Habari za Punde

Tamasha la kwanza la Urithi wa Utamaduni wa Mtanzania–Zanzibar kuzinduliwa leo

Tamasha la kwanza la Urithi wa Utamaduni wa Mtanzania–Zanzibar litazinduliwa leo saa 8:00 mchana katika Viwanja vya Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Tamasha hilo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Mh. Mohamed Aboud Mohamed.

Tamasha hilo litaendelea kufanyika katika Viwanja hivyo hadi September 30 kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi saa tano usiku.

Viongozi mbali mbali watashiriki Tamasha hilo wakiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa ya Zanzibar.

Katika tamasha hilo kutakuwa na Shughuli mbali mbali za kiutamaduni ikiwemo Burudani mbalimbali kama vile Taarab asilia ya kikundi cha Malindi (Nad-Ikhwan Swafaa), Culture Musical Club,  Maulid ya Homu na Ngoma ya Kidumbaki.

Shughuli zengine ni pamoja Utenzi, Vyakula vya asili na Paredi ya Wasanii.

Aidha kutakuwa na Michezo ya Watoto ikiwemo Ngonjera, Hadi Mfundo, Foliti, Mbio za vikwazo, Ngoma za watoto, Maigizo, Kuvuta kamba, Mbio za mbatata na Mdako.

Tamasha hilo pia litatoa fursa kwa Viongozi kutoa nasaha zao kwa lengo la kutunza na kuenzi Urithi na Utamaduni wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.  

Imetolewa na :-

Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar
25, Septemba  , 2018

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.