Habari za Punde

Katibu NEC: Maafisa habari wana dhamana kubwa

Na Mwashungi Tahir        Maelezo    

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC , Idara ya Itikadi na Uenezi Chama  Cha Mapinduzi  Zanzibar  Catherina Peter Nao  alisema maafisa habari wana dhamana kubwa ya kusambaza habari kwa jamii katika taasisi wanazozifanyia kazi.

Hayo aliyasema leo  Katika ukumbi wa Wizara ya Habari Kikwajuni alipokuwa akizungumza na maafisa wa habari wa Mawizara, Maidara na Taasisi za Serikali kuhusu majukumu wanayotakiwa kuyatekeleza katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Alisema suala la kufikisha taarifa kwa wananchi juu ya maendeleo yanayotekelezwa na Serikalini ni kitu cha msingi na moja kati ya haki yao ya msingi  na waliopewa jukumu hilo ni pamoja na maafisa habari.

Aliwataka maafisa habari kujenga mashirikiano na viongozi wa juu Serikalini wakiwemo Mawaziri na Makatibu wakuu ili taarifa za taasisi zao zitangazwe na wananchi waweze kuzielewa.

Pia aliwataka Mawaziri mambo wanayoyafanya katika Mawizara yao yasikike kwa wananchi taarifa ziende hewani ili waweze kutambua Serikali jinsi inavyofanya juhudi katika mambo ya maendeleo .

Vile vile alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DKT Ali Mohammed Shein anatekeleza majukumu yake katika kutekeleza ilani  kwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo maji safi na salama , kuimarisha miundombinu , kutangaza elimu bure, matibabu bure na kusambaza huduma ya umeme mijini na vijijini na mambo mengi yanayohusu jamii.

“ Chama cha Mapinduzi kiko madarakani hivyo yawepo mashirikiano kwa kushikamana katika kutekeleza ilani na majukumu yake kwa ujumla na wananchi waendelee kufaidika”.Alisema katibu huyo.
Pia aliwataka maofisa wa habari wabadilike  na kuwa na tabia ya kuhudhuria kwenye mikutano ya CCM kwa dhamira ya kujenga na kumsaidia Rais Shein katika kutekeleza majukumu, pia ameweza kuwalipa wazee Pencheni wote bila kujali wanatoka chama gani  kaweka wazi kwa kila mzee anayefikia miaka 70 haya yote ni mafanikio kupitia serikali  hiyo .

Nae  Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Daudi Ismail Juma alisema lengo la mkutano huo ni kuongeza mwamko kwa wananchi kuelewa juhudi zinazochukuliwa na  Serikali kupitia maafisa wa habari.
Sambamba na hayo Mkurugenzi wa  mawasiliano Ikulu Hassan Khatib Hassan  aliwataka maofisa wa habari  kuwa na mashirikiano katika utendaji wa kazi kwani juhudi zinazochukuliwa na CCM ni kubwa sana na wananchi wana haki ya kujua maendeleo yanayofanyika katika nchi yao .
Aidha alisema wananchi wanayo haki kutoa maoni yao na kuweza kufanyiwa kazi kwani Serikali ipo kwa ajili yao katika kutatua matatizo yote yanayowakabili na Mh Rais yuko makini katika kusikiliza matatizo ya wananchi wake na kuyafanyia kazi ikiwemo huduma zote za jamii.
Mwisho.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.