Habari za Punde

NEC yatangaza Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata 21


Na.Hussein Makame, NEC

Tume ya Taifa ya 

Uchaguzi (NEC) 

imetangaza Uchaguzi 

Mdogo wa Udiwani 

katika kata 21 za 

mikoa 10 ya Tanzania 

Bara utakaofanyika 

tarehe 16 Septemba mwaka huu.

Akitoa taarifa ya uchaguzi huo jijini Dar es Salaam leo, 

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. 

Athumani Kihamia, alisema fomu za uteuzi wa wagombea wa 

uchaguzi huo zitatolewa kati ya tarehe 17 hadi 23 Agosti 

mwaka huu.

Aliongeza kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 23 

Agosti wakati kampeni za Uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 

24 Agosti hadi tarehe 15 Septemba mwaka huu.

Dkt. Kihamia alisema kuwa Tume imetangaza uchaguzi huo 

baada ya kupokea taarifa ya uwepo nafasi wazi za udiwani 

katika kata hizo 21 zilizopo katika Halmashauri 15 kutoka 

kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.

“Nafasi wazi za udiwani katika Kata hizo zimetokana na 

sababu mbalimbali zikiwepo kifo, kujiuzulu, kutohudhuria 

vikao na kufutwa uanachama” alisema Dkt. Kihamia na 

kuongeza kuwa;

“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti 

ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za 

Mitaa; Tume ina utaarifu Umma kuhusu kuwepo kwa 

Uchaguzi mdogo katika Kata hizo 21.”

Kufuatia taarifa hiyo, Dkt. Kihamia alitoa mwaliko wa Tume 

kwa vyama vya siasa, wadau wote wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.

“Tume inachukua fursa hii kuviasa vyama vya siasa na 

wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015” alisema Dkt. Kihamia.

Aidha alivitaka vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi 

kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na 

Madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote 

yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa 

Uchaguzi mdogo.

Uchaguzi huu mdogo wa udiwani katika kata 21 unatarajiwa 

kufanyika sanjari na uchaguzi mdogo wa ubunge katika 

majimbo ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli na kata za 

Tindabuligi na Kisesa katika Halmashauri ya Wilayani 

Meatu, uliotangazwa juzi ambao utakaofanyika siku ya 

Jumapili tarehe 16 Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.