Habari za Punde

Watendaji Tume ya maadili ya viongozi wa Umma watakiwa na nidhamu na udilifu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman akizungumza na Uongozi na Wafanyakazi wa Tume ya Maadili ya Viongozi Zanzibar wakati wa ziara yake kutembelea Idara zilioko katika Wizara yake. akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo na Watendaji wa Tume hiyo.


Na. Raya Hamad (OR.KSUUUB)
Watendaji wa Tume ya maadili ya viongozi wa Umma wametakiwa kuendeleza  uaminifu wenye  nidhamu na uadilifu katika kutekeleza majukumu ya kazi zao kama Serikali ilivyowaamini  kuwakabidhi majukumu hayo.

Hayo yameelezwa na Waziri wanchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala bora Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman wakati alipofanya mazungumzo na viongozi pamoja na watendaji wa Tume ya maadili ya viongozi wa Umma Waziri Haroun amesema nchi haiwezi kuwa na Taifa lenye  heshima na nidhaamu bila kuwepo na maadili hivyo utunzaji  wa siri ni muhimu hasa kwa chombo kinachoaminiwa kama Tume ya maadili ya viongozi wa Umma “ haitapendeza  kuona siri za viongozi  wa serikali zinatoka nje ama kusambaa kinyume na utaratibu ”alisisitiza Haroun.

Aidha Haroun  amesisitiza kuwa  mjenga nchi ni mwananchi hivyo amewataka watendaji hao kuwa na  ari  na bidii ya kujituma ili kufikia malengo waliyojipangia  wakiamini kuwa hakuna  atakaekuja kujenga Taifa lao bila ya kuanza wao wazalendo na wengine hufuatia .

Nae Katibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Ndugu Kubingwa Mashaka Simba amesema Tume inajukumu la kupokea , kusajili na kuhakiki tamko la mali na madeni kutoka kwa viongozi wa Umma , kupokea malalamiko na kufanya uchunguzi wa tuhuma za uvunjaji wa Sheria ya maadili ya Viongozi wa umma na kutoa elimu kwa umma na viongozi kuhusu umuhimu wa kuimarisha maadili Kutoa ushauri, maelekezo na miongozo kuhusiana na maadili ya viongozi  wa umma  ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa za mali na madeni ya viongozi wa umma 

Hata hivyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 imepokea na kusajili jumla ya fomu za taarifa za mali na madeni za viongozi wa umma 1,631 sawa na asilimia 99 ya shabaha iliyopangwa ya kupokea fomu za tamko la mali na madeni.

Kubingwa amesema kuwa Tume inaendelea kutoa elimu kwa viongozi ili kujiepusha na matendo ya ukiukwaji wa maadili na kuwakumbusha viongozi wa umma juu ya umuhimu wa kukuza maadili na kuongeza kasi ya kuwatumikia wananchi ili kufikia malengo ya kitaifa na umuhimu wa kuimarisha maadili.

Jumla ya mikutano 37 iliyowashirikisha viongozi wa umma kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na kamati za masheha imefanyika Unguja na Pemba , mikutano na mabaraza ya vijana katika Mkoa wa Mjini Magharibi uliowashirikisha viongozi wa mabaraza 150 ili kukuza uelewa wa vijana ili kukuza uwelewa wa vijana juu ya majukumu ya Tume na 
kuwaandaa vijana hao kimaadili ili wawe viongozi wazuri wa baadae.

Katika kukabiliana na baadhi ya changamoto  Tume imeendelea na jitihada ya kuishajihisha jamii ili kuwa na uwelewa wa kutosha kuhusu Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma  kwani bado wapo baadhi ya wanajamii hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu yake, aidha Tume inaendelea kushirikiana na Idara ya Serikali mtandao ili kupata mfumo imara na salama wa elektronik utakaoweza kutunza taarifa hizo.

Tume ya maadili ya Viongozi wa Umma imeanzishwa chini ya sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma, Nambari 4 ya mwaka 2015 na kuanza kazi rasmi mwezi April 2016

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.