Habari za Punde

Mo Salah achunguzwa kwa sababu ya video yake akiwa bado anaendesha gari akitumia simu

Mshambuliaji wa Liverpool raia wa Misri Mohamed Salah anachunguzwa na polisi baada ya video yake kuibuka akionekana kuendesha gari akiwa bado anatumia simu.
Klabu yake inadaiwa kuwa ndiyo iliyopiga simu kwa polisi.
Polisi wa Merseyside wamethibitisha kupitia ujumbe wa Twitter kwamba video hiyo imekabidhiwa kitengo husika.
Msemaji wa Liverpool amesema waliwafahamisha polisi kuhusu video hiyo baada ya kuzungumza na mchezaji huyo.
Ameongeza kwamba hatua zozote zinazohitajia kuchukuliwa kuhusu tukio hilo zitachukuliwa kwa kufuata mifumo ya ndani.
Video hiyo ambayo imesambazwa sana kwenye Twitter inaonekana kumuonesha mchezaji huyo, akiwa anatumia simu yake akiwa amelisimamisha kwa muda huku akiwa amezingirwa na mashabiki, wakiwemo watoto. Kisha analingurumisha gari na kundoka akiwa bado anaitumia simu yake.
Msemaji wa klabu hiyo amesema: "Klabu, baada ya kushauriana na mchezaji, imewafahamisha Polisi wa Merseyside kuhusu kanda hiyo ya video na matukio yaliyokuwa yanaendelea wakati wa kupigwa kwa video hiyo."
"Tumezungumza na mchezaji huyo na tutashughulikia hatua nyingine zozote zinazohitajika kuchukuliwa kwa kutumia mifumo ya ndani.
"Hakuna yeyote kati ya klabu na mchezaji ambaye atatoa taarifa zaidi kuhusu tukio hili."
Raia huyo wa Misri aliwafungia Liverpool magoli 44 msimu uliopita.
Mo Salah alifunga bao Jumapili katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu huu ambapo aliwasaidia Liverpool kuwalaza West Ham 4-0.
Mabao hayo mengine yalifungwa na Sadio Mane (mawili) na Daniel Sturridge.

Mzozo kuhusu picha

Wakati wa Kombe la Dunia nchini Urusi, kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov alidaiwa kumtumia Mohamed Salah kujinufaisha kisiasa baada ya kupigwa picha na nyota huyo raia wa Misri, kwa mujibu wa mkuu wa shirika linalopambana na ubaguzi duniani.
Kikosi cha Misri kilikuwa katika jamhuri hiyo ya zamani iliyokuwa chini ya Urusi zamani na ambayo imeathiriwa sana na vita kwa maandalizi ya michuano hiyo.
Utawala wa kiongozi wa jamhuri hiyo Kasyrov umelaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu.
Piara Power kutoka Fare Network alisema Fifa ilifanya makosa makubwa kuruhusu Chechnya kuwa kambi ya kufanyia mazoezi.
Kadyrov alitetea rekodi yake ya haki za binadamu alipofanya mahojiano na BBC mapema mwaka huu.
Akizungumza mwezi Januari alisisitiza kuwa ripoti kuhusu mauaji ya kiholela na mateso dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Chechnya ilibuniwa.
Shirikisho la kandanda duniani Fifa limekuwa likijitetea kila wakati kuwa linalinda haki za binadamu.
"Kama unamjua Kadyrov na unafuatilia vile anaongoza eneo hilo, basi wakati fulani unaweza kujua kuwa anajaribu kujinufaisha kisiasa, na ninafikiri amefanya hivyo (kwa picha yake na Mo Salah)."
Amnesty International walisema picha hiyo na Salah ilikuwa na manufaa ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.