Habari za Punde

Takukuru yaagizwa kufanya uchunguzi haraka kwa taasisi 30 kwa kuwepo viashiria vikubwa vya rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeagizwa kufanya uchunguzi wa haraka kwa taasisi 30 ikiwamo Benki Kuu (BoT) kutokana na kuwapo na viashiria vikubwa vya rushwa katika hatua za awali za mchakato wa zabuni na utekelezaji wa mikataba

Pia imeagizwa kufanya uchunguzi kwenye miradi 98 iliyotekelezwa kwa kutumia fedha za umma kutokana na kuwapo kwa viashiria hivyo.

Agizo hilo lilitolewa jana jijini hapa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipopokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka 2016/17.

"Uchunguzi huu uanzie kwenye taasisi zilizo chini ya wizara yangu ikiwamo BoT kwani hii ilitakiwa kuwa mfano katika kutekeleza miradi bila kuwapo viashiria vya rushwa, badala yake imekuwa kinyume," alisema.

Dk. Mpango alisema uchunguzi huo unapaswa kukamilika haraka, huku akiitaka PPRA kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha waliohusika na ubadhirifu katika utekelezaji miradi wanachukuliwe hatua.

Waziri huyo pia alimwagiza Katibu Mkuu Hazina kuwaandikia barua maofisa masuhuli wote wa halmashauri na taasisi zilizotajwa kuwa na viashiria vingi vya rushwa, wajieleze kwanini zisichukuliwe hatua za kinidhamu dhidi yao.

"Nawataka maofisa masuhuli wote, makatibu wakuu na wakurugenzi wa wilaya, kuhakikisha wanasoma ripoti hii ya PPRA ili kuwasilisha utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa ndani yake," alisema.

Dk. Mpango pia alimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Dk. Marten Lumbanga, kuhakikisha kuwa ndani ya siku 30 kuzitumia taarifa taasisi zilizotajwa na kuzitaka ziandike kwanini zisichukuliwe hatua kutokana na kufanya ununuzi bila kuzingatia sheria.

Kuhusu usimamizi mbovu wa mikataba, Dk. Mpango alitoa mwezi mmoja kwa watendaji walioingia mikataba hiyo kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuingia mikataba mibovu.

Pia alimtaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuwaandikia na kuchukua hatua kwa wahusika bila kuoneana aibu kwa kuwa ununuzi mbaya unachangia kufuja rasilimali za umma.

Awali akiwasilisha ripoti ya PPRA, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakuruge
nzi ya PPRA (Lumbanga) alisema kuwa katika miradi 98 iliyokaguliwa, taasisi 30 zilibainika kuwa na kiwango cha juu cha viashiria vya rushwa katika hatua za awali za michakato ya zabuni na utekelezaji wa mikataba.

Alizitaja taasisi na mradi iliyokuwa na viashiria vingi vya rushwa kuwa ni Kampuni ya Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (Kidco), Chuo Kikuu cha Mkwawa (Muce), Shirika la Masoko la Kariakoo (SMK) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Zingine ni BoT, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Kampuni ya Reli (TRL), SMK, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Wakala wa Ufundi na Umeme na Mitambo (Temesa), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Bodi ya Filamu Tanzania, Shirika la Umeme (Tanesco) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

"Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Taasisi ya Elimu Tanzania, Bohari ya Dawa (MSD), Shirika la Posta (TPC), Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA), Hospitali ya KCMC na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)," alisema.

Lumbanga alisema taasisi zingine zilizobainika kuwa na kiwango cha juu cha viashiria vya rushwa katika hatua za awali za mchakato wa zabuni na katika utekelezaji wa mikataba ni halmashauri za manispaa ya Singida na Songea, ya Mji wa Korogwe, ya wilaya ya Babati, Bariadi, Musoma, Njombe na Ruangwa.

Alisema viashiria hivyo vimeonekana pia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Lumbanga alisema PPRA pia ilifanya uchunguzi wa tuhuma za ukiukaji wa sheria, taratibu za ununuzi zipatazo sita zilizohusu mikataba 34 yenye thamani ya Sh. trilioni moja, iliyotekelezwa na taasisi sita nchini uliofanyika kutokana na agizo la mamlaka za juu.

"Taasisi zilizofanyiwa uchunguzi huo ni Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Taasisi ya Uendelezaji Tija (NIP), Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Wakala wa Barabara (Tanroads-Arusha) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia," alisema.

UKAGUZI MAALUM

Mwenyekiti huyo alisema PPRA ilifanya ukaguzi maalum kwa taasisi sita katika miradi 29 yenye thamani ya Sh. bilioni 371.97 ambazo ni NSSF, Wizara ya Kilimo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ofisi ya Waziri Mkuu (Programu ya Ushindani wa Sekta Binafsi), HESLB na Muce.

Alisema matokeo ya uchunguzi na ukaguzi maalum huo yalionyesha serikali itapata hasara ya Sh. bilioni 23.7 kutokana na taasisi hizo kushindwa kuzingatia taratibu sahihi za ununuzi na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mikataba.

Alisema serikali itaokoa Sh. bilioni 13.84 iwapo taasisi husika zitatekeleza maelekezo ziliyopewa na PPRA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.