Baadhi ya Timu ya Madaktari Wazalendo Wanaoishi Nchini Marekani kutoka Taasisi ya Afya Elimu na Maendeleo (Head Inc) wakimsikiliza Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed wakati wa mkutano wao wa kujitambulisha walipowasili Zanzibar.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongeza juhudi za
makusudi zinazochukuliwa na Wanadiaspora katika kuiunga mkono nchi yao ya asili
katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.
Pongezi hizo
zimetolewa na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu
pamoja na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed Ikulu mjini Zanzibar wakati
walipofanya mazungumzo na Timu ya Madaktari Wazalendo waishio Marekani kutoka
Taasisi ya Afya, Elimu na Maendeleo (Head Inc).
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa pongezi
kwa Timu hiyo kwa uwamuzi wake wa kuja Zanzibar kwa lengo la kutoa huduma za
afya kazi ambayo wameifanya kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Waziri Gavu alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana mchango wa Wanadiaspora
hao ambao wameonesha uzalendo wa hali ya juu katika kutoa huduma za afya kwa
kuwahudumia wananchi waliotoka katika maeneo kadhaa ya hapa Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Waziri Gavu alisisitiza kuwa huduma zilizotolewa na Timu hiyo yenye makao makuu
yake nchini Marekani zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ambapo wananchi walio
wengi walipata fursa ya kuangalia afya zao na kupata tiba.
Aliongeza kuwa juhudi
zaidi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu ya
sekta hiyo, vifaatiba, rasilimali watu na mambo mengineyo.
Mapema Waziri wa Afya
Hamad Rashid Mohamed alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza
ushirikiano wake na Wanadiaspora hao kutoka Taasisi hiyo ambao wamejitolea
kuwasaidia ndugu zao na kulisaidia Taifa lao.
Alieleza kuwa ni
faraja kubwa kwa kufikiwa na Madaktari hao ambao miongoni mwao wamo Madaktari
Bingwa wa maradhi mbali mbali ambao walipata fursa ya kutoa huduma za afya kwa
wananchi waliotoka maeneo mbalimbali katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja
ambapo walitumia Hospitali ya Makunduchi na Hospitali ya Kivunge kama ni vituo
kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Katika maelezo yake,
Waziri Hamad alieleza juhudi zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya Unguja na
Pemba.
Waziri Hamad alitumia
fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein kwa juhudi kubwa anazochukua katika kuhakikisha sekta ya afya
inaimarika ikiwa ni pamoja na kuongezwa kwa Bajeti ya Wizara hiyo.
Hivyo, Waziri Hamad
alieleza kuwa kujitokeza kwa Madaktari hao na kuja Zanzibar kuunga mkono juhudi
hizo za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein ni
jambo la busara katika kuwapatia huduma za afya wananchi wote wa Zanzibar.
Alitumia fursa hiyo
kueleza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa bure kama ilivyoelekezwa na
Serikali hatua ambayo imeweza kuwasaidia wananchi walio wengi wakiwemo wasiokuwa
na uwezo.
Aidha, Waziri Hamad
alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kutatua changamoto kadhaa
katika sekta hiyo huku akisisitiza kuwa elimu ya afya kwa wananchi itaendelea
kutolewa ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Waziri Hamadi akitumia
fursa hiyo kuwakaribisha Wanadiaspora wa Taasisi hiyo ya Afya, Elimu na
Maendeleo (Head Inc) kuja kuekeza katika sekta ya afya hapa Zanzibar.
Nao Madaktari kutoka
Taasisi hiyo walipata fursa kueleza jinsi walivyotoa huduma za afya zikiwemo
tiba pamoja na elimu ya afya kwa wananchi katika hospitali walizofika huku
wakipongeza jinsi mapokezi makubwa waliyoyapata hatua ambayo imepelekea kufanya
shughuli zao za kutoa huduma za afya kwa ufanisi mkubwa.
Sambamba na hayo,
Madaktari hao walizipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inazozichukua katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ambapo
walieleza katika huduma zao zote walizozitoa hakupatikana hata mwananchi mmoja
aliepata maambukizi.
Pia, Madaktari hao
walipongeza hatua za Serikali katika kupamabana na maradhi ya Malaria ambapo
Zanzibar imepata mafanikio makubwa ikilinganishwa na nchi nyingi za Bara la
Afrika huku wakiahidi kutoa vifaa tiba kwa wananchi wa Zanzibar.
Madaktari hao pia,
walisisitiza haja ya kuchukua tahadhari zaidi kutokana na kuwepo kwa ongezeko la maradhi yasiokuwa ya
kuambukiza hasa shinikizo la damu na kisukari hiyo ni kutokana na wananchi
waliowengi kuonekana kuwa na dalili za maradhi hayo baada ya uchunguzi
waliofanya.
Pamoja na hayo,
Madaktari hao walieleza haja ya kuendelea kutolewa elimu ya afya kwa wananchi
wa Zanzibar hasa wanaoishi vijijini. Katika Taasisi hiyo pia, wamo Madaktari kutoka
nchini Lesotho ambao walishirikiana pamoja na Wanadiaspora hao.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment