Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akiwakabidhi zawadi wanafunzi wa St.
Joseph wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa Shule za
Sekondari za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zilizofanyika katika Chuo cha
Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akimkabidhi zawadi mwanafunzi mwenye
umri wa mika 12 wa Shule ya Sekondari Mbezi Inn, Charles Denis wakati wa fainali
za mashindano ya vilabu vya kodi kwa Shule za Sekondari za Mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani zilizofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini
Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akimkabidhi zawadi mwanafunzi bora
wa mwaka 2018 Runi David kutoka Shule ya Sekondari Tumbi wakati wa fainali za
mashindano ya vilabu vya kodi kwa Shule za Sekondari za Mikoa ya Dar es Salaam
na Pwani zilizofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es
Salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akimvisha mmoja wa wanafunzi ambaye
shule yake iliibuka mshindi wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa
Shule za Sekondari za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zilizofanyika katika Chuo
cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
(Picha na TRA)
Na. Veronica Kazimoto. Dar
es Salaam.21
Oktoba, 2018
Fainali za mashindano ya
vilabu vya kodi zilizoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zimefanyika
kwa mafanikio makubwa ambapo zawadi mbalimbali zimetolewa kwa Shule za
Sekondari zilizoibuka na ushindi na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri
katika mashindano hayo.
Fainali hizo zilizofunguliwa
na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilifanyika jana katika
Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Katika
mashindano hayo, Shule ya Sekondari St. Joseph iliibuka mshindi wa kwanza kati
ya shule 28 za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kuzawadiwa runinga, kompyuta
ya mezani, printa, saa ya ukutani, medali, ngao, na cheti.
Shule
ya Sekondari Tumbi imeshika nafasi ya pili ambayo ilijinyakulia kompyuta ya
mezani, printa, saa ya ukutani, medali, ngao, na cheti ikifuatiwa na Shule ya
Sekondari Dar es Salaam ambayo ilipata ngao,
kompyuta ya mezani, saa ya ukutani na cheti.
Kwa
upande wa uwasilishaji mada zinazohusu masuala ya kodi, Shule ya Sekondari
Zanaki iliongoza na kuzawadiwa kompyuta ya mezani, printa, saa ya ukutani,
medali na cheti ikifuatiwa na Kerege ambayo ilijibebea printa, saa ya ukutani
na cheti huku Shule ya Sekondari Misitu ikishika nafasi ya tatu na kuondoka na kompyuta
ya mezani, ngao, na cheti.
Kwenye
kipengele cha Ukusanyaji wa Risiti za Kielektroniki za EFD, walioibuka washindi
ni Shule ya Sekondari Gerezani ambayo ilizawadiwa runinga, fedha taslimu shilingi
1,000,000, cheti na medali. Mshindi wa pili ni St. Joseph iliyojitwalia ngao,
cheti na fedha taslimu shilingi 750,000 ikifuatiwa na Shule ya Sekondari
Benjamini iliyopata ngao, cheti na fedha taslimu shilingi 500,000.
Aidha,
Mwanafunzi Bora wa Mwaka huu katika fainali hizo, alikuwa ni Runi David kutoka
Shule ya Sekondari Tumbi ambaye alijinyakulia laptop, ngao, medali na
cheti.
Kilichofurahisha
zaidi katika mashindano hayo ni ushiriki wa mwanafunzi mdogo kuliko wote mwenye
umri wa miaka 12 Charles Denis kutoka Shule ya Sekondari Mbezi Inn ambaye
alizawadiwa laptop, medali na kikombe cha chai kama motisha kwa wanafunzi
wengine wenye umri kama wake kushiriki mashindano ya vilabu vya kodi.
Kwa
upande wa jambo ambalo halikuwa la furaha lakini baadaye likageuka kuwa la
shangwe ni pale mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Zawadi, Mariam Hussein aliyebubujikwa na machozi
wakati akisimulia kukatazwa kushiriki mashindano hayo na mama yake mzazi, suala
lililopelekea Mamlaka ya Mapato Tanzania kuahidi kumlipia gharama zote za
kidato cha nne ikiwemo ada, jambo lililoibua furaha isiyo ya kifani kwa
washiriki wa fainali hizo.
Fainali
hizo zilizoshuhudiwa na Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere ambaye ndiye aliyekabidhi
zawadi mbalimbali kwa washindi, zilifungwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi Richard Kayombo kwa kuwashukuru walimu, wanafunzi, majaji na kamati
ya maandalizi kwa kufanikisha mashindano hayo.
"Napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru kila mtu aliyefanikisha mashindano haya wakiwemo
wanafunzi, walimu, majaji na kamati nzima ya maandalizi ambayo imejituma
kufanya kazi mpaka usiku ili kuhakikisha kuwa fainali hizi zinafanikiwa,"
alisema Kayombo.
Vilabu vya Kodi vilianzishwa
na TRA mwaka 2008 na mpaka sasa kuna jumla ya vilabu 226 Tanzania Bara vikiwa
na jumla ya wanafunzi 27,250 ambao ni wanachama hai wa vilabu hivyo.
Mashindano ya mwaka huu ni
ya 11 kufanyika ambapo jumla ya shule 50 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani
zilishindanishwa na hatimaye shule 28 kati ya hizo zikafaulu kuingia kwenye
fainali.
No comments:
Post a Comment