Habari za Punde

Shehena ya Kwanza ya Madawati ya Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na Msingi za Zanzibar Yawasili.

Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uhamasishaji wa Uchangiaji wa Vikalio vya Wanafunzi ambae pia ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumisha wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Riziki Pembe Juma wakitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari kuhusu kuwasili vikalio vya Skuli za Serikali za Zanzibar.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati Maalum ya Uhamasishaji wa Uchangiaji wa Vikalio vya Wanafunzi pamoja na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati hiyo Haroun Ali Suleiman alipokuwa akitoa taarifa ya kuwasili awamu ya kwanza ya vikalio kwa ajili ya Skuli za Serikali katika Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini.
Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uhmasishaji wa Uchangiaji wa Vikalio vya Wanafunzi Haroun Ali Suleiman na Makamu Mwenyekiti Riziki Pembe Juma pamoja na Wajumbe wawili wa kamati hiyo Ali Khalil Mirza (kulia) na Naila Majid Jidawi wakiwa wamekalia madawati huko Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini. 
                           Picha Na Miza Othman -Maelezo Zanzibar.

Na.  Khadija Khamis Maelezo Zanzibar.
Jumla ya seti 22,000 za vikalio ikiwa ni awamu ya kwanza ya viti na meza 44,620 zilizonunuliwa na Serikali ya Zanzbar na kugharimu shilingi bilini 2.96 vimewasili nchini kutoka China kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za sekondari.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini, Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uhamasishaji wa Uchangiaji wa Vikalio vya Wanafuzi ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kazi za usambaji wa samani hizo itaanza mwezi ujao.
Alifahamisha kuwa awamu ya pili wa vikalio 22,620 unatarajiwa kufika Zanzibar Mwezi Februari 2019 na kukamilisha idadi ya viti na meza 44,620 ambavyo vitawawezesha wanafunzi wa Skuli za Sekondari 88,520 kuwa na vikalio katika madarasa yao kwa utaratibu wa mikondo miwili.
Hata hivyo Mwenyekiti Haroun alieleza kuwa pamoja na kupatikana kwa vikalio hivyo bado kutakuwa na upungufu wa vikalio 17,950 kwa Skuli za Sekondari kwa utaratibu wa mikondo miwili ya masomo.
Aliongeza kuwa Kamati Maalum ya kuhamasisha uchagiaji wa vikalio inakusudia kununua madawati ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu hivi karibuni kwa lengo la kuondosha tatizo la vikalio.
Alisema katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya vikalio na shilingi milioni 465.8 zilizobakia katika michango iliyotolewa hapo awali na wachangiaji mbali mbali na kufikia shilingi bilioni 3.36 kwa ununuzi wa vikalio.
Mwenyekiti Haroun alisema mwaka 2017, Serikali iliunda Kamati maalum ya uhamasishaji wa uchangiaji vikalio vya wanafunzi yenye wajumbe 11 wakiwemo Mawaziri wanne, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wafanyabiashara maaarufu ili kukabiliana na upungufu wa vikalio maskulini.
Alisema jukumu kubwa la Kamati hiyo ni kuwahamasisha Wafanyabiashara viongozi mbali mbali, Wafanyakazi, wananchi na wahisani mbali mbali kuchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vikalio kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za Serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Riziki Pembe Juma amezitaka Kamati za Skuli kushirikiana na Walimu na wazazi kuhakikisha madawati hayo yanalindwa na kutunzwa vizuri ili yaweze kudumu muda mrefu.
Alieleza matarajio yake kuwa kwa vile madawati hayo yanapelekwa katika skuli za sekondari zenye wanafunzi wanaojielewa watafanya juhudi maalum na iwapo atatokea mwanafunzi kufanya uharibifu wa makusudi atalazimika kulipa.
Mfuko wa Madawati umekusanya shilingi bilioni 1.37 na kupitia fedha za mfuko wa Bandari uliingiza shilingi bilioni 2.5 na kufanya jumla ya shilingi bilioni 3.84 ambazo zimetumika kununua vikalio vya viti na meza 44, 620 kutoka Kampuni ya Guangzhou Everprety Furniture ya China.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.