Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Abdallah Mabodi Amaliza Ziara Yake na Kufanya Majumuisho leo.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na Watendaji wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya za Unguja katika Mkutano wa Majumuisho ya Ziara zake za kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Taasisi hizo.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na Watendaji wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya za Unguja katika Mkutano wa Majumuisho ya Ziara zake za kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Taasisi hizo.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa Zanzibar Mwl.Kombo Hassan Juma, akizungumza katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara ya Dk.Mabodi katika Manispaa na Halmashauri za Wilaya Unguja.
MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa ufafanuzi wa hoja mbali zilizotolewa katika Mkutano huo wa Majumuisho.
BAADHI ya Watendaji wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya za Unguja wakisikiliza maelekezo ya hotuba ya  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi katika Mkutano wa Majumuisho uliofanyika katika Kisiwandui, Afisi Kuu ya CCM Zanzibar. 


Na.Is-haka Omar - Zanzibar. 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimebainisha kuwa endapo vikundi vya Ujasiriamali vitajengewa mazingira rafiki ya kupewa mitaji na mikopo yenye masharti nafuu itasaidia kuendelea  kuwainua wananchi kiuchumi. 

Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi katika majumuisho ya ziara zake katika Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri za Wilaya  na Mabaraza ya Manispaa za Unguja. 

Majumuisho hayo yaliyofanyika Katika ukumbi wa Mikutano wa Kamati Maalum ya NEC huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, Dk.Mabodi amesema sekta ya Ujasiriamali inategemewa na wananchi wengi kutokana na kuwa ndio sehemu rahisi ya wananchi kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. 

Ametoa wito kwa wananchi kuchamkia fursa za mikopo iliyopo Wizara ya Kazi, Uwezeshaji ,Wazee, Wanawake na Watoto ili wajikwamue kiuchumi.

Ameeleza kwamba wakati umefika wa serikali Kuu na Serikali ya Mitaa 
nchi kuvipa kipaumbele kwa kuviwezesha vikundi vya ushirika kupitia mfumo wa ugatuzi viweze kujitegemea na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyotoa ajira kwa wingi kwa vijana. 

Ameziagiza Manispaa na Halmashauri za Wilaya kuwasimamia Maafisa Ushirika watoe elimu na kuwahamasisha wananchi wajiunge na vikundi vya ushirika waweze kukopeshwa fedha kwa masharti nafuu.

Katika maelezo yake Dk. Mabodi amesema Wizara ya Kazi, Uwezeshaji ,Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar wanazo fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.1 zinazotakiwa kukopwa na wananchi kupitia vikundi mbali mbali vya ushirika. 

"Kila mwaka Serikali inatenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, lakini wanaokopa ni kidogo jambo linalosababisha fedha nyingi zirudi Serikali kuu bila ya kutumiwa na walengwa hivyo watendaji wa Wizara husika pamoja na Maafisa Ushirika watoe elimu ya kutosha kwa jamii",amesema Dk. Mabodi. 

Kupitia Majumuisho hayo Dk.Mabodi amekemea baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Chama kuacha tabia ya kuwagawa kisiasa watendaji wa Serikali za Mitaa na watakapobaini mapungufu katika utendaji wa Sekta hizo wafuate taratibu husika ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo. 

Pia amewataka baadhi ya viongozi na wanachama kuacha tabia za makundi ya kudhoofisha juhudi za CCM,na badala yake Watumie muda mwingi kuwaeleza wananchi mambo mema yanayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Akizungumzia ugatuzi Dk.Mabodi amesifu mfumo huo wa kuzipa nguvu na maamuzi Serikali za mitaa zipekeleke huduma bora kwa wananchi na kusema kuwa ugatuzi imetatua kwa kiwango kikubwa changamoto za wananchi. 

Pamoja na hayo amezipongeza Manispaa na Halmashauri kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na kuziagiza zifanyie kazi kwa wakati mapungufu mbali mbali yaliyojitokeza katika mfumo wa ugatuzi hasa kwenye nyanja za Elimu, Ukusanyaji wa mapato,Afya ,Kilimo pamoja na Mifugo. 

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa Zanzibar Mwl.Kombo Hassan mesema CCM itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kuwapelekea wananchi huduma bora zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab amesisitiza ushirikiano baina ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kusimamia vizuri mfumo wa ugatuzi ili uende sambamba na matakwa ya wananchi.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Garos Nyimbo amezitaka Taasisi hizo  kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya mfumo wa ugatuzi ili wachangamkie fursa zinazopatikana kupitia utaratibu huo.

 Akichangia hoja juu ya masuala ya kiutendaji kwa Taasisi hizo, Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Amini Salmin Amour, amezishauri Manispaa na Halmashauri zote nchini kuweka mifumo imara na ya kisasa katika ukusanyaji wa kodi kwa lengo la kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato.

Pia  MNEC Amini, amewataka watendaji wa Taasisi hizo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na waanzishe mfumo maalum wa kielectroniki wa kuhifadhi kumbukumbu zote za vyanzo vya mapato pamoja na miradi yote ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohusu taasisi hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi  Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud  amesema changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika Manispaa zote zilizomo katika Mkoa anaoungoza atahakikisha zinafanyiwa kazi kwa haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.