Habari za Punde

WAZIRI MKUU AONGOZA MAELFU YA WAOMBOLEZAJI KWENYE MAZISHI KISIWANI UKARA

Baadhi ya Masanduku yenye miili ya Marehemu waliofariki kufuatia kivuko  cha MV Nyerere kupinduka na kuzama.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya waombolezaji na wakazi wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na mkoa jirani wa Mara katika mazishi ya kitaifa ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya MV Nyerere Septemba 20, mwaka huu. 

Waziri Mkuu ambaye ameongoza mazishi hayo leo (Jumapili, Septemba 23, 2018) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amewataka Watanzania waiache Serikali na vyombo vya dola viendelee kufanya kazi yake. 

"Wito wa Serikali kwenu wote, ni kuwasihi tushikamane na wenzetu waliopoteza ndugu zao, wakiwemo wazazi, kaka, dada na watoto. Ninaomba tuiache Serikali na vyombo vya dola viendelee kufanya kazi yake. Tuendelee kuwa wavumilivu,” amesema. 

Akiwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Magufuli mbele ya wafiwa na waombolezaji, Waziri Mkuu amesema: 

“Mheshimiwa Rais alipokea tukio hili kwa mshtuko mkubwa na anawapa pole sana wafiwa wote pia anawaombea majeruhi wote wapate ahueni mapema.” 

Amesema jumla ya watu 224 walipoteza maisha kutokana na ajali hiyo. Kati ya hao, miili 214 kati ya 219 iliyotambuliwa, ilichukuliwa na ndugu zao. Miili minne haikuweza kutambuliwa lakini ipo miili mitano ambayo ilitambuliwa na ndugu zao na hao ndugu wakaona ni vema wazikwe hapa eneo la tukio. Kwa hiyo leo tutawazika ndugu zetu tisa katika eneo hili,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua ya kuunda tume ya uchunguzi na kuahidi kwamba tume hiyo itatangazwa wakati wowote. 

“Tume ikikamilisha kazi yake, wote watakaobainika kuwa wamehusika watachukuliwa hatua mara moja,” amesema. 

Ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililopo, Waziri Mkuu amesema meli ya MV Nyehunge imeanza kutoa huduma ya usafiri wa muda badala ya MV Nyerere iliyokuwa ikitoa huduma kati ya bandari ndogo ya Bugolora, Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara. 

Amesema jitihada za kuivuta meli ya MV Nyerere iliyopinduka zinaendelea na kwamba maafisa wote wanaohusika na usafiri wa majini ambao walizembea kwenye suala hilo, wamekamatwa na wameanza kuhojiwa. 

Akigusia chanzo cha ajali hiyo, Waziri Mkuu amesema inasadikiwa kivuko cha MV Nyerere kilibeba mizigo mingi kuliko uwezo wake ambao ni wa kubeba tani 25 za mizigo, magari matatu na abiria 101. 

“Hadi sasa inaonesha kulikuwa na watu zaidi ya 260, yaani 41 waliookolewa na 224 waliopoteza maisha,” amesema. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote wa Ukara waliojitokeza kusaidia kazi ya uokoaji tangu ajali hiyo ilipotokea. Pia aliwashukuru wote waliotoa michango mbalimbali, watumishi wa hospitali za Bugando, Sekou Toure, Ukerewe, kituo cha afya cha Bwisya na timu nzima inayofanya kazi ya uokoaji na uopoaji wa miili kwa kazi kubwa waliyoifanya. 

Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama ametangaza namba ya tigopesa ambayo wananchi wanaweza kuitumia kutuma michango yao kwa ajili ya waliopatwa na maafa hayo. 

“Tumefungua akaunti ya maafa kwenye Benki ya NMB tawi la Kenyatta lakini ili kurahisisha upokeaji wa michango kutoka kwa wananchi wa kawaida, tumesajili namba ya tigo yenye namba 0677-030-000 kwa jina la RAS Mwanza. Naomba wale wasioweza kwenda benki watumie namba hiyo,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama   katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bwisa  kisiwani Ukara

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bwisa  kisiwani Ukara

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhusu juhudi zinazofanywa  na wahandishi za kukivuta kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati aliposhiriki katika mazishi ya wananchi waliokufa katika ajali ya kivuko hicho kwenye kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati alipowasili katika kijiji cha Bwasa kwenye  kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe kushiriki katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere, Septemba 23, 2018.

Askari wakiweka kaburini miili ya baadhi ya  wananchi waliofariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama kwenye  kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati wa mazishi yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kijiji cha Bwisa kisiwani Bukara, Septemba 23, 2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula na viongozi wengine walioshiriki katika mazishi ya  baadhi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya meli ya MV Nyerere katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe Septemba 23, 2018. 

Wahandisi na mafundi wakifanya juhudi kubwa za kukivuta kivuko cha MV Nyerere ambacho kilizama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe .Baadhi Wananchi waliofariki dunia katika ajali hiyo walizikwa katika mazishi yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye kijiji cha Bwasa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.