
Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani, kulia akiongea na Wananchi pamoja na kutoa maelekezo kwa viongozi wa TANESCO na REA katika eneo la Bulengahasi lililopo Kata ya Katoro Mkoani Geita baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya shuguli za usambazaji umeme eneo hilo. Kushoto kwake ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Mhandisi Joaquim Ruweta.
Na.Yasini Silayo , GEITA
Waziri
wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani akiwa Mkoani Geita, jana
Novemba 25 amesema kuwa, kasi ya utekelezaji wa jukumu la kusambaza na
kuunganisha wananchi na huduma ya umeme kwa maeneo ya Mijini na Vijijini kote
Nchini ni ile ile ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya Nishati ya
umeme inatumika kuchochea na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na huduma za
kijamii Nchi nzima.
Sisi
Kama Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na
Wakala wa Usambazaji Nishati ya Umeme Vijijini (REA) tumeendelea kusimamia na
kutekeleza jukumu la kusambaza na kufikisha huduma za umeme kila pembe ya Nchi
ikiwa ni Mijini na Vijijini” Alisema Waziri Kalemani.
Aliongeza
kuwa hivi sasa Wizara kupitia TANESCO na REA wanaendelea kutekeleza miradi ya
usambazaji umeme Vijijini, lakini umeme huo unasambazwa kwa kasi ile ile maeneo
ya mijini ikiwemo mitaa yenye makazi mapya na ile ya zamani ambayo ilikuwa bado
hayajafikiwa na huduma za Umeme kupitia TANESCO yenye jukumu la kusambaza
huduma hiyo katika maeneo ya Mijini.
Alibainisha pia katika kuimarisha zaidi
mpango wa usambazaji umeme vijijini serikali imeanza maandalizi ya kutenga
fedha maalumu zitakazotumika kuchochea kasi ya usambazaji umeme maeneo ya
mijini.
Akiwa
katika mji mdogo wa Katoro eneo la Bulengahasi Mkoni Geita, alitoa Rai kwa
TANESCO na Wakandarasi wanaotekeleza
miradi ya umeme kuongeza kasi ya kusambaza na kuunganisha wateja na huduma ya umeme ambapo alitoa siku
kumi kwa TANESCO kuhakikisha mitaa na vitongoji vingi zaidi vya eneo la katoro
vinaunganishwa na umeme hivyo kuimarisha huduma za kijamii pamoja kuchochea
maendeleo ya wakazi wa maeneo hayo.
Aidha
waziri Kalemani, mbali na kuagiza Wakandarasi, TANESCO na REA kuharakisha
shughuli za usambazaji umeme. Pia aliwasisitiza na kuwahamasisha wananchi
kuunganisha umeme pindi miundombinu hiyo inapofika katika maeneo yao.
Waziri
alieleza kuwa serikali imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kila mwaka katika
kuhakikisha umeme unasambazwa na kuwafikia wananchi wote na kwa bei nafuu,
hivyo ni vyema wananchi wakachangamkia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi kwa
kuunganisha umeme na kubuni miradi mbalimbali inayotumia umeme kujiingizia
kipato.
Kwa
upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO aliyeambatana na Waziri
katika ziara hiyo, Mhandisi Theodory Bayona, alielezea kupokea na kutekeleza
maelekezo na maagizo yote kulingana na ilivyoelekezwa na Waziri katika ziara
hiyo lakini aliongeza pia mbali na kufikisha umeme mapema, TANESCO Itaendelea
na juhudi za kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuunganisha umeme pindi
miundombinu inapofika katika maeneo yao na kuhakikisha wananchi wote
wanaostahili kuunganisha umeme wanaunganishwa ili kuongeza idadi ya wateja wa
Shirika na hivyo kuongeza zaidi mapato ya Shirika kupitia mauzo ya umeme.
Naye
Mwananchi mmoja Mkazi wa Kijiji cha Mapinduzi kilichopo kata ya Buseresere
Wilayani Chato aliyehudhuria katika mkutano wa Waziri kijijini hapo na
aliyejitambulisha kwa jina moja la Vedasto, aliishukuru Serikali kwa kuwajali
wananchi na kuwafikishia huduma ya umeme mpaka kijijini hapo.
Alisema kuwa
umeme umekuja na matumaini mapya ya kimaendeleo kijijini hapo na tayari
wameanza kujipanga kubuni na kuanzisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo
zinazotegemea umeme kujiingizia kipato tofauti na hapo awali ambapo walikuwa
wakitegemea zaidi shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji pekee.
Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani, kulia akiongea na Wananchi pamoja na kutoa maelekezo kwa viongozi wa TANESCO na REA katika eneo la Bulengahasi lililopo Kata ya Katoro Mkoani Geita baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya shuguli za usambazaji umeme eneo hilo. Kushoto kwake ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Mhandisi Joaquim Ruweta.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiendelea na kazi ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya kusambazia umeme katika kijiji cha mapinduzi kilichopo kata ya buseresere Wilayani Chato Mkoani Geita. Kushoto ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Mhandisi Joaquim Ruweta na Kulia ni Diwani wa Kata ya Buseresere Bw. Godfrey Fulko
No comments:
Post a Comment