Habari za Punde

Kongamano la Kimataifa la Pili la Kiswahili Kufanyika Zanzibar.

*Baada ya kuvuma kwa kishindo mwaka 2017, Baraza la Kiswahili la Zanzibar 2018 mwendo mdundo. Hakuna kulala mwaka huu BAKIZA. Kwa kuwashirikisha wapenzi wa Kiswahili kutoka nchi mbalimbali BAKIZA limeandaa kongamano la pili la Kiswahili la KIMATAIFA litakalofanyika katika visiwa vya Marashi ya Karafuu; yaani Zanzibar.*

*Kongamano litafanyika tarehe 12 na 13/12/2018, ambalo litajumuisha mijadala mbalimbali inayohusu maendeleo ya Kiswahili,changamoto,tathmini,mielekeo na maazimio juu ya kukuza na kuhifadhi lugha ya Kiswahili na utamaduni wake kupitia isimu na fasihi. Halikadhalika, mijadala itachambua kinagaubaga masuala yanayohusu uandishi na uchapishaji wa kazi mbalimbali za Kiswahili ikiwemo Riwaya,tamthilia,  ushairi na taaluma nyengine*

*Wachapishaji mbalimbali watakuwepo wakiwemo E&D VISSION PUBLISHER, UJUZI BOOK PUBLIDHER, EDY PUBLICATION COMPANY LIMITED, OXFORD UNIVERSITY PRESS DAR ES SALAAM, MKUKI NA NYOTA PUBLISHER, TPH na EDUCATIONAL PUBLISHER. Njoo uonane nao utafahamu mengi kuhusu Uandishi na Uchapishaji*

*Mbalimbali na hayo, umeandaliwa Usiku wa Mswahili. Usiku ambao utakubembeleza, kukuliwaza na kukupoza machofu ya mchana ya mijadala ya kongamano kwa kukuletea igizo linalotoa taaluma  ya lahaja, ngoma za asili ya Kiafrika kama vile Kidumbaki, Msewe na Gonga zitazoonesha mitindo, mbwembwe na minenguo ya utamaduni wake Kiafrika .Vilevile imekuandalia Sehemu ya Ukumbi wa Ana kwa Ana wa dakika 60 baina ya magwiji wa Uandishi wa hapa Tanzania akiwemo, Bw. Shafi Adam Shafi wa Mtoto wa Mama, Profesa Said Ahmed Mohamed wa Nyuso za Mwanamke, Mohamed Suleiman Mohamed wa NYOTA ya Rehema*

*Njoo tufaidike, Njoo tufurahike, Njoo tukuze na kuendeleza Kiswahili*

*Karibu Tanzania, Karibu Zanzibar*

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.