwa baraza hilo, kumekuwa na vitabu vingi ambavyo vimechapishwa kiholela bila kufuata viwango bora vya lugha na vimekuwa changamoto kuu katika kuendeleza lugha ya Kiswahili.
"Hii ni pamoja na vitabu vya shule na vile vya kiada. Uchunguzi na urekebishaji wa maandishi kama haya pamoja na mengine yanaweza tu kurekebishwa na kuhakikishiwa ubora baraza la Kiswahili litakapokuwepo," anasema.
Aidha, anasema baraza hilo litasaidia taaluma ya tafsiri na ukalimani kwa kuwa "kuna matini nyingi sana ikiwemo stakabadhi za serikali, za watu binafsi, mashirika ya ndani ya nchi na ya kimataifa ambazo zahitaji kutafsiriwa. Huduma kama hii itasaidiwa sana na kusawazishwa kimsamiati na barala la Kiswahili."
Mhadhiri na msomi wa lugha ya Kiswahili Hezekiel Gikambi amesema: "Kuanzishwa kwa Baraza la Kiswahili Kenya hata kulikuwa kumechelewa. Tanzania wana Bakita kwa muda Mrefu. Ni hatua nzuri katika kusaidia Kiswahili kukita mizizi kama lugha rasmi nchini Kenya na pia kukidhi hitaji la Jumuiya ya EAC kifungu 137."
"Tunatumai wabunge watagundua hilo wapitishe haraka na wataalamu wa Kiswahili wapate kazi katika Baraza hilo. Kitakuwa chombo rasmi cha kukuza Kiswahili nchini."
Kwa muda mrefu, wasomi wa Kiswahili wamekuwa wakitegemea taasisi na vyama vya Kiswahili ambavyo si za serikali kukusanyika pamoja na kujadili masuala ya lugha.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akionyesha Kamusi Kuu ya Kiswahili baada ya kuizindua kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Juni 19, 2017.
Miongoni mwa vyama hivyo ni Chama cha Kiswahili cha Taifa (Chakita) kilichoanzishwa mwaka 1998 na Prof Kimani Njogu.
Kuna pia Chama Cha Waandishi wa Kiswahili wa Taifa Leo (WAKITA) ambacho huwaleta pamoja wadau wa gazeti la pekee la Kiswahili nchini humo Taifa Leo linalochapishwa na kampuni ya Nation Media group. (Wakita ya Kenya ni tofauti na Wafia Kiswahili Tanzania na Watetezi wa Kiswahili Tanzania)

Baraza la Tanzania

Tanzania imekuwa na Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania kwa kifupi (Bakita) ambacho ni chombo cha serikali chini ya wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Baraza hilo liliundwa na sheria ya bunge ya mwaka 1967 kwa lengo la kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahili hasa ndani ya Tanzania. Katika marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanyika mwaka 1983 Bakita ilipewa uwezo wa kufuatilia na kusaidia ukuzaji wa Kiswahili katika nchi za nje pia.
Mwaka 2015 Bakita ilifanikisha mradi wa kutunga kamusi mpya iliyoitwa Kamusi Kuu ya Kiswahili.
Kamusi hiyo ilikusanya maneno mengi makuu, yaani vidahizo, kuliko kamusi zilizotangulia na kufikia mwaka jana ilikuwa ina maneno 45,500.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.