Habari za Punde

Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Mhe. Maudline Castico Akizungumza Wakati wa Hafla ya Mahafali ya Skuli ya Trifonia Academy Fuoni Zanzibar.

Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar Mhe. Maudline Castico akihutubia na kutowa nasaha zake kwa Wanafunzi wa Skuli ya Msingi na Sekondari wa Trifonia Academy Fuoni, akimuwakilisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Juma Pemba. 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Riziki Pembe Juma amezitaka skuli binafsi kuhakikisha zinaunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa Elimu bora itakayosaidia kuengeza wataalamu wazalendo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri huyo, katika mahafali na sherehe za miaka 20 toka kuanzishwa kwa skuli Trifonia academy, zilizofanyika meli tano Fuoni Wilaya ya Magharibi "B", Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Mhe. Maudline Cyrus Castico alisema Serikali inathamini mchango unaotolewa na sekta binafsi katika kuimarisha elimu pamoja na kusaidia kuongeza wataalamu.

Hata hivyo, alisema ili malengo hayo yatimie, walimu hawana budi kujitolea katika kuwalea na kuwasomesha vizuri wanafunzi wao.

Aliwashauri walimu kuhakikisha wanajifunza mbinu mpya za ufundishaji ambazo zitawasaidia wanafunzi hasa kwa masomo ya sayansi ambayo yanakimbiwa na wanafunzi wengi.

"Jitahidini kuzalisha vibaji vingi vyenye uwezo na utaalamu wa kuingia katika ushindani soko la ajira hasa kwa upande wa masomo ya sayansi". alisema.

Alisema Seeikali inaendeleza juhudi za utatuzi wa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya elimu, ikiwa ni upatikanaji wa walimu wa sayansi pamoja na kuimarisha maslahi yao.

Aliwahimiza walimu kujenga utamaduni wa kubadilishana ujuzi pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao, wazazi na wazazi.

Alitoa wito kwa skuli binafsi kufuata utaratibu wa usajili ukataji leseni kwa wakati kwani wizara haitomvumilia mmiliki wa skuli ambayo haijasajiliwa.

Nae Mkurugenzi wa skuli ya Trifonia academy ambae ndio mmiliki wa skuli hiyo, Bi Grace Peter  Myamba, aliwashauri wadau na washirika wa maendeleo kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na skuli binafsi jambo ambalo litasaidia kupunguza kiwango cha fedha zinazotolewa na wazazi na walezi kwa ajili ya ulipiaji wa ada.

Mapema akitoa risala ya skuli hiyo alisema jumla ya wanafunzi Aroubaini na Sita (46) wamehitimu masomo ya kidato cha nne na wanafunzi sabiini na mbili (72) wamehitimu masomo ya Std VI ambao wote kwa ujumla watapatiwa vyeti vyao vya kumalizia masomo yao.

Pia alitoa wito kwa taasisi husika kuwawekea matuta skulini hapo kwani licha ya mafanikio ya kujengwa barabara mpya ya Fuoni Mambosasa kumekuwa na changamoto ya waendesha vyombo vya moto kwa wanafunzi wa skuli hiyo wakati wakukatiza barabara hiyo.

Wakati huo huo, Waziri Castico, alisema Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa utupaji watoto wachanga.

Alisema hayo wakati akizungumza na walimu, wazazi, walezi na wanafunzi, Meli tano Fuoni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.

Alisema vitendo hivyo ambavyo vinajitokeza siku hadi siku na kuleta athari kwa watoto, vinapaswa kuthibitishwa kwa wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha alisema ni jambo la busara kwa jamii kuhakikisha inaungana na Serikali kupambana na watu wenye tabia mbaya ya kuwatupa watoto.

Aliwaomba madiwani, masheha na wananchi kushirikiana na Serikali katika kuwafichua wanawake wenye tabia hiyo.

Alisema ni wakati wa jamii kuwa mabalozi wema wenye kufuatilia kwa karibu mwenendo wa watoto pamoja na wajawazito walio kwenye familia zao ili kuthibiti wimbi hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.