Habari za Punde

Zao la Pilipili Hoho Lilikuwa Likizalishwa Kwa Wingi Zanzibar.Na Khadija Khamis –Maelezo  24/9/2018
Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema zao la pilipili hoho lilikuwa likizaliswa kwa wingi hapa Zanzibar kwa kipindi kirefu na lilipotea kutokana na kukosekana soko la uhakika la bidhaa hiyo .
Hayo aliyasema kwa niaba ya Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe.Balozi Amina Salum Ali huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani  wakati akijibu suala la Mhe. Hidaya Ali Makame Viti Maalum Wanawake aliyetaka kujua kwa nini zao hilo limepoteza hadhi yake .
Alisema kukosekana kwa soko la uhakika la zao la hilo  kwa kipindi kilichopita zao hilo lilipotea katika mazao ya biashara ambayo yalikuwa yanazalisha vizuri kwa Zanzibar .
Aidha alisema Shirika la Biashara la Taifa la ( ZSTC ) hivi karibuni limekuwa likichukua juhudi kuhakikisha zao hilo linalimwa kwa wingi pamoja na kufanyiwa usarifu kwa zao hilo na mazao mengine ya viungo  kwa kuyaongezea thamani na kuyatafutia masoko ya uhakika.
Alieleza Shirika kupitia katika  mikutano ya wakulima na wadau wa karafuu na mazao ya viungo limekuwa likitoa elimu mbali mbali kwa wakulima hao ambayo inahusiana na umuhimu wa uzalishaji wa mazao ya viungo .
Hata hivyo alisema Wizara kwa kupitia shirika la biashara limeanza kununua na kuuza zao la pilipili hoho pamoja na bidhaa nyengine ambazo zinazalishwa hapa Zanzibar zikiwemo mdalasini,  pilipilimanga pamoja na pilipilihoho .
Naibu waziri huyo alisema katika bajeti ya mwaka 2017 hadi 2018 shirika limenunua bidhaa za pilipilihoho, pilipilimanga, pamoja  na mdalasini zenye thamani ya TZS 14,850.000 ili kuwapa moyo wakulima kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi .
“uhamasishaji na usajili kwa wakulima wa mazao ya viungo husaidia kuengeza nguvu ya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa lengo la kuongeza ubora wa mazao ya viungo ambayo yatakidhi haja ya shirika pamoja na soko kwa ujumla “alisema Mhe.Hassan.
Alieleza shirika la ZSTC limeweza kuhamasisha wakulima mbali mbali katika mkoa wa kusini Muungoni Kitogani pamoja na Bweju na eneo tayari limeshatengwa kwa shughuli ya upandaji wa mazao hayo na kwa upande wa Pemba wilaya ya Mkoani, Chakechake na Wete tayari elimu hiyo imeshatolewa kwa wakulima hao.
Aidha alisema mazao ya viungo kwa Zanzibar ni kivutio kikubwa kwa watalii ambao wanaingia nchini jambo ambalo linaipatia kipato serikali hivyo shirika inajitahidi kuvifunga katika hali nzuri ambayo inaengeza thamani kwa  kusafirisha nje ya nchi.
Pia Naibu huyo aliwataka wakulima wa zao la viungo ikiwemo pilipilihoho,pilipilimanga  pamoja na mdalasini kulima  kilimo hai chenye ubora na kiwango maalum na kuhakikisha kilimo hicho ni chenye thamani ambacho kitasaidia kuipatia pato serikali .
MWISHO
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.