Habari za Punde

Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahmoud Asisitiza Utoaji wa Huduma Bora Kwa Watalii Zanzibar.

 
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt. Abdalla Mohamed Juma,kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizindua program ya kuwajengea uwezo wanawake juu ya masuala ya utalii Zanzibar iliyoandaliwa na NVCT huko hoteli ya Zanzibar Paradese Amani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa kampuni ya New vision consortium Trainers(NVCT) Pili Khamis akizungumza katika mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.

Baadhi ya washiriki kutoka kampuni mbali mbali za masuala ya utalii, vyuo vya utalii pamoja na wajasiriamali katika sekta za utalii wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi.(Picha na Is-haka Omar-Zanzibar).

Na.Is -haka Omar -Zanzibar.
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema suala la huduma bora kwa wateja bado ni changamoto katika Sekta ya utalii jambo linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu na wadau mbali mbali katka sekta hiyo.
Changamoto hiyo ameibainisha leo(Jana) katika ufunguzi wa Mafunzo ya  kuwajengea uwezo wanawake wazitumie fursa zilizomo katika sekta ya utalii yaliyoandaliwa na Kampuni ya NVCT huko Hoteli ya Zanzibar Paradese iliyopo Amani Wilaya ya Mjini Unguja.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri huyo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt. Abdulla Mohamed Juma alisema wageni wanapokuja Zanzibar kwa ajili ya utalii jambo la mwanzo wanaloliangalia na kudadisi ni huduma bora za mapokezi pamoja na huduma zingine muhimu zinazopatikana katika maeneo wanayokuja kutembelea zikiwemo ulinzi na usalama pamoja na historia halisi ya vivutio vya utalii.
Kupitia ufunguzi huo Katibu huyo aliwasihi wadau mbali mbali katika Sekta hiyo ambao ni kampuni za utalii, milango mikuu ya njia za usafiri wa anga na baharini pamoja na hoteli mbali mbali zinazohusika na utalii kuhakikisha wanawapatia mafunzo endelevu ya huduma kwa wateja watendaji wao ili wageni waridhike na mapokezi na huduma wanazozipata pindi wanapokuwa nchi.  
"Sekta ya utalii ndio sehemu pekee inayotegemewa na Zanzibar katika kukuza Uchumi wa Zanzibar kutokana na kuingiza fedha nyingi za kigeni, hivyo ni lazima wadau katika sekta hiyo tuwe wabunifu wa kufanya vitu wageni wateja wetu ambao ni watalii wa ndani na nje ya nchi.", alisisitiza Dkt. Abdalla.
Alisema wanawake ni miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kunufaika na fursa zilizomo katika Sekta ya utalii zikiwemo kutembeza watalii na kujiajiri kupitia fursa zinazopatikana katika utalii.
Alieleza kuwa ni muda mwafaka kwa wanawake nchini kuchangamkia fursa zinazopatika katika sekta ya utalii ili wajiajiri wenyewe na kuanzisha kampuni zitakazoweza utengeneza ajira nyingi kwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Alisema watalii wengi wanaokuja nchini wanavutiwa kuwaona wanawake wa kizanzibar wakiwa katika mavazi yao halisi wakifanya kazi katika maeneo ya utalii zikiwemo mitindo na ubunifu wa mavazi ya asili, upishi, ufumaji, upakaji wa hina pamoja na kutembeza watalii.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia kama nyenzo ya kubadilisha changamoto za vikwazo kwa wanawake na zikawa fursa za kudumu katika kuzitumia ipasavyo, fursa zinazopatikana katika Sekta ya Utalii.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sera ya utalii imepanga kuwapatia mafunzo mbali mbali wanawake ili waweze kushika nafasi za ngazi za juu za masuala ya utawala na uongozi katika sekta za utalii kama walivyo wanaume.
Amesema kupitia Chuo cha Utalii kilichopo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA),kuna idadi kubwa ya wanawake wanaosomea fani mbali mbali katika Sekta ya utalii na watakapohitimu mafunzo yao wataweza kufanya kazi katika mahoteli na sehemu zingine za utalii kwa lengo la kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.
Amesema mavazi na mitindo ya maisha ya kila siku ya wanawake nchini ni sehemu ya vivutia vya utalii kwani uwepo wa utalii hauna maana ya kubadilisha uhalisia wa maisha, utamaduni na mila za Kizanzibar.
Amesema Serikali imebaini kwamba wanawake wengi wanaoshiriki katika sekta ya utalii wapo mijini hivyo kupitia mabaraza ya utalii ya wilaya wameweka mikakati ya kudumu ya kuhakikisha na wanawake wa maeneo ya vijijini nao wananufaika na fursa zilizopo katika Sekta hiyo.
Pamoja na hayo amesema Serikali imechukua hatua mbali mbali za kudhibiti upotoshaji wa historia ya zanzibar kwa kuhakikisha kila mtembeza watalii binafsi pamoja na makampuni ya kutembeza watalii lazima wawe na vyeti maalum vinavyotolewa na Chuo cha Utalii Zanzibar kwa lengo la kupata watembeza watalii wenye sifa.
Katika maelezo yake Katibu huyo amesema kuanzia Januari mwaka 2019,Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar itazindua Kitabu maalum kinachoelezea Historia halisi ya maeneo yote ya utalii Zanzibar, ambapo watu wote wanaotembeza watalii watatakiwa kufuata muongozo wa kitabu hicho kwa lengo la kuondosha tatizo la upotoshaji wa mhistoria ya vivutio vya utalii nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya New vision consortium Trainers(NVCT) Pili Khamis, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake mbali mbali wa mijini na vijijini ili washiriki ipasavyo katika sekta ya utalii.
Alisema NVCT wamefanya utafiti na kubaini kuwa bado kuna idadi ndogo ya wanawake wanaofanya kazi za kutembeza watalii nchini suala ambalo wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuhamasisha jamii na kutoa mafunzo kwa wanawake waweze kujiajiri kupitia fursa hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mipango na Uendeshaji wa NVCT Ali Hemed Ali, amesema sekta ya utalii nchini inakuwa kwa kasi hivyo ni lazima wanawake wajengewe uwezo ili waweze kwenda sambamba na fursa za ajira zinazopatikana katika Utalii.
Akizungumzia mafunzo hayo ameeleza kwamba yameshirikisha yatakuwa ya siku mbili kuanzia Disemba 1 hadi 2, mwaka 2018 yamewashirikisha wanawake kutoka kampuni za utalii, wanafunzi, wajasiriamali katika sekta za utalii pamoja na watu wenye ulemavu kutoka Mikoa mbali mbali ya Tanzania bara na Zanzibar.
Akizungumza mshiriki wa mafunzo hayo kutoka kampuni ya Mozeti Tours and Safaris Aisha Haji Said, ameelezea matarajio yake kuwa baada ya kupata taaluma ya kuzitumia vizuri fursa zilizomo katika sekta ya utalii ataweza kujiajiri katika masuala ya kutembeza walii.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mjasiriamali wa kampuni ya kutengeneza Icecream Aida Rajab Ali, amesema amekuwa akifanya biashara zake bila mafunzo jambo ambalo limekuwa ni changamoto katika kuziona na kutumia fursa zilizomo katika sekta ya utalii.
Akizungumza Munawar Suleiman Mbarouk kutoka Chuo cha Muna Beuty Academy Urembo Zanzibar,amesema amefurahi kupata mafunzo hayo kwani huduma za masuala ya urembo zinatolewa katika mahoteli mbali mbali ya kitalii hivyo ni lazima wafanyakazi katika fani hiyo wawe na ujuzi wa kutoa huduma bora kwa wateja wao ambao ni watalii.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mwanamitindo wa mavazi mbali mbali Aisha Ally, aliishauri Serikali kuondosha changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya utalii ili watumie vizuri fursa zilizowazunguka kuitangaza zanzibar kupitia masuala mbali mbali yakiwemo mitindo na ubunifu wa mavazi yanayoendana na utamaduni na mila za Zanzibar.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufungwa rasmi na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud mnamo Disemba 2, mwaka 2018.
CAPTION
Picha no.0055-KATIBU Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt. Abdalla Mohamed Juma,kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizindua program ya kuwajengea uwezo wanawake juu ya masuala ya utalii Zanzibar iliyoandaliwa na NVCT huko hoteli ya Zanzibar Paradese Amani Mjini Zanzibar.
Picha no.0012-MKURUGENZI wa kampuni ya New vision consortium Trainers(NVCT) Pili Khamis akizungumza katika mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.
Picha no.BAADHI ya washiriki kutoka kampuni mbali mbali za masuala ya utalii, vyuo vya utalii pamoja na wajasiriamali katika sekta za utalii wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi.(Picha na Is-haka Omar-Zanzibar).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.