Habari za Punde

Kongamano la Kimataifa la Kiswahili Kufanyika Kesho Zanzibar Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt,Mohamed Seif Khatib akionesha kitabu cha Mtoto wa Mama kilichotungwa na Mtunzi mashuhuri Shafi Adam Shafi kwa  Waandishi wa Habari ambacho kinatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein  katika  Kongamano la Pili la Kimataifa la kiswahili litakalofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil 12-12-2018 Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt,Mohamed Seif Khatib akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Kongamano la Pili la Kimataifa la kiswahili litakalofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika mkutano wa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuhusiana na Kongamano la Pili la Kimataifa la kiswahili litakalofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil


Na Miza Kona  Maelezo – Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika kesho katika ukumbi wa Sheikh Abdulwakil Kikwajuni mjini Zanzibar.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa la Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dkt. Mohammed Seif Khatib amesema Kongamano hilo litajadili fursa na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika Lugha ya Kiswahili sambamba na kubadilishana uzoefu.
Mwenyekiti huyo ameelezaa kuwa zaidi ya watu 200 kutoka nchi mbalimbali watashiriki katika kongamano hilo ambapo mada mbalimbali za fasihi zitajadiliwa.
Amesema katika kongamano hilo pia Washiriki watapata fursa ya kulitatathmini kongamano lililopita mwaka jana na kuzinduwa kitabu cha Mtoto wa Mama kilichotungwa na mwandishi maarufu wa Riwaya Shafi Adam Shafi.
Ameongeza kuwa Kongamano litatoa nafasi ya kuwatunza na kuwapa heshima Waandishi maarufu wa vitabu vya Riwaya na kutunukiwa Vyeti kwa mchango mkubwa walioutoa kwa jamii katika kutunga vitabu vyenye mantiki ya Kiswahili.
Aliwataja watakaopewa Vyeti kuwa ni pamoja na Marehemu Shafi Adam Shafi (KULI) Mohamed Said Abdalla (Bwana MSA), Mohamed Suleiman Mohamed (KIU na NYOTA YA REHEMA) na Said Ahmed Mohamed (ASALI CHUNGU).
“Hawa wote ni wazaliwa wa Zanzibar na tunaamini sisi kwamba ni waandishi bora wa riwaya ya Kiswahili Zanzibar na Baraza litawatunuku vyeti kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika uandishi”, alifahamisha Mwenyekiti huyo.
Aidha pia Baraza litawatunuku vyeti baadhi ya watunzi wa mashairi walioweka majina makubwa katika kukitunza Kiswahili  akiwemo bwana  Masauni Yussuf Masauni, marehemu Seif Salum, marehemu Bakar Abeid, marehemu Hijja Saleh Hijja na marehemu Idd Farahani.   
Kongamano hilo ni la siku mbili ambalo litawashirikisha wataalamu, walimu na wanafunzi kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwandwa, Nchi za Ulaya, Misri, Japan, Tanzania Bara na Australia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.