Habari za Punde

Upatikanaji wa Dawa Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ni Asilimia 94 Kwa Wananchi wa Wilaya Hiyo.

 
 Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kakunyu, Auston Martin (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kuangalia taratibu za usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera jana. Kulia ni Mwanahabari Peter Saramba.
 Meneja wa MSD Kituo cha Muleba, Egidius Rwezaura, akikagua dawa katika stoo ya kuhifadhi dawa ya zahanati hiyo ya Kakunyu. Kushoto ni Muuguzi Msaidizi wa zahanati hiyo, Devotha Kamugisha.
Majengo ya Zahanati ya Kata ya Kakunyu.


Na Dotto Mwaibale, Kagera
Kupatikana kwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa wakati kwenye vituo vya afya nchini kunasaidia sana kupunguza malalamiko ya wananchi na kudhibiti magonjwa ambayo yanaweza kuzaa usugu kwa wagonjwa kutopata dawa kwa wakati. 

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kakunyu, Auston Martin, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kuangalia taratibu za usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera.

"Kupatikana kwa dawa muhimu kwa wakati katika zahanati yetu kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa mawili makubwa ya malaria na yale ya zinaa yaliyokuwa yanasumbua eneo hili kwa muda mrefu" alisema Martin

Dkt. Martin alisema kwamba hivi sasa dawa wanazozipata kutoka MSD zinapatikana kwa asilimia 94 ukilinganisha na awali, hivyo kuwa faraja kwa wananchi wanao pata huduma za matibabu katika zahanati hiyo.

Alitaja magonjwa ya zinaa yanayosumbua katika eneo hilo kuwa ni kaswende na kisonono na hali hiyo inasababishwa na wananchi kuona aibu kwenda kuchukua mipira ya kiume (kondomu) na uelewa mdogo kuhusu matumizi ya mipira hiyo, hivyo wanaangalia utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupata zana hiyo kwa njia itakayokuwa rahisi kwao kuzipata.

Martin alitaja sababu nyingine kuwa ni muingiliano wa watu kutoka nchi jirani ya Uganda Wilaya ya Usingilo na wanaume wengi kutofanyiwa tohara ambapo tayari Mashirika ya nje ya nchi yanayojishughulisha na masuala ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi (MDH) yameanzisha  kampeni  ya utoaji wa tohara kuanzia watoto wenye umri wa miaka 10 hadi watu wazima.

Dk. Martin alisema pamoja na kupungua kwa magonjwa hayo changamoto nyingine ni maambukizi ya virusi vya UKIMWI, HIV ambapo katika zahanati hiyo ina wananchi 21 wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wanapatiwa huduma katika kliniki za kudhibiti makali ya virusi vya UKIMWI ya mama na mtoto.

Alisema katika zahanati hiyo kwa mwezi wanahudumiwa wagonjwa 200 kutoka katika vitongoji vinne vya Kitoboka, Nsheshe, Kakunyu na Kalola.

Meneja wa MSD Kituo cha Muleba,Egidius Rwezaura alisema wana mpango wa kuanzisha  utaratibu wa kupeleka dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali kila baada ya miezi miwili badala ya miezi mitatu kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya dawa na MSD tayari imeongeza idadi ya magari ya usambazaji pamoja na kuajiri madereva wa kutosha.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.