Habari za Punde

Kamati za Usimamizi wa Maafa Zashauriwa Kuwa na Mpango wa Kkujiandaa na Kukabiliana na Maafa.

Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, akieleza umuhimu wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa kuwa na Mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa wakati wa Mafunzo ya Usimamizi kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa wakiwa katika Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 2015, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
Mratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Msangi, akieleza umuhimu wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa kuzingatia  Mzingo wa Maafa, ambao ni Kuzuia maafa Kujiandaa na maafa, Kukabili maafa  na kurejesha hali, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Bi Winnie Kijazi, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu (katikati) na Mratibu wa Maafa  Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia majadiliano wakati wa Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa kamati  ya maafa mkoani Rukwa.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa wakiwa katika Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 2015, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.




Na. OWM, SUMBAWANGA.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa maafa nchini kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kuwa na mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa ili kuwa na uwezo wa  utayari wa kujiandaa na kukabili maafa kwa ufanisi.

Akiongea wakati wa mafunzo kwa Kamati ya Usimamizi ya Maafa ya Mkoa wa Rukwa, juu ya Usimamizi wa Maafa kwa Mujibu wa Sheria ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, alifafanua kuwa Mpango huo ni muhimu kwa kuwa huainisha majukumu na hatua zitakazochukuliwa na Kamati za  maafa kuanzia  ngazi ya kijiji, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine wa maafa.

“Ili kuweza kukabiliana na maafa pindi yanapotokea na kuhakikisha kuwa wanazuia au kupunguza athari za maafa yanapotokea kwa ufanisi tumeishauri kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa katika bajeti ijayo watenge bajeti  kwa ajili ya maafa,  pia wabuni mbinu za upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika usimamizi wa maafa,  hili linawezekana iwapo kamati zote nchini za Usimamizi wa maafa  katika ngazi zote zikiwa na Mpango wa kujiandaa na kukabili maafa” alisisitiza Taratibu

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya  Mkoa wa Rukwa , Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Winnie Kijazi, aliihakikishia ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mkoa huo umeamua kuandaa mpango huo kutokana na changamoto walizo zipata wakati wa maafa ya mvua yenye  upepo mkali uliotokea mwishoni mwa mwaka jana katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na Nkasi.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa uratibu na misaada ya haraka pindi tulipopata maafa , na sisi tumeamua kuwa na ufanisi katika usimamizi wa maafa kwa kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili maafa na tutaelekeza wilaya zote kuandaa mipango yao na  kutenga  bajeti kwa ajili ya utekelezaji huo” alifafanua Kijazi

Naye Mratibu wa maafa mkoani Rukwa Aziza Kalyatiilya alieleza kuwa, tayari wameandaa Mpango wa kutoa elimu ya  Maafa  kwa Umma  ili kuijengea jamii uwezo wa kujiandaa, kuzuia, au kukabili na kurejesha hali kwa haraka na ufanisi pindi maafa yatakapotokea mkoani humo.
Mnamo mwezi Desemba mwaka jana Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa zilipatwa na maafa ya mvua yenye upepo mkali iliyosabaisha vifo, uharibifu wa mali na Miundo mbinu. Aidha Kamati ya maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, tayari shughuli za kurejesha hali zinaendelea.

Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha  majukumu ya  kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na  Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji  wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.