Habari za Punde

TANZANIA YANG'ARA KUANDAA KONGAMANO LA WATAALAMU WA MAGONJWA YA DAMU (HAEMATOLOGY) BARA LA AFRIKA

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu (Haematology), MUHAS Prof. Julie Makani (kulia) akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio ya kongamano la kwanza la wataalam wa magonjwa ya damu (Haematology) linalokutanisha watalaam wa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla. Pembeni yake ni Msimamizi wa Mafunzo hayo Prof. Lucio Luzzatto. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Msimamizi wa Mafunzo ya Wataalam wa magonjwa ya damu (Haematology) Prof. Lucio Luzzatto akionyesha chembe chembe zinazosababisha upungufu wa tamu mwilini wakati wakizungumza na wanahabari jijini  Dar es Salaam.
  Wataalam wa magonjwa ya damu (Haematology) kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo bara la Afrika wakiwa katika sherehe ya kukaribishwa nchini Tanzania.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Tanzania yang'ara kwa nchi za Afrika kwa kuwa nchi pekee ya kwanza kuandaa kongamano linalowakutanisha wataalam wa magonjwa ya damu (Haematology) kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Hayo yamezungumzwa na jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu (Haematology), MUHAS Prof. Julie Makani wakati akielezea mafanikio ya  kongamano la wataalam wa magonjwa ya damu (Haematology) linalokutanisha watalaam wa Tanzania na mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Bara la Afrika.

"Nitoe pongezi kwa serikali na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya afya na ndiyo maana kila kukicha kunakuwa na mabadiliko yanayopelekea kutokea matokeo chanya, wagonjwa badala ya kukimbilia nje ya nchi wanapata matibabu ndani" amesema Prof. Makani. 

Kongamano hilo lililoandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Mfuko wa Kimataifa kusaidia masuala ya elimu Menarini (Fondazione Internazionale Menarini) la nchini Italia, ambalo limeweza kuwakutanisha madaktari bingwa ikiwemo watoa huduma ya magonjwa ya damu (Haematology) takribani nchi zipatazo 15 barani Afrika wanaojadili changamoto wanazokumbana wakati wa utoaji wa huduma ya magonjwa ya damu (Haematology).

Aidha Prof. Makani amesema kuwa mpaka sasa Tanzania imeweza kujitahidi kufanya jitihada za kipekee katika utoaji wa huduma japo changamoto inayowakumba ni uhaba wa wataalam zaidi wanaopenda kusomea utoaji wa huduma ya magonjwa ya damu (Haematology).

Nae Msimamizi wa Mafunzo hayo Prof. Lucio Luzzatto amesema kuwa ni vyema Tanzania ikajivunia bahati iliyopata kwa kuweza kuwapa mafunzo watalaam wengi zaidi ili kuweza kuondokana na tatizo la magonjwa ya damu (Haematology) na kumekuwa na muitikio mkubwa wa kupokea mafunzo hayo.

Ameongeza kuwa Tanzania ndiyo itakuwa ikiandaa Kongamano hilo kila mwaka huku wakiongeza ushiriki wa nchi toka bara la Afrika ili kuweza kusambaza elimu hiyo zaidi.

"Tutawafundisha njia za bora ya kutoa tiba ya kisasa kwa magonjwa ya damu na hata kuanzisha tiba hiyo sehemu zao walizotoka ili kuweza kupunguza idadi ya wagonjwa wengi ambao wanaokimbilia kupata huduma hiyo hospitali kubwa," amesema. Nchi zinazoshiriki Kongamano hilo kutoka bara la Afrika ni Tanzania ambao ndiyo wenyezi, Uganda, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Ivory coast, Swaziland, DRC, Madagascar, Ghana, Ethiopia pamoja na Burkinafaso.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.